Mtafiti aanika Ziwa Victoria limejaa tani 150 za plastiki

29Jul 2021
Anthony Gervas
Mwanza
Nipashe
Mtafiti aanika Ziwa Victoria limejaa tani 150 za plastiki
  • Samaki asilimia 20 wamemeza plastiki
  • Wakubwa & wadogo wamezana balaa

ZIWA Victoria ni moja ya vyanzo muhimu kiuchumi na biashara katika jiji la Mwanza. Pia, ni kituo nyeti cha uwekezaji katika Kanda ya Ziwa.

Uchafu plastiki katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza. PICHA: ANTHONY GERVAS.

Unapotaja utalii, ziwa hilo ni kivutio kikubwa cha wageni wanaoingia jijini humo, penye mandhari ya kipekee kuanzia yanayotajwa kila siku; milima yenye miamba ya mawe makubwa, visiwa mbalimbali vinavyotumika kwa makazi ya watu na shughuli za uvuvi.

Humohumo ziwani, kuna utajiri mwingine unaobeba mazingira na uchumi. Hao ni samaki wa aina mbalimbali wakiwamo sangara na sato, wanyama kama kiboko na mamba, wenye sifa kuishi majini na nchi kavu.

Ziwa hilo hadi sasa linakabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira ndani ya ya maji, kutoka watumiaji wakuu walioko jirani na Ziwa.

UTAFITI

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar-es salaam,(UDSM) Bahati Mayoma, anaeleza uchafuzi wa mazingira uliopo sasa kuwa mkubwa unaoweza kuhatarisha afya na maisha ya watu wanaotumia maji hayo au huduma zake, ikiwamo kupata magonjwa kama vile kansa, kwa kurejea utafiti uliofanywa.

Mayoma anayefanya utafiti, anataja kubaini kuwa chini ya ziwa hilo kumegubikwa na vipande vidogo vya chupa za plastiki zilizozama majini na kusambaa ziwani kote, hata zikatengeneza sakafu ya taka hizo, pamoja na nyavu za kuvua samaki, kama vile makokolo.

Mwanazuoni huyo, anasema utafiti wake wa uchafuzi wa mazingira ya ziwa hilo unaokadiriwa ifikapo mwaka 2050 kama hakuna hatua ya udhibiti, uzalishaji taka za plasitiki utaongezeka zaidi.

Anasema, utafiti unaonyesha hivi sasa kuwa taka za vipande vya plastiki vilivyozama na zilizosambaa chini ya maji ni zaidi ya tani 150, ambazo madhara yake ni makubwa kwa afya na maisha ya binadamu wanaotumia huduma ya maji hayo na viumbe vilivyomo kama samaki.

Mayoma anasimulia kuwa, nyavu za kuvulia samaki na makokolo zinazotelekezwa na wavuvi zinapokuwa chakavu baada ya kutumika, huzama chini ya maji na kuungana na taka za vipande vya chupa za plastiki na kutengeneza sakafu ya taka hatarishi kwa afya na maisha ya watu.

“Kuna taka za vipande vidogo vidogo vya plastiki vimezama chini ya ziwa victoria na kusambaa na zingine kuelea juu ya maji, nyavu za kuvulia samaki na makokolo zinazotelekezwa na wavuvi baada ya kuchakaa na kuzama chini, hivyo vyote vimegeuza chini ya ziwa (Victoria) kuwamo sakafu ya taka,” anaeleza Mayoma.

Kiuchumi, inaelezwa zaidi ya watu milioni 30 wananufaika moja kwa moja na vyanzo vya maji, zikiwamo maziwa makuu.

Anasema, utafiti uliofanyika mwaka 2014 iligundua asilimia 95 katika Ziwa Victoria kuna taka za aina hizo na mwaka 2015 utafiti mwingine nao uligundua samaki waliomo wastani wa mmoja kati ya watano wanabainika kumeza vipande hivyo vya plastiki.

