Mwenyekiti Mkuranga ang’aka ‘amcos’ kuamua bei peke yake

22May 2020
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Mwenyekiti Mkuranga ang’aka ‘amcos’ kuamua bei peke yake
  • •DC: Tunadaiwa Sh. bn. 1 za korosho; Sh. 33 dalili ‘kupigwa’

JANA jarida la Afya na Mazingira lilikuwa na mwendelezo wa simulizi za Mkuranga, kuhusu afya ya wanafunzi kipindi cha likizo iliyopo.

Sehemu ya korosho ikiwa ghalani Mkuranga, ikifanyiwa ukaguzi na uongozi wa serikali mwaka jana. PICHA: MTANDAO.

Ni mwendelezo wa simulizi ya Ijumaa iliyopita kuhusu janga la wakazi kukosa daraja ambalo ni janga la kiuchumi.

Kimsingi, wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wakazi wake wakuu ni wakulima na zao lao la biashara mahsusi ni ‘dhahabu ya taifa’ korosho.

Kutokana na zao hilo kuwa juu hivi sasa, wakazi wa Mkuranga, kama walivyo wenzao wa mkoa wa Pwani; Rufiji, Kibiti na Kibaha, pia mikoa ya Lindi na Mtwara, wanawajibika kwa palizi za kila msimu, ili waweze kunufaika na jasho lao shambani.

Vilevile Mkuranga wanajituma kulima mazao mengine kama mihogo, viazi, matikiti maji, nazi na aina mbalimbali ya matunda.
Hiyo yote ni kumuwezesha mwananchi kuinuka kiuchumi na kujiongezea kipato yeye na familia yake.

Hivi karibuni katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, walilalamikia vyama vya msingi vya ushirika maarufu ‘amcos’ kuwa chanzo cha kudumaza uchumi wa wilaya ambazo kimsingi wakazi wake ni wakulima.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Juma Abeid, ambaye ni pia ni Diwani wa Kata ya Magawa, anasema Mkuranga ina jumla ya ‘amcos’ 45 zinazotambulika.

Abeid anafafanua kuwa, vyama hivyo vinashindwa kufanya mikutano na wakulima, ili kujadili changamoto za korosho

Mwenyekiti analalamika vyama hivyo vya ushirika vipo chini ya serikali, lakini inashangaza kuyumbisha bei ya wananufaika wakulima, hivyo anacholilia ni ‘amcos’ zisifanye bei peke yao.

"Amcos zote zinatakiwa kuwa na bei moja,” anasema Abeid, huku akilalamika kuwa dai lingine katika kipindi kilichopo, mazao ya wakulima yanaharibika kwa kukosa wanunuzi.

Anafika mbali na malalamiko ya kutokukubaliana na ushuru wa mazao kwa bei Sh. 127 kwa kilo, akihoji kwa gadhabu: "Mkulima atapata wapi huo ushuru, ukizingatia hakufanya biashara kutokana na mvua ambazo zimeharibu korosho na kusababisha kurudishwa majumbani?"

DC AFAFANUA

Mkuu wa Wilaya hiyo, Filbeto Sanga, katika kikao cha Baraza la Madiwani, anasema korosho za mwaka 2018 na 2019, wakulima wanadai malipo ya mauzo zaidi ya Sh. bilioni moja.

Sanga anaahidi malipo kufanyika taratibu na hadi sasa anataja changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu katika vyama vya ushirika vya wakulima.

"Kuna chama kimeleta majina ya wakulima wanadai milioni 33. Nimewaambia wawalete hao wanaodai na sio majina, hawajaletwa mpaka leo wanaodai na sisi tutafuatilia. Tukibaini kuna udanganyifu na majina yasipothibitishwa, tunayafuta," anasema Mkuu wa Wilaya.

Sanga anasema licha ya Mkuranga kuwa na jumla ya vyama vya ushirika 45vya wakulima, vilivyofanya mikutano kwa mujibu wa katiba zao ni vyama 14 tu.

Rai yake ni kwamba wataalamu wa ushirika wanapaswa kwenda kusimamia mikutano ya vyama hivyo.

Kuhusu wabanguaji korosho, Sanga anawakumbusha ubia wa ufanisi wa kazi yao, madiwani wanapaswa kuendelee kushirikiana na wananchi, kukamilisha kazi za wananchi.

Moja ya majukumu yao madiwani, Sanga anakumbhusha ni kuwa karibu na wataalamu wa korosho, ili wajifunze jinsi ya kutatua matatizo ya wakulima wa zao hilo.

DED

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Injinia Mshamu Munde, anasema makusanyo ya mapato katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2016, ilikuwa kiasi cha Sh. bilioni 2.5.

Pia, anasema katika mwaka wa fedha 2017/2018, walikusanya jumla ya Sh. bilioni 6.3; mwaka 2019/2020 walifikisha Sh. bilioni 6.5.

Anasema hadi kufikia mwezi uliopita, alitarajia kufikia asilimia 100 ya malengo na anajigamba: “Tuna uhakika makusanyo yatapanda mpaka kufikia Sh. bilioni saba,"

Habari Kubwa