Mzazi daktari aliyenusurika ‘leba’ anena

22Sep 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mzazi daktari aliyenusurika ‘leba’ anena

LICHA YA kuwa tabibu, Dk. Safira Telatela naye ana simulizi kuhusu mazito yaliyomkuta wakati wa kujifungua mtoto wake wa pili, mwaka 2004.

Anasema katika kipindi cha ujauzito, hakuwahi kukutwa na tatizo lolote, ikiwamo alipohudhuria kliniki na hata ilipofika wakati wa kujifungua, kwani alijisikia uchungu na aliwahishwa hospitalini kwa ajili ya kujifungua.

Dk.Telatela anasema alijifungua salama akiwa jijini Dar es Salaam, lakini muda mfupi baadaye alianza kuvuja damu kwa wingi, hali iliyofanya aishiwe nguvu na kupoteza fahamu.

''Tukio hili ninalowaelezea hapa nililishuhudia kwa kipindi kifupi, nikiwa bado nina ufahamu baada ya kujifungua, lakini baada ya hapo nilipoteza fahamu na sikujua kilichoendelea tena, isipokuwa nilisimuliwa kesho yake na ndugu zangu pamoja na jopo la madaktari waliokuwa wananihudumia kuokoa maisha yangu,'' anasema.

Anasema katika kuokoa maisha yake, waliokuwapo hapo kwa kushirikiana na madaktari walifanuya kasi ya ziada na walijitolea damu haraka aliyowekewa na ndicho kilichofanikisha akapona.

Daktari huyo anasema baada ya kusimuliwa mkasa huo, aligundua kilimchomnusuru kilikuwa mazingira ya mjini tena katika hospitali kubwa, wanakopatikana madaktari na wauguzi wenye ujuzi, ambao walichukua hatua za haraka kumuokoa.

Anasema, ni jambo linalomfanya ajiulize, kama hilo lingemtokea katika zahanati ya kijijini, ambako hata uwezekano wa kupata huduma ya nyongeza ya damu ni tatizo kubwa, ingekuwaje?

''Sasa nikizungumzia tatizo la kutokwa damu kwa mwanake mwenzangu ambaye yuko huko vijijini, akipata tatizo lililonitokea mimi kuna kupona kweli?” anahoji Dk. Talatela.

''Nitoe mfano kwa mkoa wa Rukwa ambako nimefanya kazi. Ukienda mkoani humo, kule wilaya ya Nkasi kuna kijiji kinaitwa Wampembe, kipo Ziwa Tanganyika ‘ndani ndani.’

“Yaani huko, mama akipata tatizo la kutokwa damu kama lililonitokea mimi, kupona kwake ni vigumu. Kwa sababu kutoka kwenye hicho kijiji hadi hapo Nkasi, ni kama kilomita 80 hadi 100.

“Barabara yake ni mbaya sana, hata ikipigwa 'radio call' ya kupeleka ‘ambulance’ (gari la wagonjwa) kwenda kumchukua mgonjwa hadi kufika huko ni saa nne na kumpeleka mjini ni saa nne. Jumla ni saa nane, sasa hapo kuna kupona kweli?'' anahoji kwa maraya pili, katika ujumbe unaoashiria mazingira magumu ya kupona.

Dk.Telatela anasema hata upatikanaji wa damu ni hadi mako makuu ya mkoa mjini Sumbawanga, ambako wanaagiza damu hiyo kutoka Benki ya Damu ya Kanda, iliyopo jijini Mbeya, ambako kijiograifia ni mbali sana.

''Mimi siku ile nilikuwa navuja damu kweli kweli, kwa hiyo nilipona kwa sababu tu kulikuwa na hiyo huduma, ingekuwa kama niko Wampembe, Nkasi ningekufa tu na leo hii ingekuwa imebaki ni historia kwamba alikuwapo daktari fulani alikufa kwa uzazi, 'thanks God' (Ashukuriwe Mungu)nilikuwa mjini ambako niliweza kupata hizo huduma haraka,” anaeleza.

Dk. Telatela anaeleza kwamba, kitaalam mwanamke anayetokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, anatakiwa ahudumiwa ndani ya saa mbili, kwani kinyume chake anapoteza maisha.

Anamtambulisha mwanawe aliyepata msukosuko wa kuijifungua, ni sasa mhitimu wa mtihani wa darasa la la saba mwaka huu na bado anaendekea kuwashukuru wote waliojitolea damu katika hali ya dharura kunusuru maisha yake.

USHUHUDA WA MBUNGE

Anna Lupembe ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Katavi, ambako Dk. Telatela aliwahi kufanya kazi.

Mbunge huyo ana ushuhuda wa kifamilia, wa namna alivyompoteza mjukuu wake.
Anasimulia kuwa hivi karibuni mtoto wa dada yake ambaye amemlea, alipelekwa hospitalini baada ya kupata uchungu, lakini akiwa katika chumba cha kujifungua, alikaa muda mrefu pasipo kujifungua na hazikuchukuliwa hatua za haraka kubaini tatizo.

Akisubiri kujifungua, alibaki katika chumba hicho kwa siku mbili na alipofanikiwa kujifungua, muda mfupi baadaye alifariki, kutokana na mtoto kuchoka, kwani muda wote huo kiumbe kikiwa tumboni, mama yake alikuwa akipambana kujifungua.

Anasema kama ilivyozoeleka baada ya mtoto kufariki, majibu ya watu yalikuwa ‘haikuwa riziki,’ pasipo kutambua huenda zingefanyika jitihada za haraka kubaini tatizo, mtoto angepona.

