Museveni kuishi miaka 41 Ikulu?

13Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Museveni kuishi miaka 41 Ikulu?
  • *Bobi Wine ‘rais wa ghetto’ kumbabua?

LEO ndio leo siku ambayo maswali hayo yatakapojibiwa. Wapigakura wataamua iwapo Rais Yoweri Museveni, ambaye ni miongoni mwa marais wa Afrika walioongoza muda mrefu atafanikiwa kuitawala Uganda kwa miaka 40.

Akiwa amechukua nchi mwaka 1986 kutoka Chama cha National Resistance Movement (NRM), ameliongoza taifa hilo kwa miaka 35 na endapo atafanikiwa kushinda uchaguzi wa leo na kukaa ikulu kwa miaka mingine mitano ataandika historia ya kuwa rais wa nchi aliyeongoza kwa nusu karne.

Mpinzani wake mkuu ni Bobi Wine au Robert Kyagulanyi Ssentamu, ambaye kwa mara ya kwanza amekuwa tishio kwa kiongozi huyo, anayeamini kuwa ndiye pekee anayeweza kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, anamtikisa akijiita ‘rais wa ghetto’.

Anajiamini kwa sababu anaungwa mkono na vijana wengi aliowahamasisha kuwa wanahitaji mabadiliko na kuwa na kiongozi anayetoka kwenye umaskini ili kuwakomboa.

UCHAGUZI KUWA HURU?

Ni swali linalojibiwa na Makala ya DW, likisema kuwa Waganda wana mashaka kama uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki.

Licha ya kwamba joto la uchaguzi nchini Uganda ni kali kila mahala kutokana na matamshi ya wanasiasa pamoja na askari wa jeshi na polisi wanaonekana kila mahala wakiwa wamejihami kama ambao wanaelekea vitani, hakuna Imani kuwa utakuwa huru.

Wananchi wenyewe wanaonekana kujiandaa kwa hali ambayo wengi wanahisi uchaguzi utakuwa wa ushindani mkali nap engine wenye vurugu na machafuko.

Sheikh Abdallah Sabiila Kadhi wa Sebei, ananukuliwa akisema vyombo vya dola vimetumiwa kupindukia kukandamiza wapinzani na upinzani umejaribu kukabiliana nao kulinda maslahi yao.

Anasema kwa hali hiyo patakuwa na mapambano kwa sababu kuna msemo kuwa mgombea wa NRM lazima ashinde kwa vyovyote vile.

DW inaeleza kuwa upinzani unalaumu utawala wa Rais Museveni kwa kuleta sintofahamu na kusababisha hofu nchini Uganda.

Viongozi wa upinzani wana mtazamo kuwa utawala wa Rais Museveni ndiyo ulaumiwe kwa hali hii ya taharuki iliyotanda na kuwasababisha wananchi kuingiwa na hofu.

"Uchaguzi usichukuliwe kuwa vita ili tutazamane kama watu walio katika uwanja wa mapigano kwani majeshi yamedhibiti kila suala la uchaguzi huo na kwa hiyo hauwezi kuwa huru wala haki," anasema Winnie Kiiza Mratibu wa Kampeni wa Chama cha ANT

Wanaharakati wa haki za binadamu kwa upande wao tangu wiki iliyopita walianza kueleza kuhofia usalama wao nchini Uganda.

Wanasema kinachoshangaza ni kwamba hata Rais Museveni mwenyewe anashuku kwamba kuna njama za udanganyifu kufanyika ili kumsababisha asishinde katika uchaguzi huu. Museveni anasema kuna watu wanaopanga kuiba kura wakiwamo maofisa wa uchaguzi ambao watapewa rushwa kubadili matokeo.

Lakini baadhi ya wapinzani, wanamtaka Rais Museveni akubali matokeo ya uchaguzi endapo atashindwa na aonyeshe uzalendo kwa kukabidhi madaraka kwa amani.

La sivyo, itamaanisha kuwa yeye hajali kama nchi itatumbukia katika hali ya sintofahamu wakimkumbusha kuwa mwaka 1980, Museveni ndiye aliitumbukiza Uganda katika sintofahamu iliyodumu miaka mitano na kusababisha vifo vya mamia ya watu pale alipopinga matokeo ya uchaguzi na kuanzisha harakati za kumwondoa Rais aliyetangazwa mshindi, Milton Obote.

KANUNI MPYA ZAHOJIWA

Wakati huo huo, upinzani na baadhi ya wagombea kwa upande wa utawala aidha wameikosoa Tume ya Uchaguzi kwa kanuni mpya ambazo imezitoa hivi karibuni.

Tume hiyo imetishia kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi ya kituo chochote ambacho watu watakataa kuondoka baada ya kupiga kura na pia hakuna mtu atakubaliwa kwenda na simu kwenye vituo hivyo.

Wadau wanaelezea kuwa simu zitasaidia katika kuwasilisha na hata kuhifadhi ushahidi wa vitendo vyovyote vitavyoweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.

VUGUVUGU LA BOBI WINE

Bobi Wine au Robert Kyagulanyi Ssentamu, mwaka 2008, aliachilia kibao maarufu kama
'Kiwani' na hakuna aliyekuwa na mawazo kwamba mbunge huyu wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, angekuja kuwa mwanasiasa mashuhuri na kumkalia kooni Rais Yoweri Museveni.

Mwanamuziki huyo amekuwa mshindani namba moja wa Rais Yoweri Museveni na chama chake cha NRM katika uchaguzi mkuu wa Uganda ambao leo unaamua hatima ya mahasimu hao.

Miaka kadhaa iliyopita, Bobi Wine alikuwa akijulikana kwa kuimba nyimbo zinazoeleza maisha ya watu maskini yeye mwenyewe akiwa amezaliwa na kukulia katika mazingira ya kimaskini huko Kamwokya.

Hilo ndilo jambo lililompa umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi wa taifa hilo ambao wengi wao ni masikini.

Ni dhahiri kuwa wengi wamepigwa na butwaa walipoanza kusikia habari za Bobi Wine kuwa ni mwana siasa aliyepamba moto na kushangaa zaidi waliposikia amefanikiwa kuwa mbunge mwaka 2017; akiwa mgombea binafsi huku akiwabwaga wagombea wa vyama vikuu vya NRM cha Museveni na FDC vilivyokuwa na wagombea maarufu kwenye jimbo hilo.

UMAARUFU

Nini hasa kimemfanya mwanamuziki huyu mashuhuri aliyekuwa akisifika kwa kuimba nyimbo za kimapinduzi na kujiita ''Rais wa ghetto' kubadilika na kuwa mshindani wa kipekee dhidi ya utawala wa takribani miongo minne wa NRM.

Pengine ni kuwatetea na kuwazungumzia maskini ambao ni vijana.

Bobi Wine ni miongoni mwa wagombea 10 wanaochuana na Museveni.

Akiwa na miaka 38 na kujibandika jina la “rais wa ghetto", ni mwana muziki maarufu Afrika Mashariki ambaye ameng’ara vikali na amefanikiwa kisiasa baada ya kuwahamasisha vijana na wengi kumkubali na kumuunga mkono na kutaka awe rais wao.

Bobi Wine amekuwa mkali na mkosoaji mkali wa Museveni akimwambia kuwa anawaogopa wananchi na kwamba yeye hamhofii.

DW/BBC

Habari Kubwa