Mwaka mmoja bila Mkapa anakumbukwa kwa haya

21Jul 2021
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Mwaka mmoja bila Mkapa anakumbukwa kwa haya
  • *Ana kivuli uuzwaji NBC, mabadiliko NEC

JULAI 24, mwaka 2020, haikuwa siku salama kwa Watanzania maana waliamshwa na taarifa za kifo cha kiongozi wao aliyewaongoza kwenye awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Mkapa katika harakati za kisiasa enzi za uhai wake. PICHA: MTANDAO

Mkapa au Ben ni kama alifariki ghafla, kwa vile habari za ugonjwa wake hazikufahamika na wengi, kama ilivyokuwa kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Ben ameondoka, lakini anasifika kwa kuanzisha taasisi imara za umma ikiwamo Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), MKURABITA na kufungua uchumi mambo ambayo hadi sasa yanafanyakazi na kunaendelea kuimarisha maisha ya Watanzania.

Ni kiongozi ambaye aliweka vizuri mambo yake kwa kutumia taaluma ya kidiplomasia aliyokuwa amebobea, na moja ya mambo aliyoyafanya ni kuungwa mkono na mashirika na taasisi za kimataifa likiwamo Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine ambao walisaidia juhudi za kufufua na kuinua uchumi wa Tanzania.

Akiwa amezaliwa mwaka 1938 katika Kijiji cha Lupaso –Masasi mkoani Mtwara, ni zao la Uhuru wa Tanzania kwa vile alishuhudia bendera ya Muingireza ikishushwa na kupandishwa ya Tanganyika mwaka 1961 akiwa na miaka 23.

Ni miongoni mwa vijana waliozijua siasa za kupinga ukoloni, waliothamini misimamo ya kimapinduzi kama uhuru na kazi, ubeberu na ukoloni ni unyama na hamu yake ilikuwa kama chama kilicholeta uhuru cha TANU, kuona Tanzania inaendelea na kujitegemea.

Ingawa alifariki miezi michache baada ya kuzindua kitabu chake cha My Life, Ma Purpose: A Tanzanian President Remembers, amewaachia Watanzania na dunia yale yote aliyopitia na namna ambavyo kwa asili ni mpenda maendeleo pamoja na mleta mabadiliko.

NGUZO YA MAWASILIANO

Mkapa anasifika kwa kuwa kinara wa soko huria na kubadilisha muundo wa mashirika na sekta ya umma. Akianza kuipangua sekta ya mawasiliano na kuuondoa ukiritimba wa Shirika la Posta na Simu (TPTC) na kubariki ujio wa wa kampuni za simu za mkononi za Tritel na Mobitel.

Kazi yake imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa duniani ambayo watu wake wengi wanatumia simu za mkononi kwa mawasiliano na kwenye uwekezaji.

Kwa mujibu wa hotuba ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mawasiliano hadi Aprili mwaka huu, Watanzania wanaomiliki simu za mkononi ni milioni 53.

Kwa upande wa intanet wapo watumiaji milioni 48.9 hadi, wakati laini za simu zilizosajiliwa kwa vidole ni milioni 53, kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, ilipowasilisha bajeti Juni mwaka huu.

UJIO BENKI BINAFSI

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokuwa hazina benki za kutosha na huduma za fedha zilikuwa zinafuata mkondo wa kizamani, lakini awamu ya Mkapa ilisimamia uanzishwaji wa benki nyingi binafsi na maduka ya kubadilisha fedha (bureau).

Aidha, aliasisi uanzishwaji wa benki za wananchi (community) ikiwamo Dar es Salaam, Mwanga, Mufindi, Tandahimba na Mbinga (Community Banks).

Aidha, aliendeleza taasisi za kifedha (micro finance) zisizokuwa za kibenki ambazo ziliendelea kuhudumia mijini na vijijini hata kule kusikokuwa na huduma za benki.

MKURUBITA

Mkapa anaweza kuitwa baba wa kuondoa umaskini kwa imani kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.

Ndiye mwanzilishi wa Mkakati wa Kurasimisha Mali za Wanyonge (MKURABITA) uliokuwa unalenga kurasimisha makazi, biashara, ardhi na mali zote zikiwamo zilizojengwa kwenye makazi duni na ardhi ambayo haijapimwa.

MKURABITA ulilenga mali hizo kupata vibali na uhalali wa kisheria ili zitumike kuondoa umaskini kupitia mikopo na alikuwa akirejea mali hizo kama "dead assets" au ‘mitaji mfu.’

