Mwongozo mkoa wa ‘Mwanga Elimu’ ulivyolinda wanafunzi

01Aug 2020
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
Mwongozo mkoa wa ‘Mwanga Elimu’ ulivyolinda wanafunzi
  • • Waliofikishwa wakiri ‘tuko sawa’

“KABLA ya kuanza utekelezaji wa mpango mkakati wa kuwawezesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kusoma katika kipindi cha likizo ya dharura ya tahadhari ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu (COVID 19).

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mahaha, Charles William, akiwa ofisini kwake, anaeleza jambo kuhusu wanafunzi wake. PICHA: HAPPY SEVERINE.

“Nilipata wakati mgumu wa kufikiria ni namna gani nitaweza kuwasaidia wanafunzi wangu wa madarasa ya mtihani,” ndivyo anavyoanza simulizi, Robert Mathias, Mkuu wa Shule ya Msingi Kidinda, katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu.

Anasema baada ya kutangazwa likizo hiyo, alishikwa na mshituko wa ghafla uliomfanya ashindwe kufikiria cha kufanya kuwasaidia wanafunzi wake, aliyohitaji muda zaidi kuwanoa kitaaluma, kuwapa majaribio na maarifa ya namna ya kujibu vyema mitihani yao.

UAMUZI GHAFLA

Mathias anasema, kabla hajajua cha kufanya, alipokea taarifa zilizomtaka atekeleze mpango mkakati wa mkoa, wa kuwasaidia wanafunzi ndani ya likizo ya corona.

Ni agizo lililowangukia waliopo katika shule za msingi na sekondari, kwa kupatiwa majaribio na mitihani ya kuwapa maarifa katika masomo yao

Anasema, mara baada ya kupokea mkakati, ndipo alipoanza kuona mwanga na nuru ya mafanikio yake shuleni.

“Nilifurahi sana kupokea mkakati huo maana hapo nyuma kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa corona shule yake ilijipanga kushika nafasi ya kwanza kimkoa, katika mitihani ya kitaifa. Hivyo, naamini kwa sasa mipango yetu itatimia,” anasema.

Pia, anaeleza kuwa wameutekeleza mkakati walivyoelekezwa, hata umeweza kuonyesha mafanikio makubwa, kutokana na wanafunzi kudumisha kumbukumbu za kutosha katika walivyojifunza.

Mathias anaueleza mkakati huo umewasaidia wanafunzi wake na shule nyingine ndani ya wilaya Bariadi, kupata masomo (vidokezo na majaribio)wakiwa nyumbani.

Ni kazi inayofanywa na walimu wao kupitia mkakati uliokuwa na malengo makuu manne yanayotarajiwa kuifanya Simiyu iendelee kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.

"Malengo makuu ya mkakati huo yalikuwa ni kumwezesha mwanafunzi kuendelea kujifunza, walimu kuwa na mawasiliano ya kitaaluma na wanafunzi wao,” anaeleza Mathias na anaongeza:

“Wazazi kufanya kufuatilia taaluma za watoto wao pamoja na watoto (wanafunzi) kutulia nyumbani wakijisomea kipindi hicho cha likizo, huku tahadhari zote za maambukizi ya virusi vya corona zikizingatiwa."

Geodfrey Kamugisha, ni mwalimu wa taaluma shuleni hapo, anasema malengo yote manne yalifikiwa kwa mafanikio, hali inayowapa matumaini kuwa na utayari wa wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani kitaifa wakiwa na ufaulu wa juu.

Anasema katika shule ya Kidinda, mpango umesaidia kuwafikia wazazi wa wanafunzi, wakiwapatia majaribio katika kipindi chote kilichopita cha tahadhari ya corona, wakiwa na mrejesho sahihi.

“Wakiwa nyumbani wanafunzi walikuwa wakijisomea na kufanya majaribio mengi zaidi. Wazazi walijitokeza kwa wingi kuja shuleni kuwachukulia majaribio na masahihisho yao.

