Mwanamitindo Odemba kumtua mama ndoo

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwanamitindo Odemba kumtua mama ndoo

SERIKALI ilizindua kampeni iitwayo ‘Kumtua Mama Ndoo Kichwani."Hapo lengo kuu ni kuhakikisha kila maeneo kunapatikana huduma ya maji safi na salama.

Na Tatu Tambile

Hiyo inafanyika mbali na kupata huduma ya maji bomba, pia kunachimbwa visima virefu na vifupi, kutumia maji ya maziwa na mito kuyapeleka katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alionekana kuunga mkono kampeni hiyo mwishoni mwaka jana alipozungumza na waandishi wa habari na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule Sekondari Bugando, wilayani Geita.

Aliwaagiza wakuu wa wilaya kusimamia uhifadhi wa maeneo vyanzo vya maji, ili kuyafanya yaendelee kuwa chepechepe na kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji ya uhakika na kuainisha maeneo ya misitu na vyanzo vya maji, yatunzwe vizuri.

Katika hatua nyingine za juhudi za kuunga mkono kampeni ya "Kumtua Mama Ndoo Kichwani" mwaka huu Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, alizindua na kukagua miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, katika Kata ya Ibwera, eneo la Rugaze yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi 500, ambako juhudi za serikali zikiendelea kufanyika kuwafikia wengine kuhakikisha wanapata huduma bora ya maji safi na salama.

Vijijini ndiko wahanga wakuu wa upatikanaji na maji safi na salama. Sasa taasisi nyingine zisizo ya kiserikali, zimekuwa zikiunga mkono kampeni hiyo ya kiatifa, chini ya msimamizi mkuu, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hapo ni asasi ya African Reflection Foundation, chini ya mwanamitindo ya zamani, Miriam Odemba. Alipozongumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, anasema ameamua kutoka nchini Ufaransa alipokuwa akiishi, kuja nchini Tanzania ili kuunga mkono jitihada za serikali.

Odemba anasema kwa kutambua changamoto hizo ameamua kuunga mkono jitihada za serikali kufanya kazi kwa kushirikiana wadau, ili ama kuondoa au kupunguza tatizo la upatikanaji maji safi na salama.

"Wote tuna malengo ya kuisaidia jamii katika nyanja tofauti, ikiwamo kutafuta wafadhili kwa ajili ya kuendelea na kufanya utafiti wa miradi tunayoilenga hapa nchini.

“Basi, tumeona vyema tufanye kazi kwa kushirikiana huku taasisi ya ARF imebobea katika misaada ya kuchimba visima na wameshafanya hizo kazi sehemu nyingi nchini,” anasema.

Odemba anasema, Oktoba mwaka huu walitembelea Wilaya ya Mkuranga kutimiza ahadi ya kuchimba visima katika lijiji cha Kiwambo, katika Shule ya Msingi Kiwambo, yenye wanafunzi 366, ili wapate maji safi na salama, kuokoa kinamama watoto walio katika changamoto nyingi wanapofuata maji mtoni.

Aidha, mwanamitindo huyo anasema anapenda kuwasaidia wasichana wanaopenda kujihusisha na uanamitindo kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na ameweza kuwasadia walimbwende kadhaa kutimiza ndoto zao.

Wito wake ni jukumu la kila Mtanzania mwenye hofu ya Mungu kuguswa kwa namna moja au nyingine kuchangia wahitaji wanaoishi katika mazingira ambayo si rafiki kusaidia kukabiliana na changamoto zinazowazunguka ya huduma ya kijamii ikiwamo ya maji safi, elimu, afya na malazi kwa ujumla kuhakikisha watoto, wamama, wazee na vijana wanapata huduma bora ya kijamii.

Habari Kubwa