Lupembe anashuhudia tukio lingine la mwezi huu alipokuwa safarini, kwamba alikutana na mama mjamzito barabarani porini mkoani Katavi akiwa ameketi chini anahangaika.

Anasema, alilazimika kusimamisha gari na baada ya kumsogelea, alibaini kwamba alikuwa mjamzito na wakati huo alikuwa akiumwa na uchungu.

Lupembe anasema alilazimka kubeba jukumu la kumsaidia kumzalisha, licha ya kutokuwa na utaalam wa ama udaktari au ukunga na katika kile anachokitamka “namshukuru Mungu’ mtoto huyo alizaliwa salama.

''Nataka niwaambie kwamba, katika masuala ya uzazi, wanawake walio vijijini wanapata shida kuliko mnavyofikiria. Watu wengine wakisikia hayo, mambo yanasemwa wanafikiri ni hadithi.

“Haya mambo yanatokea! Nendeni vijijini mtashuhudia, ni hatari, wanawake wanajifungua kwa neema za Mwenyezi Mungu, pasipo daktari, tena wengine kama hivyo porini wakati wanatembea kwenda vituo vya afya. Sasa huyo unategemea akivuja damu nyingi, anawezaje kupona? anahoji.

NINI KIFANYIKE?

Dk. Telatela, ambaye ni mtaaluma na muathirika wa tukio hilo, anashauri serikali ihakikishe katika benki za damu ilizojenga katika kila mkoa, ziwe na akiba ya damu ya kutosha.

Naye Livingstone anaishauri serikali kuwa makini weakati wa kuajiri wataalam wanaomudu majukumu ya uzazi, kwani ni mazito na ya hatari, huku ikiwa makini dhidi ya uzembe.

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya, anasema serikali bado ina wajibu wa kuhakikisha inaboresha vituo vuya afya vilivyopo, kwa kuweka huduma zote muhimu za uzazi, ikiwamo watumishi wenye ujuzi na kuongeza idadi ya vituo, ili kupunguza tabu wanayopata kinamama wakati wa kujifunguia.

Mbunge Mariam Msabaha(Viti Maalum), anasema tatizo la ukosefu wa wataalam wa kutosha kushughulikia masuala ya uzazi, ni vyema elimu ikapanuliwa kwa wakunga waliopo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Hawa Ghasia, anawaomba wabunge kuwa mstari wa mbele kuipigia kelele serikali, ili katika bajeti zake ikumbuke kutenga fedha za kutosha kushughulikia huduma za afya.

''Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, ninakiri kabisa kwamba suala la uzazi salama bado halijapewa kipaumbele na hili ni kwa sababu, halizungumzwi. Watu wanaliona kama la kawaida, wakati wanawake na watoto wanazidi kuteketea,'' anasema.

''Sisi wabunge tumekuwa tukitembea na kushuhudia wanawake na watoto wanavyokufa na wengine kati yenu hapa ni waathirika. Vifo hivyo vinatokana na kukosekana huduma za dharura za uzazi ikiwamo damu, vifaa tiba na huduma nyinginezo muhimu zinazohitajika wakati wa kujifungua. Tusiposema haya yote, hakuna atakayejua tatizo hili ni kubwa kiasi hiki hata wapanga bajeti hawatafahamu.''

Anaahidi katika bunge lijalo, watahakikisha suala hilo linapewa kipaumbele.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge, Peter Serukamba, anasema tatizo linalochangia huduma hizo za zisitengewe bajeti ya kutosha, ni kutokana na mfumo usiofaa wa upangaji bajeti katika wizara husika.

Aidha, Meneja Mradi wa Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama(WRTZ), Sizarina Hamisi, anasema kuwa utafiti walioufanya, umebaini zaidi ya Halmashauri 40, kwenye bajeti zao hazikutenga pesa ya kushughulikia huduma hizo muhimu na na hata pesa zikitenghwa kwa matymisi hayo, zinaelekezwa kwingine.

Makamu Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge Wanaoshughulikia Masuala ya Uzazi Salama, Magreth Sitta, anaahidi katika Bunge lijalo, wamepanga kuwakutanishaa wabunge ili kupanga mikakati ya kushughulikia tatizo lililopo.

Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe, Rose Mlay, anasema, kuna haja makundi mbalimbali ya kijamii, viongozi wa serikali kuu na za mitaa, kupigia kelele tatizo hilohasa katika bajeti za Halmashauri.

Mlay anasema kunapaswa kuwapo mjadala wa kitaifa kuhusu idai ya wanawke 24 wanaopoteza maisha kila siku, kutokana na mataizo ya uzazi, takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani.

WAZIRI UMMY MWALIMU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anataja sababu kubwa za inazosababisha vifo vya wanawake ni kutokwa na damu nyingi, ambalo linachangia asilimia 90 ya vifo vyote vya uzazi.

Anasema, kuna haja kuwapo hali ya kujitosheleza katika huduma muhimu na wataalam wenye uwezo wa kushughulikia masuala ya uzazi katika vituo vya afya na kwingineko kunakopatikana huduma.

Kuhusu suala la upatikanaji damu salama, anasema ametenga Sh.bilioni 10 katika bajeti mwaka huu, kusaidia hilo na kwamba Wizara yake imeamua iwe na benki ya damui kila mkoa, badala ya kuwa nayo katika kila mkoa.

''Katika Baraza la Mawaziri, nina wahakikishia tutaendelea kuzungumzia hili suala,” anasema Waziri Ummy na kuahidi kupigana katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo zito.

Habari Kubwa