Mvua ilivyotishio kwa uhai na afya za watoto

14May 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe Jumapili
Mvua ilivyotishio kwa uhai na afya za watoto

WAKATI mvua za masika zinaendelea kunyesha mchana na usiku, huu ndiyo msimu wa wananchi kuchukua tahadhari ili kujikinga na maradhi mbalimbali yaletwayo na maji taka na unyevu.

Hiki ndicho kipindi cha magonjwa ya mlipuko kama homa ya matumbo, kuharisha damu, na hata kichocho bila kusahau nyungunyungu, mafua na homa za vichomi hasa kwa watoto na wazee.

Familia nyingi zenye watoto wachanga na wanafunzi wa shule huanika nguo ndani na kusababisha unyevunyevu vyumbani ni hatari zaidi kama utaawacha watoto kuishi kwenye mazingira haya. Upo uwezekano mkubwa wa kupata vichomi na mafua.

Lakini pia unatakiwa kuzinyoosha kabla watoto kuzivaa.

Mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na magonjwa ni chanzo cha vifo vya watoto kama wazazi na walezi hawatachukua tahadhari za kuwakinga na maafa pamoja na maradhi.

Wazazi na walezi pia ni vyema kuchukua hadhari na kuwa na ulinzi kwa watoto kwani kipindi kama hiki cha mvua watoto wengi hufariki dunia kutokana na kuzama katika madibwi ya majitaka.

Watoto wadogo wanapokwenda shule au kurudi huvuka mito, mitaro ya maji na wakati mwingine hukutana na madimbwi makubwa . Kwa vile hawana
waangalizi wakiwa njiani wakati mwingine hutumbukia majini na kupoteza maisha.

Mara nyingi watoto ndiyo wahanga wakuu wa maafa mbalimbali yatokanayo na mvua kwa kuwa hawajui athari ama madhara kwani hutokea wakashawishika kuogelea mabwawani, kutembea majini na kucheza sehemu hizo kwa kujifurahisha.

Wazazi kipindi hiki cha mvua wafuatilie na kuzijua njia ambazo watoto wanapita wanapokwenda shuleni wazichunguze kama kuna kasoro wazirekebishe kuwaokoa watoto.

Tatizo la kuacha makaro ya vyoo, visima na mashimo ya vyoo wazi ni suala linalotishia watoto msimu wa mvua. Wazazi wakemee na kukabiliana na watu wenye mashimo na visima au makaro yasiyofunikwa ikibidi waripotiwe polisi.

Licha ya kupoteza maisha kwenye mvua, lakini pia kuna uwezekano wa kupata maradhi ya kipindupindu,kichocho, minyoo, homa ya matumbo, kifua na ngozi.

Baadhi ya magonjwa haya vimelea vyake vinatokana na vinyesi, mikojo na uchafuzi wa mazingira kwa ujumla na wakati mwingine vinaishi katika hali ya hewa yenye unyevunyevu.

Kipindupindu kinaweza kuletwa na maji machafu yanayochanganyikana na yale ya vyooni. Pia mabomba ya maji taka ambayo kwenye sehemu nyingine maboamba ya maji safi ambayo huchanganyikana na taka zinazosambazwa na mvua.

Aidha ,iwapo maji ya kunywa hayatachemshwa au kuwekwa dawa yanaweza kuchangia kupata maradhi ya kuharisha.

Kutokana na hali hii inayoambatana na mvua wazazi wawape watoto maji safi na salama na si jambo la busara kumuacha mtoto kunywa maji yoyote ambayo ni hatari kwa afya yake.

Aidha, jamii nayo kwa upande wake haina budi kuwakataza watoto wao kucheza ovyo mitaani kwenye maji taka, kuwaachia waende mitoni kuvua samaki na kuokota vitu vichafu ambavyo vingine husafirishwa na mvua kutoka eneo moja kwenda jingine.

Iwapo jamii itachukua tahadhari wakati wa mvua itaepusha maradhi ya milipuko na vifo vya watoto vinavyotokana na kutumbukia majini, mtoni au kusombwa na mafuriko.