Mtoto kuzaliwa utumbo uko nje

06Jun 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mtoto kuzaliwa utumbo uko nje
  • Mabingwa Muhimbili wataja kiini cha ugonjwa na hali ilivyo
  • Mwanza, Kilimanjaro, Dodoma, Tanga na Mbeya vinara

​​​​​​​GASTROSCHISIS ni jina la kitaalamu la ugonjwa wa mtoto kuzaliwa utumbo ukiwa nje.

Wataalamu wa tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wanasema tatizo linalosababishwa na hali ya ukuta wa tumbo kuwa wazi wanaozaliwa nalo watoto.

Matabibu hao wanabainisha kuwa takwimu zinaonyesha kati ya watoto 2,000 wanaozaliwa duniani kote, mmoja ana tatizo hilo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa MNH, Zaituni Bokhari, anasema tatizo hilo limeenea duniani kote na idadi ya wagonjwa inaongozeka kila mwaka.

Anasema katika nchi za magharibi, takwimu zinaonyesha kati ya watoto 2,000 wanaozaliwa, mmoja ana tatizo hilo na katika nchi zilizoendelea ni asilimia nne ya watoto wanaopoteza maisha.

Anasema katika nchi changa watoto kuanzia asilimia 75 hadi 100 wanapoteza maisha, wakati Tanzania asilimia 90 hadi 100 wanaozaliwa na hali hiyo wanapoteza maisha.

Kadhalika, takwimu zinaonyesha wagonjwa 20 hadi 30 kwa mwaka wanatibiwa kutoka maeneo mbalimbali nchini na wengi hufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya.

CHANZO CHA TATIZO

Dk. Zaituni anasema hakuna sababu ya msingi ya watoto kuzaliwa na tatizo hilo isipokuwa kuwapo kasoro kadhaa.

Anasema moja ya kasoro ni mtoto kuzaliwa akiwa hajatimia miezi tisa, akifafanua kuwa anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na tatizo hilo kwa sababu viungo vyake vinakuwa havijakamilika.

Anasema mama mjamzito anapokuwa na magonjwa sugu kama moyo, figo, Ukimwi na sukari yanayomfanya atumie dawa kwa muda mrefu, ni rahisi kuzaa mtoto mwenye hitilafu hiyo.

Hata hivyo, daktari bingwa huyo anaweka wazi kuwa siyo wanawake wote wenye magonjwa hayo sugu wanazaa watoto wenye tatizo hilo hasa wakizingatia masharti ya watoa huduma wa afya wakati wote wa ujauzito.

"Mimi nina msemo wangu wa kuwaambia wanawake wajawazito waangalie nini wanakula, wafikirie kuhusu watoto wao," anasema.

Dk. Zaituni anasema mama mjamzito kuhudhuria kliniki zote kunaweza kuepuka kuzaa mtoto mwenye hitilafu hiyo kwa kuwa kutohudhuria kunasababisha kukosa kupatiwa kinga muhimu za mtoto akiwa tumboni.

KWANINI WENGI HUFARIKI?

Dk. Zaituni anasema nchini watoto waliozaliwa na tatizo hilo, iliaminika hawawezi kupona na hata watoa huduma za afya walikuwa wakiamini hivyo.

Anasema kutokana na kukithiri kwa tatizo hilo, madaktari waliamua kufanya utafiti wa kubaini sababu za vifo kuwa vichache katika nchi zilizoendelea.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, utafiti ulibaini nchi zilizoendelea zina mfumo wa kubaini tatizo tangu mtoto akiwa tumboni kama ana hitilafu katika mwili wake au viungo vyake.

"Wameenda mbali zaidi hata kuanza kumtibu mtoto akiwa bado yupo ndani ya tumbo la mama yake wakati sisi bado hatujafikia hatua hiyo lakini ndiko tunakokwenda," anasema.

Dk. Zaituni anasema utafiti pia ulibaini nchi zilizoendelea zina vifaa vya kutatua tatizo hilo.

Anasema mtoto anapozaliwa na tatizo hilo, anatakiwa kufunikwa utumbo wake kwa kutumia teknolojia maalum (silo bags) iliyotengenezwa na vifaa maalum.

"Kwanza tulibaini watoto hawa wanapozaliwa katika nchi hizo wanakuwa katika mazingira mazuri ya kuwahi kupata matibabu na wanapelekwa kwenye huduma nzuri zaidi," anasema.

Dk. Zaituni anasema pia walibaini watoa huduma wa nchi zilizoendelea wana elimu ya kutosha ya namna ya kumhudumia mtoto mwenye tatizo hilo.

"Nchini kwetu elimu inahitajika zaidi kwa sababu ya mazingira wanakozaliwa watoto hawa kutoka maeneo ya pembezoni ambako hutumia muda mrefu hadi kufika Muhimbili," anasema.

Daktari bingwa huyo anasema katika zahanati, vituo vya afya na hosptali za mikoa ndiko wanakozaliwa watoto hao na hadi kufikishwa Muhimbili wanakuwa katika hatua mbaya.