Mayoma anasema, ni uchafuzi wa mazingira unaosababishwa pia na wingi wa kazi Kanda ya Ziwa, akitahadharisha madhara ya plastiki huwa hayashi na zina uwezo wa kudumu miaka 100, iwapo ziatasambazwa ovyo.

Hadi sasa kuna mkakati kitaifa wa kupunguza matumizi yasiyokuwa endelevu katika bidhaa za plastiki. Ni hali inayotajwa kupunguza zaidi uchafuzi wa mazingira.

Nchini, utafiti unaonyesha bidhaa nyingi za plastiki na nyavu za kuvua samaki na makokolo hazielei juu ya maji Ziwa Victoria, bali zinazama.

Katika utafiti mwingine uliofanywa na mtaalamu huyo, umegundua samaki aina ya sangara kila siku wanameza samaki wadogo saba aina ya furu, ambao ni jamii ya sato na kusababisha upungufu wa samaki aina hiyo kwa watumiaji wake.

MBINU MBADALA

Mtafiti Mayoma anataja mbinu mbadala au teknolojia inayoweza kutumika kupunguza uchafuzi wa mazingira ziwani humo au usambaaji wa taka hizo, ni pale wenye viwanda vikubwa na vidogo wanaofanya ubunifu wa kuzalisha upya bidhaa zingine za plastiki zinazotumika mbadala wa kuzitupa.

Anatoa mfano, viwanda vinavyozalisha chupa za maji na juisi za plastiki Kanda ya Ziwa ni vingi na vinatakiwa kuwa na ubunifu mbadala wa kutengeneza malighafi mpya pindi zinapomaliza matumizi ya awali, ili kuongeza uchumi na faida kwa umma.

Mbinu nyingine ni watoto kufundishwa usafi wa mazingira, waweze kuepuka utupaji ovyo wa taka, kupitia wadau wa mazingira wanaposhirikiana na serikali na taasisi za kiraia, wameshaanzisha kampeni ya usafi wa mazingira nchini.

Anataja njia nyingine ni kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya utupaji ovyo taka na kusimamia sheria; miongozo ya kudhibiti hali uchafuzi huo; na Ziwa Victoria linategemewa kiuchumi, kibiashara kwa karibu hasa na majirani wa Afrika Mashariki wanaopakana nao.

Mayoma anasema Tanzania inajaribu kuzuia taka kuingizwa katika ziwa hilo kupitia mito, hali kadhalika kuna uchafuzi unaotokea kwa majirani wanaopakana na Ziwa Victoria.

Hadi sasa Tanzania inamiliki asilimia 51 ya Ziwa Victoria, katika ukanda wake ulioko katika Afirika Mashariki na kwamba jamii ndiyo kinara wa rekodi ya utupaji taka.

UCHAFU NYWELE

Hali kadhalika, wadau wa mazingira na uvuvi wanadai nywele bandia za wanawake maarufu rasta, au wigi zinapomaliza muda wa kutumika hutupwa ovyo katika maeneo mbalimbali kisha kusafirishwa na vyanzo vya maji hadi ziwani.

Nywele za kawada watu wanaponyolewa hupelekwa dampo au kutupwa kwenye vyanzo vya maji na baadaye husafirishwa na maji hadi ziwani humo, zinazodaiwa siyo rahisi kuoza, pia ni hatari kwa afya ya binadamu anayetumia huduma za maji hayo.

Mkazi Juvenali Matagili, anaitaka mamlaka ya usafi wa mazingira, kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa kudhibiti utupaji ovyo nywele za binadamu ziwani, ilhali ni vitu visivyooza kirahisi.

"Nywele zinazonyolewa kwa binadamu hutupwa ovyo kwenye vyanzo vya maji, kama vile kwenye mito ambazo haziwezi kuoza kwa miongo mingi, husambaa kisha kusafirishwa na maji hadi ziwani,” anasema.

Mdau huyo wa uvuvi anakiri kuwapo zana za nyavu na makokolo kutumika vibaya katika uvuvi, pamoja na kutelekezwa na wavuvi majini, pale nyenzo hizo zinapochakaa.