Mtaji wa kampuni na masharti yake

26Feb 2016
james kuyangana
Dar
Nipashe
Mtaji wa kampuni na masharti yake

Mara kadhaa katika makala zetu za nyuma kupitia safu hii ya kila Ijumaa, tumewahi kuzungumzia mambo muhimu kuhusiana na sheria za makampuni.

Waziri wa Sheria na Katiba Dk. Harison Mwakyembe.

Kwa sababu kampuni zimetumiwa na wafanyabiashara makini kote duniani kama injini za kujiletea maendeleo ya uhakika na ya haraka, nimeona si vibaya kama ewe msomaji wetu mpendwa ukajiongezea maarifa zaidi ya kibishara katika uelewa wa misingi muhimu inayohusiana na makampuni. Basi kwa sasa leo tuelimishane kuhusiana na dhana ya mtaji wa kampuni.

Sheria yetu ya makampuni ya mwaka 2002 haina tafsiri ya neno ‘mtaji’ kwa maana hivyo basi, maana ya neno hili ni ile ambayo inatambulika katika matumizi ya kawaida ya Kiswahili na katika nyanja ambalo neno hili limezoeleka, hususan katika medani za uchumi, biashara na sheria.

Kwa maana iliyo rahisi kabisa kueleweka na mwananchi wa kawaida tunaweza kusema tu kuwa mtaji ni kile kinachoifanya biashara fulani ianze au kama imeshaanza basi iendelee kusimama pasipo kuyumba. Mtaji waweza kuwa ni fedha ambayo
inapaswa iwepo benki au mfukoni mwa mjasiriamali, mfanyabiashara au mwekezaji ikiwa imetengwa kwa lengo moja tu la kuhakikisha kuwa inatumika katikakunununulia ama kugharimia mahitaji muhimu yanayoifanya biashara husika izidi
kustawi pasipo kukwama.

Mathalan unataka kuanzisha dula la kuuza nafaka wakati ambapo hujafanya chochote, hilo likiwa ni wazo tu kichwani.Kitu cha kwanza kwa kawaida ni kwa wewe kukaa chni na kupiga hesabu ya gharama zote unazohitaji kutumia, mauzo
unayotarajia kupata na hatimaye faida utakayotia kibindoni, yaaani yale masalia baada ya kutoa gharama zote ndani ya mauzo yako.

Katika kupanga huko, utabaini kuwa utahitaji fedha taslimu kununulia bidhaa kwa mkulima, gharama za usafirishaji kutoka unaponununua nafaka husika hadi lilipo duka lako, kodi ya pango, ushuru na ada za kulipwa serikalini, mishahara ama posho za vibarua, muuza duka, mlinzi, na gharama nyinginezo kama umeme na kadhalika.

Utahitaji pia kutenga bajeti za ulipwaji wa kodi, leseni ya biashara, ada za wataalam wa nyaraka na ushauri kama wahasibu, wanasheria, bima, na kadhalika. Hata hivyo, baadhi ya gharama ni za lazima na nyingine zaweza kuwa za hiari, katokana na ukubwa wa mtaji, aina ya biashara, mahali ulipo, uzoefu wako na vigezo vinginevyo.

Gharama hizi zote ni mtaji kwa sababu ni kile unachokiwekeza kama misingi ya kupata kikubwa zaidi baadae. Basi, kwa mtazamo mwingine mtaji ni kama mbegu anayopanda mkulima na gharama nyinginezo kama mboleo, umwagiliaji na kadhalika. Unatumia kiasi fulani ili uje upate kikubwa au zaidi na hata maradufu ya hapo.

AINA ZA MITAJI
Ukitazama hapo juu utagundua kuwa zipo gharama ambazo unapaswa kuingia awali ama mara moja tu na hupaswi kuwa unaingia mara kwa mara, wakati gharama nyingine utaendelea kuzigharimia mara kwa mara. Mathalan, gharama za usajili wa kampuni ama kutengeneza mpango-biashara (business plan) hizi unazigharimikia mara moja tu unapoanza wakati gharama nyinginezo kama fedha unayopaswa kuwa nayo kila mara bidhaa inapopungua ili ukanunulie mali nyingine (fedha ya kuzungushia) unapaswa kuwa nayo muda wote na utagharimia mara kwa mara kwa sbabau, kama bidhaa inamalizika na huna tena amana ya kununulia bidhaa nyingine basi biashara yako itadhoofu na kufa na watu kusema umefilisika.

Mtaji wa aina ya kwanza ambapo unaingia gharama kubwa kuanza biashara ama kampuni hujulikana kwa kimombo kama ‘initial capital’ (mtaji wa awali) ama mtaji wa kuanzia ‘starting capital’ na hapo ndipo kuna changamoto kubwa kwa sababu gharama zinakuwa ni nyingi, kubwa na inakubidi ujitoe mhanga ukitaraji kuwa gharama hizi zitakuwa zinapungua na faida kuongezeka kwa kadri muda navyosonga mbele.

Ikumbukwe mfanyabiashara unastawi na kuaminika, inafikia hatua unaweza kuchukua mzigo kwa ’mali-kauli’ huu nao uikiwa ni mtaji wako wa uaminifu badala ya fedha. Mabilionea wengi wamefika hapo walipo kwa mtaji wa
uaminifu wao pia nawe waweza kuwa mmoja wao, hujachelewa.

Aina ya pili ya mtaji, kama tulivyoona, ni fedha inayopaswa isikauke katika biashara ili kukuwezesha kununulia bidhaa na kugharimia huduma za lazima za kila siku kama umeme na wafanyakazi. Huu hujulikana kama mtaji wa kuzungushia na ki-uhalisia ndio mtaji unaozunguka (kimombo ‘revolving capital’).

