Mwanzo wa Sh. laki umewapa kuku 500 waliojaa bandani, mtaji mpya mil.

22Mar 2019
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Mwanzo wa Sh. laki umewapa kuku 500 waliojaa bandani, mtaji mpya mil.
  • Wajenga banda mil. 16/-; mbioni kuwa kampuni
  • Wote waajiriwa wa mshahara kwenye mradi wao

MRADI wa ufugaji kuku unaoendeshwa na kikundi kinachojulikana kama ‘Bosi Kuku’ katika kijiji cha Mlilingwa, Kata ya Tununguo, Ngerengere wilayani Morogoro, kazi zake zimewasha taa ya mafanikio.

Nyuwaji Bakari, Katibu wa Wacoma Mkaa wa Mlilingwa, Morogoro, akieleza jambo kuhusu uandaaji wa mkaa endelevu. PICHA: CHRITISTINA HAULE.

Hiyo ni kutokana na mafanikio ya kumiliki mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 25 sasa, ikiwa ni matokeo chanya ya Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Mtaa Tanzania (TTCS), maarufu kama mkaa endelevu.

Selemani Mwishehe, mwenyekiti wa kikundi hicho cha wanachama 12 kilichoanzishwa mwaka 2015; kinamama watatu na wanaume tisa, alipozungumza katika maonyesho ya wazi ya shughuli za mkaa endelevu kijijini Mlilingwa, ana mengi.

Anataja mzizi wa mafanikio kupitia mradi wa uchomaji mkaa, ulianza kila wiki walipokutana na kila mmoja alichanga fedha shilingi 10,000 na kukusanya shilingi 120,000. Mtaji ulipofika shilingi milioni moja, walianza kutengeneza banda dogo.

Mwishehe anasema, walianza kwa kununua mbegu za vifaranga kwenye shamba la kuku na walipokua waliwauza na kubakiza wachache, kwa ajili ya kuendeleza mradi.

Pia, anasema fedha zingine za mapato ya mauzo, walitumia kutotoa mayai 1000 kwa wakati mmoja na kuuza kuku 1000, kila baada ya miezi mitano waliowapatia. Walivuna kati ya shilingi milioni 12 hadi 13.

Mwishehe anasema, hadi sasa wameshauza kuku mara tatu tangu kuanza mradi na wamejenga banda kubwa la kuku lenye thamani ya shilingi milioni 16.

Anafafanua kuwa, mpaka sasa wana kuku 500 na 100 kati yao ni jogoo na majike 400 na mbolea itokanayo na kinyesi cha kuku, wanawauzia walima mboga, pia wanauza mayai, vifaranga na kuku wakubwa.

Katika kuhudumia, anasema wanatumika katika nafasi ya wafanyakazi na wanalipana ujira shilingi 300,000 kila mwezi, lengo ni kupandisha daraja mtaji mradi uwe kampuni, badala ya kikundi.

Changamoto

Mwishehe anasema kuwa, mabanda yao ni madogo hayakidhi hitaji la idadi ya kuku walio nao na wanaoongezeka.

Mtazamo wao ni kuwa na mabanda manne kukidhi hitaji la uzalishaji kuku 4,000 wakubwa watakaoweza kuingiza kati ya shilingi milioni 48 hadi 52 kila miezi mitano inapopita.

Kuku hao wanaweza kuhudumiwa panapokuwapo banda lenye wastani wa mita 80, linaloweza kuingiza kuku 1,000. Ushauri wake kwa vijana wengine wanaojishughulisha na mkaa endelevu, waungane kwenye vikundi wawekeze katika namna wanavyoshauriwa.

Mmoja wa wana - kikundi hicho cha kuku, Barat Gatilali, anasema amefanikiwa kujenga nyumba ya vyumba vitatu yenye thamani ya shilingi milioni 3.5, kitu ambacho hakuwa nacho kabla ya mradi.

Anasema kushamiri kikundi hicho, ni matokeo ya mradi mkaa endelevu kuwa mazuri kwao na kuna uwezekano wakawaachia wenzao shughuli hiyo, ili baadaye nao wapate mitaji ya kuanzisha biashara zitakazowasaidia.

Barat anasema, ni namna yenye nafasi kuondokana na uharibifu wa mazao ya misitu, pia wanaachiana fursa ya kupiga hatua.

Mwenyekiti Halmashauri

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro, Kibena Kingo, anasema halmashauri hiyo imetenga shilingi milioni 26, kwa ajili ya kuwakopesha vijana kuendeleza miradi yao.

Kingo anasema, tayari kuna kitengo maalum kimeshafikisha katika halmashauri vikundi vinavyotambuliwa na sasa, kazi ya ukaguzi unafanyika, kabla ya kuviidhinisha vipatiwe fedha hizo.

