Mwanadada ‘alivyotoka’ kupitia kilimo mseto

14Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mwanadada ‘alivyotoka’ kupitia kilimo mseto
  • *Avuna mamilioni kila nusu mwaka

KWA umri, jinsi, elimu na kazi yake ni nadra kukuta anajihusha na kilimo mseto, lakini akiwa na umri wa miaka 21 mwaka 2016, Monica Mizambwa alijikuta akivutiwa na kilimo mseto, akichanganya mahindi na maharage kwenye shamba la mkonge.

Monica, mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka minne, amekuwa mfano wa kuigwa wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa kujikita kwenye kilimo hicho ambacho kimemwezesha kumudu maisha yake, pia kuendesha biashara.

Kijana Monica (26), ambaye ni Ofisa Kilimo wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilayani Korogwe, mbali na shughuli zake za ajira, amewekeza katika sekta hiyo ya taaluma yake, akiwa na shamba la mkonge lenye ukubwa wa hekta nne.

Mwanamama huyo kijana anayedokeza ana miaka miwili tangu aanze kuonja matunda ya jasho lake, ana simulizi ya ubunifu wa kipekee namna anavyochanganya mazao kuusindikiza mkonge ndani ya hekta hizo.

Kwa mujibu wa Monica, kwenye shamba hilo lililoko Kitongoji cha Mkokola, Kijiji cha Mkokola, Kata ya Magunga wilayani Korogwe, huwa anatumia ubunifu wa kunufaika na nafasi ya ardhi ulikopandwa mkonge kwa kadri anavyoweza.

Anataja matunda yake kwamba mbali na mkonge, eneo hilo linamnufaisha kwa mavuno ya mahindi, maharage na mimea jamii ya kunde.

Namna ubunifu huo unavyoendesha, mzaliwa huyo wa Chalinze mkoani Pwani anafafanua kitaalamu, akitamka:

"Unapofanya kilimo mseto kwenye mashamba ya mkonge, unakuwa unaitumia ardhi ipasavyo kwa sababu nafasi za kupanda mkonge kutoka mraba mmoja hadi mwingine ni mita nne.

"Sasa hiyo nafasi kubwa ya katikati unaitumia kupanda mazao ya msimu kama mahindi, maharagwe au mimea jamii ya kunde.

"Kwa hiyo, kuliko kuiacha hiyo ardhi ikiwa wazi, unaitumia kupanda mazao mengine ya msimu huku ukisubiri ile miaka mitatu ya mkonge kuwa tayari kuanza kuvunwa.

"Maharagwe unavuna baada ya miezi miwili, mitatu, mahindi miezi mitatu. Ukipanda mazao ya muda mrefu ni hatari kwa sababu mizizi yake inaenda mbali.

"Mizizi ikienda mbali inakutana na mizizi ya mkonge ambayo pia inaenda mbali. Mizizi ya mazao hayo ikikutana huko ardhini, lazima mmea mmojawapo utaathirika.

"Pili, mkonge huwa hauhitaji kivuli, unahitaji jua muda mwingi. Kwa hiyo, ukipanda mazao ya muda mrefu, mfano michungwa na mikorosho, yanaweka kivuli ambacho hakihitajiki kwenye mkonge.

"Mkonge ukishapata kivuli, nyuzi zake zinakuwa nyepesi. Kumbuka kuwa mwisho wa siku kinachouzwa na mkulima wa mkonge ni nyuzi kwa kilo."

Monica mwenye stashahada ya kilimo, ana ufafanuzi zaidi kwamba klimo mseto kwenye mashamba ya mkonge hufanyika ndani ya kipindi cha miaka mitatu baada ya mkonge kupandwa.

"Inaruhusiwa kuchanganya mazao ya msimu tu (ya muda mfupi) kama vile mahindi, mimea jamii ya kunde na pamba, lakini ni muhimu kuzingatia kwamba uchanganyaji huo unapaswa kufanyika kwenye miaka mitatu ya mwanzo baada ya mkonge kupandwa," anasema.

FAIDA ZA KILIMO MSETO

Kuhusu manufaa ya kilimo mseto, Monica anasema ubunifu huo unamsaidia mkulima kurutubisha ardhi hasa pale anapotumia mimea jamii ya kunde kwa kuwa inatoa madini chuma na rutuba muhimu kwa udongo.

"Pili; kilimo mseto kinamsaidia mkulima kupunguza palizi kwa sababu mimea jamii ya kunde hufunika ardhi na hivyo kuzuia uotaji wa magugu.