Kama ambavyo mkulima anaruhusiwa kula mazao anayovuna shamnbani lakini hapaswi kula mbegu za
kupanda msimu unaofuata, kanuni muhimu ya kibiashara iko hivyo hivyo: Waweza kula faida lakini kamwe usile mtaji. Sharti hili linahusika pia katika taratibu za mitaji ya kampuni.

Jambo jingine muhimu unalopaswa kulitia maanani ni kuwa mtaji si lazima uwe fedha peke yake. Elimu, utaalam ama uzoefu wako au wa mtu mwingine vyote ni mtaji kwa sababu vinaongeza thamani ya kile unachokifanya na hivyo kukuza mapato na kukuzalishia faida kubwa ama kwa haraka tofauti na kama usingekuwa navyo.

Muda, nguvu, ubunifu na jitihada nao ni mtaji muhimu sana na hili limeandikwa vizuri sana na mchumi maarufu kutoka Urusi, Karl Marx katika kitabu chake maarufu kiitwacho Das Kapital (Mtaj’)

Baada ya kutoa utangulizi wa dhana ya mtaji kwa ujumla, tuzungumzie sasa mtaji wa kampuni ni kitu gani na kuna taratibu hizi kuhusiana nayo.

MTAJI WA KAMPUNI NA MASHARTI YAKE
Kwa kawaida mtaji wa kampuni haupaswi kupunguzwa baada ya kampuni kusajiliwa na kuanza ikiwa na mtaji lioainishwa. Hili ni sharti lililowekwa katika hukumu ya kesi maarufu, Trevor v. Whitworth, iliyotolewa umauzi mwaka 1887 huko Uingereza.

Sharti hili liliwekwa ili kulinda haski za wanahisa lakini pia mtaji wa kampuni yenyewe usitetereke na pia kuepusha ampuni isitumbukie katika anguko la kufilisika.

Pili, hisa za kampuni hazipaswi kutolewa mfano kuuzwa kwa punguzo (Discount), yaani chini ya beo ya soko (Rejea hukumu katika kesi ya Ooregum Gold Mining Co.of India Ltd v. Roper (1892)). Lengo ni hilo hilo kulinda mtaji wa kampuni na maslahi ya wanahisa. Sharti hili lilifafanuliwa kwa kina na uamuzi wa mahakama ya Rufaa ya Uingereza katika shauri maarufu la Trevor v. Whitworth (1887), kampuni fulani likuta imenunua baadhi ya hisa zake yenyewe. Mahakama ikatamka kuwa kitendo hicho tafsiri yake ilikuwa ni upunguzwaji wa hisa za awali za kampong na hakikubaliki.

Lakini sharti limelegezwa kidogo, angalia mathalani Sura ya 18 katika Sheria ya Makampuni ya Uingereza ya mwaka 2006.

Linganisha pia na vifungu husika vya Sheria yetu ya Makampuni ya mwaka 2002 (Sheria namba 12). Kampuni inapotokea kutaka kupunguza mtaji, basi sharti Sheria ziwe zimeruhusu na taratibu za kisheria zifuatwe, mathalan mahakama kuidhinisha jambo hilo.

Kwa namna yoyote ile, hata kama yanakuwepo mazingira ya kuruhusu kampuni kupunguza mtaji wake, kikubwa kinachoangaliwa kwanza huwa ni iwapo jambo jambo hiilo litawaathiri wakopeshaji wanaoidai kampuni, na kwa kiasi gani. Rejea kesi ya Scottish Insurance Corporation Ltd v. Wilson & Clyde Coal Co. Ltd (1949).

Katika utangulizi wetu awali, tuliona namna ambavyo mfanyabiashara wa kawaida ambaye hapaswi kula mtaji lakini anaweza kugusa faida. Ndivyo ilivyo pia kwa kampuni. Mtaji wa kampuni kamwe haupaswi kumegwa-megwa lakini inapotokea kuna faida basi gawio laweza kufanywa kwa wanahisa. Msingi wa kuweka sharti la kuzuia mtaji usiguswe ama kugawiwa kwa wanahisa wenyewe awali uliwekwa ili kuwalinda wakopeshaji wa kampuni kama benki, ili wakopeshaji hawa wawe na dhamana ya kuchukua pale kampuni inaposhindwa kulipa deni.

Hata hivyo, kwa uhalisia mtaji wa kampong hautoi kinga thabiti kwa sasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na zaidi ni kwambambajapo haupaswi kumegwa kwa wanahisia bado unaweza kupungua au kuisha kabisa kutakana na namna ulivyotumika katika shughuli za uendeshaji wa kampuni.

Ma-gawio ya aina hii hujulikana kama Dividends. Huu ni utaratibu unaofanyika kwa kampuni binafsi (private companies) lakini pia kampuni yaliyojiorodhesha kuuza hisa zake kupitia masoko ya mitaji, kama ilivyo kwa Soko la Hisa (DSE), hapa Tanzania ambapo ni utaratibu wa kawaida kwa makampuni yenye hisa kutoa gawio kwa wanahisa wake, kila yanapofanya vizuri.

Dhana ya mitaji ya kampuni ni pana na ngumu na inatubidi tuisitishie hapa kwa leo.
Majaliwa, tutazungumzia mada nyingine wiki ijayo.

*Denis Maringo ni Wakili wa Kijitegemea aliyeko Dar es Salaam. Simu: 0719270067; Barua-pepe:[email protected]

Habari Kubwa