“Pia, kwa mkakati huo imewasaidia sana wanafunzi kubaki na kumbukumbu ya masomo waliyofundishwa,” anasema.

Anautaka kuwa ni mpango uliowezesha kuwasaidia wanafunzi wao wa madarasa ya mtihani, waendelee kujifunza na kusoma wakiwa majumbani.

Ni mazingira yaliyotumika kuchunguza kilichotumika kufanya mkakati na walibaini wanafunzi wengi kuwa na uelewa, pia kumbukumbu zinazopaswa kimasomo.

Kamugisha anasema, wanafunzi wote walio katika madarasa ya mitihani, walifanya majaribio mengi zaidi wakiwa majumbani na wote walirejesha majaribio hayo, ili wasahihishiwe na kupatiwa tena.

“Kwa wanafunzi wa darasa la nne, walifanya jumla ya maswali 2010, huku darasa la saba maswali 3500, ambayo yamewasaidia sana kutunza kumbukumbu na uelewa wao wakati wakiwa nyumbani,” anasema Kamugisha.

Adalbert Chambia, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gamondo, anaupongeza kwamba ni mkakati uliosaidia kudumisha njia sahihi ya kufanya vizuri katika mitihani kitaifa, chini ya kivuli cha mkakati wao mkuu kushika nafasi tatu za juu kitaifa.

“Bila ya kuwapo mkakati huo, sidhani kama wanafunzi wengi wangeendelea kuwa na kumbukumbuku kama walizorudi nazo katika masomo yao,” anasema.

YALIVYOFAYIKA

Mwalimu Mkuu huyo anasifu, majaribio yalikuwa yanatolewa kupitia shule, makanisa, misikitini na masoko makubwa, hali iliyowapa urahisi wazazi kufuatilia majaribio hayo.

Charles William, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mahaha, anakiri mafanikio ya kitaalamu kwenye likizo ya corona, asilimia kubwa ya wanafunzi waliyafanya kwa wakati na kupewa mrejesho.

Pia, anataja ushiriki wa wazazi kuwa wenye mafanikio makubwa, kwani wazazi walijitokeza kufuatilia mazoezi, jambo analoamini ni ishara sahihi kuelewa umuhimu wa ushiriki wao katika elimu ya watoto wao.

WANAFUNZI WAELEZA

Wanafunzi wa Shule za msingi Gamondo A, Kidinda na Mahaha, wanasema mpango mkakati wa kujifunza wakati wa likizo umewaongezea uelewa na ujuzi kujibu maswali, kutokana na kufanya mazoezi mengi kwa wakati.

“Tunawashukuru sana walimu na wazazi wetu…wamekuwa wakijitoa kwa kadri wawezavyo ili kuhakikisha wanatusaidia, tuweze kusoma wakati wa likizo.

“Wazazi wetu walikuwa wakitufuatia maswali shuleni,” anatamka Maria Sayi, mwanafunzi darasa saba, shuleni Gamondo A.

Mwanafunzi Yohana Masunga, aliyeko darasa la nne, anakiri mpango kumsaidia kujifunza nyumbani na sasa anamudu majaribio mengi peke yake, kwa mbinu mbalimbali.

“Binafsi, mpango umenisaidia, wazazi walikuwa wakinifuatia maswali shuleni na nilifanya maswali yote na kupatiwa majibu na walimu.

“Kwa sasa sina shaka katika kujibu mtihani wa kitaifa, maana mbinu nyingi za kujibu maswali nimezipata vyema,” Masunga
Wasi Boniphace, anayesoma mjini Bariadi, anadokeza hisia zake kwamba pasipo kutolewa mkakati wa kusoma likizoni, wanafunzi wa madarasa ya mitihani wangepoteza kumbukumbu ya walichokisoma kwa kiasi kikubwa.

Anaeleza nafsi yake wakati huo keamba hakupata shida aina yoyote kujisomea, kwani alisaidiwa mwongozo na mkakati uliowekwa na mkoa.

Habari Kubwa