Mtihani wa Dk. Magufuli katika kurejesha viwanda

26Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mtihani wa Dk. Magufuli katika kurejesha viwanda

KATIKA mikakati yake, Rais Dk. John Magufuli ameeleza kunuia kwake katika kufufua sekta ya viwanda na hata kuirudishia uhai iliyokuwa nayo tangu zama zilizopita, Tanzania ilipokuwa nchi ya viwanda.

Rais Dk. John Magufuli.

Ni mikakati aliyokuwa akiinadi katika kampeni zake kila alikopita nchini. Sasa ndoto yake ya kuwa rais imetimia na yuko madarakani kwa muda sasa.

Ikiangaliwa kwa kina, kiu ya rais huyo analiangalia taifa katika matazamo wa iliyokuwa zama za awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi, chini ya Baba wa Taifa Rais Julius Nyerere.

Mfumo wa uchumi kitaifa ulipiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda, ikigusa nyanja na sekta nyingi za uchumi ukiwa na mfumo mahsusi ulioanisha namna bidhaa zinazozalishwa shambani, kuwa na mahali pa kuzipeleka, muungano unaoitwa na wataalam wa uchumi ‘backward and forward linkage.”

Tofauti iliyokuwepo wakati huo na anachoktaka kukifanya Rais Dk. Magufuli sasa ni kwamba, mfumo wa uzalishaji na soko ulikuwa hodhi kwa maana ya kusimamiwa moja kwa moja na serikali na ndivyo ilivyo uwekezaji wake.

Hali iliyoko sasa, ni kwamba uwekezaji anaouhitaji Dk. Magufuli sasa unahitaji kutoka kwa vyanzo binafsi na wakati huo huo, soko ni huria kwa uwekezaji huo kukabiliana na ushindani mkali sokoni.

Ushindani huo una sura kuu mbili. Moja ni kutoka sehemu mbalimbali za dunia, pia katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kipindi hiki inatekelezwa itifaki ya soko la pamoja.

Je inapofunguliwa soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya nchini, ni namna gani viwanda vipya vya nchini vimejiandaa katika kupambana katika soko la EAC.

Hilo linamfanya Rais Dk. Magufuli kuwa na wakati wa kuumiza kichwa katika maeneo hayo ingawaje haina maana kwamba hakuna hatua za awali zilizochukuliwa kuimarisha maeneo hayo.

Kwa mfano kuna mikakati ya kisera na kisheria imeshafanyika katika kuboresha mfumo wa kuunda ubia wa sekta binafsi na serikali katika kujenga uchumi (Public and Private Sector Partnership – PPP). Katika uhalisia bado sehemu kubwa ya kupanua sekta ya viwanda.

Mafanikio makubwa ya sekta ya viwanda ambayo yalifikiwa katika awamu ya kwanza ya uongozi, mikakati yake ilianza katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Nchi ya Miaka Mitano ya 1964 hadi 1969.

Ni mpango wa maendeleo ya viwanda ulioanza kwa kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa za matumizi ndani ya nchi na dira ya mpango huo katika sekta nyingine kwa ujumla ilisimama katika mtazamo huo wa kukidhi mahitaj ya ndani.

Ilikuwa kipindi kinachokumbukuwa sana kwa kujengwa viwanda vya nguo nchini, lengo kuu ni kujitosheleza kwa mahitaji ya bidhaa hiyo na zao la matumizi bora ya pamba inayozalishwa kwa wingi nchini. Ilikuwa sehemu mojawapo ya utekelezaji wa “backward and forward linkage programme.”

Leo hii inapozungumziwa viwanda vya nguo vya kihistoria vilivyojengwa nchini katika zama za mpango huo na baadaye, ikiwemo Tabotex (Tabora), Mwatex (Mwanza), Mutex (Musoma) na Urafiki (Dar es Salaam).

Hata ulipoingia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano, suala la maendeleo ya viwanda mtazamo wake ulipanuliwa kutoka kutazama viwanda vya kuzalisha bidhaa za msingi pekee na kuelekea hadi kwenye maendeleo ya viwanda vidogo.

Hoja hiyo ndio inayoelezwa kuwa ilisababisha kuanzishwa kwa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) ambalo lililenga kuhakikisha malighafi yote kitaifa yanatumika katika ngazi zote nchini, baadhi yakikidhi mahitaji ya wananchi waliko.

Pia, mtazamo wa kuanzishwa Sido ulilenga kupanua wigo wa ajira na matumizi bora ya ujuzi wa wananchi mahali waliko na kadhalika.

Mwaka 1976 uliundwa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu- miaka 20 ambao ulilenga Tanzania kuwa na viwanda vya ngazi zote, ikiwemo viwanda mama.

Hata hivyo, mpango huo uliishia njiani baada ya mabadiliko makubwa ya kisera nchini, wakati mfumo wa uchumi ulihama kutoka ukiritimba wa serikali kuendesha uchumi hadi mfumo huria. Ulianza rasmi mwaka 1985.

Katika tafsiri rahisi ni hatua iliyofungua mlango rasmi wa kudorora sekta ya viwanda vya nchini, kutokana na bidhaa zake kuelemewa sokoni na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi, hali iliyoendana na viwanda vya serikali kufa kimoja baada ya kingine.

Sera ya serikali iliingia katika mageuzi makubwa, ikiwemo kujiengua katika shughuli za uzalishaji na kuchukua jukumu la usimamizi wa uchumi na biashara.

Iliundwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), ambayo katika hatua ya kwanza ilianza kwa kubinasisha taasisi zote za umma zinazoendeshwa kwa hasara, japo miaka kadhaa baadaye uamuzi huo uliimarishwa na kuwa kwa taasisi zote za umma.

Kwa bahati mbaya, taasisi hizo za umma zilizobinashwa kwa wawekezaji binfasi ambao wengi walikuwa ni wageni, sehemu kubwa ya viwanda vimekufa na vingine kutoweka kabisa katika uzalishaji na ndio kwenye kilio cha Rais Dk. Magufuli.

Hiyo ndiyo inanfikisha kiongozi huyo katika changamoto ya kufufua viwanda nchini katika mtazamo wenye sura kuu tatu.
Moja ni namna gani atawapata wawekezaji wa kujenga viwanda mbalimbali mbali nchini vinavyofanana na uliokuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka 20, kuanzia mwaka 1976 katika mtazamo wa kukidhi mahitaji ya sasa katika soko.

Maana ule uliangalia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ambavyo ni viwanda mama vitavayofunga milango ya kuangalia nje ya nchi katika ununuzi wa mambo mengi.

Pili, ni namna gani viwanda hivyo tarajiwa vinavyoweza kupasua ukuta wa sioko lenye ushndani mkali kutoa pande zingine za dunia na soko la EAC ambako sasa kunatekelezwa itifaki ya soko la pamoja.

Mwisho kuna mtihani mkubwa wa maboresho ya kisheria na marekebisho mengine ya kuvirejesha katika hadhi ya zamani viwanda vilivyobinafsishwa na PSRC na vikafa au vipo taabani, kurejea uwezo wa zamani.”

Habari Kubwa