Mwalimu afukuzwa, kisa neno 'Father Christmas'

07Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwalimu afukuzwa, kisa neno 'Father Christmas'

MWALIMU mmoja amepoteza kazi baada ya kuwaambia wanafunzi wake kuwa Santa Claus ama maarufu kama Father Christmas, hayupo ulimwenguni.

Picha ya Father Christmas.

Mwalimu huyo msaidizi alikuwa akifundisha wanafunzi wa darasa la kwanza huko New Jearsey nchini Marekani.

Santa Claus ama Santa kwa ufupi, ni hekaya ya zamani ambayo yadaiwa babu huyo mwenye ndevu nyeupe zinazofika tumboni na ambaye huvalia mavazi ya rangi nyeupe na nyekundu pamoja na kofia, huwapatia zawadi watoto watiifu katika mkesha na asubuhi ya siku ya Krismasi.

Hekaya hiyo ni maarufu sana katika nchi za magharibi na huaminiwa kabisa na watoto.

Mwalimu huyo pia inadaiwa aliwaambia wanafunzi wake wenye umri kati ya miaka sita na saba kuwa, hekaya nyingine kama 'Tooth Fairy' na 'Easter Bunny' pia ni za uongo. Easter Bunny au Sungura wa Pasaka, anaaminika kuwapatia watoto wema mayai na zawadi nyingine wakati wa pasaka, nayo huaminiwa sana na watoto.

Father Christmas na Easter Bunny ni hekaya ambazo zinalenga kuwafanya watoto kuwa watiifu na wenye adabu, na kuwaaminisha kuwa ukiwa mkaidi hautopata zawadi itakapowadia sikukuu. Ni sawa na usemi wa waswahili kuwa: 'Mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi.'

Tooth Fairy ni hekaya ambayo watoto wanaaminishwa baada ya kung'oa jino endapo wataliweka chini ya mto wa kulalia, basi asubuhi hugeuka kuwa zawadi na pesa. Lengo ni kuwafanya wasiogope na wawe na hamu ya kung'oa meno ili wapate zawadi.

Kwa mujibu wa maofisa elimu wa jimbo hilo, kitendo cha mwalimu huyo hakikubaliki na kimewaathiri wanafunzi wake.
Ofisa Elimu wa eneo hilo, René Rovtar, hakutaja jina la mwalimu huyo aliyefutwa kazi.

"Kitendo hicho kimenitesa na kunisikitisha sana, hatafundisha tena hapa," anasema.

Aidha, anasema kuna umuhimu mkubwa sana kimaadili kwa watoto kuamini katika hekaya hizo na kisha akapiga picha na Father Christmas na kuirusha kwenye mtandao wake.
BBC.

Habari Kubwa