BABA WA ELIMU

Mkapa hakuisahau sekta ya elimu, alianza na mkakati wa kuendeleza elimu ya msingi (MMEM), sekondari MMES, akaanzisha mpango wa elimu ya msingi kwa walioukosa MEMKWA, zote hizo zilikuwa ni jitahada za kuwaamsha Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini ambao pia ulichangiwa na kukosekana elimu bora.

MMES na MMEM ulijenga sekondari na madarasa, nyumba za walimu, katika maeneo mengi nchini.

Ulifanikisha kuchonga madawati, kufunza walimu na kuanzia hapo juhudi za kuboresha elimu ya awali, msingi na sekondari zimekuwa na suala endelevu, zama hizi serikali ikiondoa ada na kugharamia elimu ya awali hadi sekondari.

UJIO SHULE BINAFSI.

Katika awamu yake aliruhusu taasisi za dini, jumuiya mbalimbali na sekta binafsi kuanzisha shule za awali, msingi, sekondari, taasisi za elimu ya juu na serikali kuziunga mkono kwa kila hatua.

Kwa mujibu Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Tanzania ina vyuo vikuu vya umma 12 na vya binafsi 32, hatua iliyoanza na awamu ya Mkapa.

MTANGAMANO

Wakati wa awamu yake, Mkapa alikuwa kinara wa kusimamia uundwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kazi iliyoanzishwa na mtangulizi wake Rais Ali Hassan Mwinyi.

Pia alishiriki bega kwa bega kuiboresha zaidi Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuipa majukumu makubwa kiuchumi baada ya harakati za ukombozi.

Aidha, alikuwa kinara wa kuundwa kwa Umoja wa Fordha wa Nchi za Kusini mwa Afrika (COMESA) na aliendelea kusimamia uwepo wa umoja huo.

ANAPOKOSOLEWA

Katika uongozi wake wa miaka 10 kuanzia 1995 hadi 2005, Mkapa amefanya mengi. Lakini hataacha kukosolewa. Wengine wangetegemea kuona akisimamia mabadiliko ya katiba na kuwezesha kupata katiba mpya inayoakisi uwepo wa vyama vingi.

Aidha, kuunda Tume Huru ya Uchaguzi (NEC) na kubadilisha sheria za uchaguzi kwa kuwa ndiye aliyekuwa baba wa mageuzi na msimamizi wa siasa za vyama vingi kwenye uchaguzi wa 1995.

Mwaka 1995 alikuwa mgombea urais wa kwanza wa CCM kwenye uchaguzi ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na ndiye aliyekuwa kiongozi wa kuanza kuzitekeleza siasa za mabadiliko ya mifumo ya siasa za vyama nchini, kwa vile Tanzania ilikuwa taifa la chama kimoja kwa miongo mitano.

Mkapa ilitegemewa, ili kudumisha demokrasia, angeiunda upya NEC na sheria za uchaguzi ili uwanja wa demokrasia usiwe na mabonde na milima kama ilivyo sasa, kwani kutoangaliwa eneo hilo kumekuwa ni changamoto ya kisiasa inayoitafuna Tanzania hata leo.

Kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 hadi wa mwaka jana 2020, kilio cha wanasiasa, wapinzani na wanaharakati wa demokarasia na uliberali kimebakia kuwa NEC na sheria za uchaguzi ni kikwazo cha kuwapo uchaguzi huru na haki nchini.

KUPINGA UBINAFSISHAJI

Mkapa alifungua milango na njia za uchumi na kualika wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi. Aliboresha na kubadilisha muundo wa mashirika ya umma kupitia ubinafsishaji.

Kwenye eneo hilo, mashirika na kampuni za umma ziliuzwa kwa wawekezaji wa kigeni wengi kutoka Afrika Kusini.
Mkapa anakosolewa kwenye uuzwaji wa benki ya NBC, Shirika la Ndege, la Reli, miradi ya kuboresha TANESCO kupitia Net Group Solution ya Afrika Kusini na kubinafsisha kitengo cha makontena cha bandari ya Dar es Salaam.

Katika kitabu chake anakiri na kuomba radhi kuwa, kwenye ubinafsishaji ‘alichemka’. Lakini anawasihi Watanzania kumsamehe kutokana na ukweli kuwa wakati wa uongozi wake, yalitokea mauaji kisiwani Pemba mwaka 2001 na tafrani nyingine nyingi zilizoibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Anasema hilo lilimuumiza, lakini angependa watu kusamehe na kusahau kwa kuwa, ni wakati wa kuangalia yaliyofanyika Pemba yasijirudie tena kwingine.