Mtafutano Tigray

21Nov 2020
Moshi Lusonzo
Dar es Salaam
Nipashe
Mtafutano Tigray
  • *Dk. Tedros Ghebreyesus ahusishwa
  • *Kamatakamata yaongeza wasiwasi

MGOGORO kati ya serikali ya Ethiopia na waasi wa jimbo la Tigray, unazidi kutanuka na sasa baadhi ya wanasiasa wa ngazi za juu wanahusishwa kufadhili vita.

Mvutano kati ya serikali ya Shirikisho inayoongozwa na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed na uongozi wa jimbo hilo lililopo kaskazini mwa nchi hiyo, ulianza kidogokidogo, lakini sasa hali imekuwa ya kutisha baada ya majeshi kila upande kukabiliana kwa silaha.

Katika hali ya kushangaza, wiki hii mgogoro huo umepata sura mpya baada ya Mkuu wa majeshi ya Ethiopia, kumnyooshea kidole Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, kufanya ushawishi kwa maslahi ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF), kinachopambana na majeshi ya serikali.

Mapaka sasa mamia ya raia wameuawa katika mapambano yanayoendelea ndani ya Tigray, tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Dk. Ghebreyesus anatoka katika jamii ya Watigray na alikuwa waziri wa afya katika serikali iliyopita ya Ethiopia, iliyoongozwa na TPLF.

Hata hivyo, kiongozi huyo hajajibu tuhuma hizo.

Mkuu huyo wa majeshi, Jenerali Berhanu Jula, amewaambia wanahabari kuwa Dk. Ghebreyesus, anafanya kampeni za chini kwa chini kuwasaidia waasi hao kupata silaha.

"Anafanya kila awezalo kuunga mkono chama cha TPLF na kuwasaidia kupata silaha,” amesema bila kutoa ushahidi.

Ameongeza "Hatumtarajii kuunga mkono Waethiopia na kukemea watu hawa. Amekuwa akifanya kila kitu kuwaunga mkono, amefanya kampeni ili nchi jirani zikemee vita. Amewafanyia kazi ili wapate silaha."

Ghebreyesus, alichaguliwa kuongoza WHO mwaka 2017, na jina lake lilijitokeza na kuwa maarufu baada ya kuibuka kwa janga la virusi vya corona.

DK. GHEBREYESUS NI NANI?

DK. Tedros Ghebreyesus, alizaliwa katika mji wa Asmara, ambao wakati huo ilikuwa nchini ya Ethiopia, kabla ya Eritrea kujitenga na kuufanya mji wake mkuu.

Baba yake Adhanom Gebreyesus na mama Melashu Weldegabir, walitoka katika eneo la Enderta awrajja katika jimbo la Tigray.

Dk. Ghebreyesus, anakumbuka mambo mengu magumu aliyopitia wakati akiwa mtoto ikiwamo kumshuhudia mdogo wake akifariki baada ya kuugua ugonjwa wa malaria.

Mnamo mwaka 1986, alipokea Shahada yake ya kwanza Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Asmara. Pia alisoma chuo cha London School of Hygiene & Tropical Medicine cha Uingereza na kupewa shahada ya uzamili ya Sayansi katika eneo la kinga ya magonjwa ya kuambukiza mwaka 1992.

Mwaka 2000, alipata shahada ya uzamivu ya Udaktari wa Falsafa katika afya ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham cha Uingereza.

NI MWISHO WA TPLF?

Mapigano yanayoendelea katika jimbo hilo, pengine itakuwa mwisho wa chama cha (TPLF) baada ya wanachama wake wengi kukamatwa au kukimbilia uhamishoni.

Waziri Mkuu Abiy, hivi karibuni amesema majeshi yanapata ushindi na wanakaribia mji wa Mekelle, ambao ni makao makuu ya Tigray.

Tayari jeshi la polisi kutoka shirikisho limetoa hati ya kukamatwa kwa maofisa 76 wa kijeshi, baadhi yao wanadaiwa kuwa ni wastaafu ambao wanatuhumiwa kushirikiana na TPLF.

Akizungumza na BBC, Billene Seyoum, msemaji wa Waziri Mkuu, amepinga madai kwamba Watigray wanaoishi maeneo mengine wanakamatwa kwa misingi ya kikabila.

Mgogoro huo umeanza muda mrefu kati (TPLF) na serikali kuu ya Ethiopia.

Mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kuahirisha uchaguzi kutokana na janga la corona, lakini TPLF ilichukulia hatua hiyo ya serikali kuu ni batili ikadai kuwa kiongozi huyo hana mamlaka ya kuendelea kuongoza nchi.

Baadae serikali inailaumu TPLF kwa kushambulia kambi ya kijeshi kwa lengo la kuiba silaha, madai ambayo chama hicho iliyakana.

Kiongozi wa TPLF, Debretsion Gebremichael, ambaye ni mzaliwa wa Shire, amethibitisha katika televisheni moja jimboni humo kwamba wanajeshi wake wamepoteza udhibiti wa miji ya Kusini na Magharibi mwa Tigray.

MAJIRANI WAZIDIWA

Nchi jirani zimeanza kutoa wito wa suluhu baada ya kuelemewa na wakimbizi ambao wamekimbilia katika nchi hizo kunusuru maisha yao.

Sudan inasema watu 36,000 wameingia nchini humo kupitia mpaka wa Tigray, wakati mapigano yakiendelea.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya kutokea kwa mzozo kamili wa kibinadamu.

"Huenda kukawa na watu wengi waliokimbia makazi yao ndani ya Tigray, hali ambayo inastahili kuangaliwa wakati tunapojiandaa kuwasaidia kadili ya uwezo wetu," anasema Jens Lark, msemaji wa ofisi ya umoja huo inayeshughulikia masuala ya kibinadamu (OCHA).

MAMBO MUHIMU KUHUSU TIGRAY

Jimbo hilo ndiko kulikuwa na Ufalme wa Aksum, ikielezwa ni sehemu yenye alama ya ustaarabu wa ulimwengu wa zamani.

Kuna wakati eneo hilo lilikuwa na utawala wenye kuvu zaidi kati ya milki za Kirumi na Uajemi.

Magofu yaliyoko ndani ya miji wa Aksum yametambuliwa na Umoja wa Mataifa kama eneo la turathi za kale duniani. Eneo hilo ambalo limekuwepo kati ya karne ya kwanza hadi ya tatu AD, linajumuisha , makasri, makaburi ya wafalme na kanisa linaloaminiwa na baadhi ya watu kuwa sanduku la agano la kale.

Watu wengi katika eneo la Tigray ni Wakristo wa dhehebu la Orthodox Ethiopia. Mzizi wa Dini ya Kikristo ulianza miaka 1,600 iliyopita.

4. Lugha kuu katika eneo hilo ni Tigrinya, lahaja ya Kisemeti ina wasemaji wasiopungua milioni saba ulimwenguni.

5. Ufuta ni zao kuu la biashara, unasafirishwa Marekani, China na nchi nyingine.

Habari Kubwa