Anasisitiza elimu inahitajika katika hospitali hizo ili watoa huduma wanapopata mtoto wa aina hiyo wajue nini cha kufanya.

Abainisha kuwa watoto wanaozaliwa na tatizo hilo husumbuliwa na tatizo la upumuaji, hivyo hutakiwa kuwekwa kwenye mashine ya upumuaji na pia hulishwa chakula kwa njia ya mshipa kwa sababu hawawezi kunyonya wala kula chochote.

Dk. Zaituni anasema walifanya utafiti na nchi nyingine za Afrika ambazo ni Malawi, Zambia na Ghana ili kuangalia kwa nini watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje wanakufariki dunia, wakabaini sababu hizo.

Anasema waliomba kufanya mafunzo na madaktari bingwa wa hospitali kutoka nchi zilizoendelea kwa muda wa miaka miwili.

Dk. Zaituni anasema walikubaliwa kufanya utafiti huo kwa kukubaliana kila nchi kuanza kuwahudumia watoto wenye matatizo hayo kulingana na vifaa na namna wanavyoweza kuwapa huduma ili kuona njia ya kusaidia kuwaokoa.

"Kwa Tanzania tulitumia zana za matibabu za ndani ya nchi, tulikuwa tukipokea watoto kutoka Tanga, Mtwara, Morogo na walikifika wakiwa wameshapata maambukizi ya bakteria," anabainisha.

Anafafanua zaidi kuwa watoto hao walikuwa wanapokewa wakiwa wameshapigwa baridi kali kwa sababu wanazaliwa na kusafirishwa.

"Ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa sababu vifaa tulivyokuwa tukitumia hapa Muhimbili, watoto wote waliokuwa wanazaliwa na tatizo lazima wanapelekwa chumba cha upasuaji ili kuhudumiwa na daktari bingwa wa watoto," anasema.

Anabainisha kuwa walikuwa wanatumia mpira wa mkojo wanaowekea wagonjwa ambao uliundwa na kuwa kama begi maalum la kuhifadhia utumbo wa mtoto uliotoka nje.

Anasema kwa sababu vifaa vilikuwa vya kienyeji, mipira ilikuwa inapasuka na utumbo kutoboka na hivyo mtoto kupoteza maisha.

Dakatri bingwa huyo anasema mtoto pia alikuwa akichomwa sindano za usingizi ambazo zilikuwa na madhara kwake kwa sababu bado ni mchanga, hivyo kupoteza maisha.

Kadhalika, alisema kikwazo kingine ni mtoto anapopokewa usiku anakosa daktari bingwa wa kumtibu, hivyo kutumia zaidi ya saa nne kufuatwa nyumbani na kusababisha mtoto kucheleweshewa huduma.

MATIBABU YAKE

Dk. Zaituni anasema baada ya kubaini vikwazo hivyo, kwanza walipatiwa msaada wa mabegi maalum ya kuhifadhia utumbo huo badala ya kutumia mipira.

Anasema pia walianza kutoa elimu kwa watoa huduma wote wa hospitali zote za Mkoa wa Dar es Salaam na wilaya chache za Mkoa wa Pwani ili wanapopata mgonjwa wa aina hiyo, waanze kumpatia huduma sahihi badala ya kumsubiri daktari bingwa.

Anasema baada ya kuchukua hatua hizo, walifanya utafiti mwingine wa kuangalia wanavyotoa huduma bila kumpeleka mtoto chumba cha upasuaji wanapata matokeo gani.

Dk. Zaituni anasema hospitali nyingi sasa zinatoa huduma ya kwanza ya kumtafutia plastiki safi ya kuhifadhi utumbo huo kabla ya kumpeleka Muhimbili.

Anasema awali watoto waliokuwa wanapatikana walikuwa wanajazwa kitambaa cheupe maalum (gozi) kilichojazwa maji maji wakiamini zitasaidia kuhifadhi utumbo huo ili usiwe mkavu.

Anasema njia hiyo ilikuwa ikiujaza utumbo maji na kusababisha joto la mwili la mtoto kupungua na kupata maambukizi ya bakteria.

Dk. Zaituni anasema walitengeneza mabegi hayo maalum ya kuhifadhia utumbo wakayasambaza katika hospitali za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ili kutoa huduma ya kwanza kwa watoto hao.

"Baada ya kumaliza utafiti huo wa mwaka mmoja, tulisadia kuokoa maisha ya watoto kwa asilimia 78 kutoka asilimia 90 hadi 100 waliokuwa wakipoteza maisha," anabainisha.

Anasema baada ya utafiti huo, walipanga kuanza kutoa elimu nchi nzima kwa kuanza na mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Dodoma, Tanga na Mbeya.

Dk. Zaituni anasema waliamua kuanza na mikoa hiyo kwa sababu inaongoza kwa kuwa na watoto wengi wenye tatizo hilo.

"Tuliamua kuanza kutafuta wadhamini ambao wamepatikana watakaofadhili mikoa miwili ya Mwanza na Dodoma, katika kampeni ya 'Okoa Maisha ya Watoto Wanaozaliwa Utumbo Nje'," Dk. Zaituni anahitimisha.

Habari Kubwa