Nachingwea katika operesheni ya kumilikisha vijiji utajiri wa misitu

03Mar 2016
Mashaka Mgeta
Aliyekuwa Nachingwea
Nipashe
Nachingwea katika operesheni ya kumilikisha vijiji utajiri wa misitu

MSEMO wa penye miti hapana wajenzi, sasa unatoweka kwa jamii za vijiji vilinavyomiliki misitu katika wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.

Sehemu ya uharibifu unavyofanyika kwenye misitu ya wilayani Nachingwea, mkoa wa Lindi. (Picha: Na Mashaka Mgeta)

Hali hiyo inatokana na vijiji vitatu kati ya 12 vinavyomiliki misitu ya hifadhi kuanza kunufaika kwa mauzo ya mazao yanayotokana na rasilimali hiyo.

Mazao hayo ni kama miti na magogo kwa ajili ya wafanyabiashara ya mbao, ufugaji nyuki na uchomaji mkaa. Vijana pia hujipatia ajira ya muda kamavibarua kwa wanaovuna mazao hayo.

Hata hivyo, manufaa yanayopatikana kwenye sekta hiyo, yanaelezwa kuwa kichocheo cha wasiomiliki misitu kutaka kuharakishwa kwa utekelezaji wa mpango huo, ili kuwadhibiti vijana na wanavijiji kwa ujumla, wasishawishike kushirikiana na wahalifu wa misitu.

Kabla ya vijiji kumilikishwa misitu kwa mujibu wa sheria na kubuniwa kwa mpango shirikishi, taifa lilikabiliwa na ongezeko kubwa la uharibu wa rasilimali hiyo kiasi cha kuathiri uchumi wa taifa.

Mathalan, ripoti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka jana, ilionyesha jumla ya hekta 372,000 za misitu zilipotea, kutokana na uharibifu na shughuli za binadamu katika maeneo yanayosimamiwa na halmashauri za wilaya.

Lakini wilayani Nachingwea, kunaelezwa hivi sasa hakuna msitu unaomilikiwa na halmashauri, isipokuwa vijiji na mingine ikiwa katika mchakato wa kumilikishwa rasmi vijijini.

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Nachingwea, Paiton Kamnana, anataja vijiji vinayomiliki misitu wilayani humo ni Chimbendenga, Mtua, Nahimba, Nakalonji na Majonanga. Vngine ni Ngunichile, Namatunu, Ntira, Rupondo, Mtumbatu, Kilimarondo na Matekwe.

Kamnana anayezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, anasema vijiji vya Ngunichile, Kilimarondo na Matekwe pekee. vilikuwa vinamiliki na kuvuna mazao ya misitu kwenye rasilimali hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ngunichile, Seif Ng’wang’wa, anasema mchakato wa kijiji hicho kumiliki msitu wa Namitonga ulianza Septemba mwaka jana na hadi Januari mwaka huu, kibali cha uvunaji kiklikuwa bado kutolewa.

Kwa mujibu wa Ng’wang’wa, msitu huo ulikuwa na ukubwa wa ekari 2,248, lakini ukavamiwa na wakulima kutoka Newala walioweka makazi ya kudumu.

Anasema wakati huo wakazi wa kijiji hicho waliendelea kuuhifadhi na kuulinda msitu huo, licha ya kuwa bado hawajaruhusiwa kuvuna mazao yake.

Hifadhi hiyo inachangiwa na mipango ya uelimishaji na uhamasishaji unaofanywa na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) kwa ufadhili wa Finland.

Kimsingi, vijiji vinavyomiliki misitu, vinapata manufaa kama kusamehewa mrabaha wa serikali, kwa mazao ya misitu katika misitu wanayoihifadhi na wanayoisimamia na kubakiza asilimia 100 ya maduhuli.

Ofisa huyo anasema vijiji husika vinaruhusiwa kutoza faini kwa waharibifu wa misitu na kutaifisha mazao ya misitu na zana zilizotumika kufanya uhalifu.

Wilayani Nachingwea,vijiji ambavyo havijapewa vibali vya kuvuna mazao ya misitu hivi sasa vipo katika mchakato wa kufikia hatua hiyo, ili mapato yatakayopatikana yasaidie kugharamia huduma za jamii.

KAULI KUTOKA KIJIJINI

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wenzake wa kijiji hicho, Bakari Lilomba, anasema wana mahitaji ambayo wakiruhusiwa kuvuna mazao ya msitu huo, itachangia kugharamia huduma za jamii.

Naye Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Selemani Soya anasema wamejiwekea malengo kadhaa yanayopaswa kufikiwa kutokana na mapato yatakayotokana na mazao ya misitu.

Mahitaji hayo ni pamoja na ununuzi wa trekta kwa ajili ya shughuli za kilimo, upatikanaji maji safi na salama, ujenzi wa zahanati hususan wodi ya kujifungulia na nyumba za walimu.