“Kwa hawa tumeona leo ni kweli wanafanya (kazi), ukiwapa wataendeleza. Nina uhakika kamati ya fedha itakayokaa mwezi huu itawasikiliza.

“Kwa bahati nzuri leo viongozi wengi tumekiona hiki kikundi kwa hiyo tunalo la kusemea kwenye kikao,” anasema Kingo.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mlilingwa, Raheli Abdueli, anasema kijiji hicho kimepanga kutumia zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya shughuli za kijamii na uhifadhi misitu kijijini.

Pia, anasema wameshakusanya shilingi milioni 155 zitokanazo na tozo za leseni 144 za uvunaji mkaa, kijijini humo.

Betty Luwuge, ni Ofisa Mawasiliano wa TTCS, anasema, wamekuwa wakihamasisha wananchi vijijini wanaozalishaji mkaa endelevu, wajiunge na kuendeleza biashara ndogo, ili kupunguza msukumo au mahitaji ya kwenda msituni.

Anasema, biashara au shughuli mbadala wanazoweza kufanya, inasaidia kuendeleza kuhifadhi misitu ya nchi na hizo biashara zinaonyesha kuwa na mafanikio.

Katibu Tawala Moro

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Hilary Sagala, anasema elimu inayotolewa na mradi huo ni nzuri na inapaswa kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo, kuwawezeshwa walioko shuleni warithi.

Anasema sekta ya misitu ni muhimu sana katika kuleta maendeleo na kunufaisha sekta zingine na kwamba elimu nzuri ikizidi kutolewa, itasaidia jamii ikiwamo vijana kupata ajira tosha kupitia uhifadhi endelevu wa misitu.

Sagala anasema, misitu inayosimamiwa vyema na kuwa endelevu italeta mchango katika sekta zinazotegemea mifumo ya ikolojia ya misitu ya asili, kama vile kilimo, maji na nishati na maendeleo ya kisasa ambayo serikali inategemea.

Hivyo, anawahimiza wajumbe kujitoa katika kuhifadhi misitu ya asili iliyopo kwenye ardhi za vijiji kwa kuwa ndipo takwimu zinaonyesha kutoweka kwa misitu kwa kiwango kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu.

“Nimeelezwa kuwa dhana ya mkaa endelevu ni chanzo kimojawapo cha uhifadhi misitu, ambayo hutumia eneo dogo la msitu,” anasema.
Meneja Mradi

Meneja wa mradi huo, Charles Leonard, anasema mradi wake umekuwa muhimu kimkoa, hususan wilayani Morogoro, inakohakikisha wananchi wake wanapata maendeleo kutokana na rasilimali miti zinazowazunguka.

Anataja mifano ya mafanikio, ni madarasa ya shule za msingi yaliyojengwa kwa fedha hizo na wananchi kuingizwa kwenye huduma ya bima ya afya.

Pia, shughuli mbalimbali za maendeleo yote kwao zinafanyika kutokana na mapato kupitia uvunaji endelevu wa rasilimali miti kwa ajili ya mkaa endelevu na mbao.

Anasema, mradi unalenga kuhifadhi rasilimali miti kwa njia endelevu zinazonufaisha wananchi kupata faida za moja kwa moja, wanaboresha maisha yao, huku wakipunguza uharibifu wa misitu unaoendelea nchini.

“Nchini tuna takribani hekta milioni 48.1 za misitu na zaidi ya asilimia 90 ni misitu ya miombo, wakati kwenye hekta hizo milioni 48.1 zaidi ya nusu zipo katika ardhi za vijiji.

“Nchi hupoteza misitu hekta zaidi ya laki 4 na misitu hiyo hupotea katika ardhi za vijiji, hivyo sote tuna jukumu la kuangalia namna gani tunapunguza uharibifu wa misitu katika ardhi za vijiji,” anasema Leonard na kuongeza:

“Pili, namna gani rasilimali misitu zitawanufaisha ili waweze kuona rasilimali hizo ni mali yao kwa kupata faida ya moja kwa moja kama vile kupata bima za afya na shughuli za maendeleo mahali walipo.”

Anasema, mradi huo unatekelezwa katika vijiji 30, kati yake 20 Wilaya ya Kilosa; na vitano kwa kila wilaya za Mvomero na Morogoro.

Vijiji vilivyoko Morogoro, ni Mlilingwa, Matuli, Lulongwe, Tununguo na Diguzi, ambavyo vyote vimeshawezeshwa kwenye Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kunatolewa mafunzo kwa wazalishaji mkaa na mbao.

Ni mradi unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na mtandao wa jamii wa usimamizi wa misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati ya Asili Tanzania (TaTEDO), mfadhili mkuu akiwa Shirika la Maendeleo la Ushirikiano la Uswis (FDC), kuanzia Machi 2012.

Habari Kubwa