"Tatu; kilimo mseto humsaidia mkulima kuwa na uhakika wa chakula kwa mazao anayolima kwa kipindi cha miaka mitatu anayosubiri kuanza kuvuna mkonge.

"Nne; mkulima anakuwa anajitosheleza wakati wote wa kulima mazao ya muda mfupi na kukidhi mahitaji yake mengine. Kwa hiyo mkulima anakuwa na uhakika wa chakula na fedha, hivyo anakuwa na fedha ya kuhudumia shamba," anasema.

SAFARI YA MAFANIKIO

Monica anayepaza sauti kwa vijana kuwekeza kwenye kilimo cha mkonge na mseto wake, anasema alianza kujishughulisha na kilimo hicho miaka mitano iliyopita baada ya kupata darasa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

"Kilimo cha mkonge na mseto wa mahindi kinakupa uhakika wa kuvuna magunia 20 kwa hekta moja. Jamii ya maharagwe ni magunia kuanzia 25 hadi 30 kwa hekta moja.

"Kwa mkonge ambao uko kwenye usimamizi mzuri zaidi, hekta moja mkulima ana uhakika wa kupata kuanzia Sh. milioni mbili hadi milioni 2.5 kwa hekta baada ya makato yote.

"Ukumbuke mkonge unavunwa mara mbili kwa mwaka, kila baada ya miezi sita unavuna. Mimi kwa sasa ni shamba la hekta nne, yaani ekari 10. Nilianza kulima mkonge mwaka 2016, lakini sikuanza kwa kupanda kwenye hekta zote nne.

"Mwaka 2016 nilianza kwa kupanda hekta mbili, kwa maana ya ekari tano. Huu nimeshaanza kuuvuna. Mavuno ya kwanza mwaka 2019 nilipata Sh. milioni 1.2 baada ya makato yote.

"Makato hayo ni zile gharama za uzalishaji, mfano kwenye kuvuna tunatumia watu, kuna gharama za kusafirisha kutoka shambani hadi kiwandani, gharama ya kiwanda kinachochakata na kuna gharama ya chama ya uendeshaji kwa sababu tunafanya kazi chini ya Ushirika ambao pia una tozo zake," anasema.

Monica anabainisha kuwa uzoefu wake kwamba mavuno ya kwanza ya mkonge huwa ni madogo kwa sababu unakuwa si mzuri kutoa singa nzito, pia mkonge huo wa mavuno ya kwanza unakuwa si mrefu.

"Kwenye mauzo ya mkonge kinachozingatiwa ni urefu wa singa, kiwango chake na rangi. Rangi yenye soko zuri ni cream (rangi ya maziwa) isiyokuwa na doa lolote lakini urefu wa nyuzi zake uwe kuanzia sentimeta 60.

"Kwenye 'cut' (mavuno) ya kwanza, mkonge hauwezi kufika urefu huo wa sentimeta 60. Hiki kiwango cha juu kinapatikana kwenye 'cut' ya pili ama ya tatu.

"Mwaka 2017 nilipanda hekta moja na mwaka jana nilimalizia kupanda ya mwisho. Ninaendelea kuvuna maana mkonge unavuna mara mbili kwa mwaka.

"Mkonge hauhitaji mvua nyingi, kuna wadudu walikuwa wanaleta usumbufu lakini TARI wametusaidia dawa za kuwakabili. Mwaka wa kwanza nilipochanganya mahindi, nilivuna magunia sita lakini sikutumia mbegu bora.

"Mwaka wa pili sikulima tena mahindi, Nikalima maharagwe, nikapata magunia manane. Mwaka 2019, nikachanganya mahindi kwa mbegu bora, nikapata magunia 15 ya mahindi. Mwaka jana sikulima tena mazao mengine na hata mwaka huu sijachanganya kwa sababu muda umenibana. Wakulima wengine wanaendelea na wanafanya vizuri sana.

"Mwaka huu katika 'cut' ya kwanza ya mwaka nimevuna hekta mbili za mkonge na nimepata faida ya Sh. milioni 2.13. Kwa kifupi, kwa sasa nina uhakika wa kukidhi mahitaji yangu ya kifamilia na nimefanya vitu vingi vya kimaendeleo. Ninawekeza kwenye biashara fedha hizo za mavuno ya mkonge na mseto wake.

Monica ambaye pia anajishughulisha na kilimo cha tangawizi, anabainisha kuwa aliajiriwa kuwa Ofisa Kilimo wa Korogwe AMCOS mwaka 2019 baada ya kujitolea kufanya kazi hiyo kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016, akiwasaidia wakulima.

Habari Kubwa