Lakini wanakijiji hao wanakabiliwa na matatizo mengi katika maisha yao. Tatizo moja kubwa wanalolitaja ni uhaba wa maji, jambo linawalazimu kufuata maji kwenye mto Mbwemkuru, uliopo umbali wa takribani kilomita 6.5.

Lilomba anasema, kuendeleza mchakato pasipo kutoa vibali vya uvunaji kwa vijiji vilivyokamilisha hatua za umiliki wa misitu, kunaweza kusababisha wakazi wa kijiji hicho wasiokuwa waaminifu, kuwasaidia majangili kuihujumu rasilimali hiyo.

“Wananchi wamehamasika na wanachohitaji sasa ni kuona wananufaika kwa mazao ya misitu wanayoisimamia na kuilinda, vinginevyo watatokea wa kuwasaidia ama kushirikiana na wahalifu wakaiharibu,” anasema.

WANAWAKE WASHIRIKI

Maua Chila ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, anayesema kuwa mwamko wa wananchi kushiriki ulinzi na uhifadhi wa msitu umewachochea wanaume wenye wanawake walio wajumbe wa serikali ya kijiji, kuwaruhusu kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Awali isingekuwa rahisi kwa mwanaume kumruhusu mke wake kwenda doria msituni, lakini kwa kutambua umuhimu wa msitu na manufaa yake kwa jamii sasa tunapewa ruhusa na fursa pana ya kushiriki,” anasema Chila.

Chila anasema bado ulinzi wa misitu hiyo unafanywa kwa ushirikiano wa askari wa wanyamapori, skauti na kamati za maliasili za vijiji, ingawaje bado wanakabiliwa na
changamoto kama vile kukosa silaha za kuwakabili wahalifu wa misitu.

Kamnana anasema kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), kumechagiza kuwepo kasi ya ufanisi wa umiliki, usimamizi na uhifadhi wa misitu na ongezeko la nguvu kazi hususan watumishi na rasilimali.

Anasema vijiji kuufaika na biashara ya mazao ya misitu, ari ya wakazi wake kushiriki katika uhifadhi wa rasilimali hiyo imekuwa kubwa, hivyo kupunguza kiwango cha uvunaji haramu wa mazao yake.

“Mwanakijiji anapouona msitu kuwa ni mali yake inayomnufaisha, ni dhahiri kwamba atashiriki ipasavyo katika kuulinda dhidi ya vitendo viovu kama uvunaji haramu na uchomaji moto,” anasema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Ngunichile, Ng’wang’wa anasema ujangili ni tatizo linalotokea zaidi nyakati za usiku kwa vile wajumbe wa kamati za maliasili kutokuwa na uwezo wa kufanya doria kutokana na ukosefu wa vitendea kazi kama magari na silaha za kisasa.

“Wakati mwingine tunasikia ‘chain saw’ (misumeno mikubwa) inapotumika kukata miti msituni, lakini tunashindwa kwenda kuwadhibiti kutokana na ukosefu wa vitendea kazi,” anasema.

FAIDA KWA HALMASHAURI

Kamnana anasema, kwa sababu vijiji ni sehemu za halmashauri za wilaya, kwa namna vinavyonufaika kutokana na mapato ya mazao ya misitu, inakuwa ni faida kwa halmashauri husika.

“Vijiji vinapopata fedha kwa ajili ya maendeleo ya kijiji, shughuli zinazofanyika zinaondolewa kwenye mipango ya utekelezaji ya halmashauri hivyo (fedha) ambazo zingetumika, zinaelekezwa kwa matumizi mengine,” anasema Kamnana.

Mbali na manufaa hayo, Kamnana anasema Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya inapokea asilimia tano ya malipo ya mazao ya misitu.

MITI ADIMU

Kamnana anasema misitu ya wilayani humo ina miti adimu na iliyo bora, lakini manufaa yake hayajajulikana, hivyo kushindwa katika ushindani wa soko.

Anasema kinachofahamika zaidi ni uwapo wa miti kama vile Mtumbati (Mninga), Mbambako (Mkongo), Mtomwi, Njale, Chibulele, Chihimbili na Nchenga.

Hata hivyo Kamnana anasema miti mingi bora, inastahili kutangazwa ili kuwawezesha wafanyabiashara wawasilishe maombi ya kuivuna.

Anatoa mfano wa miti hiyo kuwa ni Mpande anaodai kuwa ubora wake unazidi aina nyingine za miti ikiwamo Mninga, Mpingo na Mkongo.

Kamnana anasema kuendelea kuwapo miti bora na isiyovunwa, kunasababisha kupoteza thamani ya ubora wake na inaishia katika kuharibika.

Anasema ni hali iliyosababisha msitu kupimwa upya ili kuziepusha jamii zinazoishi katika eneo hilo kuingia katika mgogoro na mapigano, hivyo ukubwa wake ukawa hekta 1,800.

Habari Kubwa