Naibu Waziri alipotua Moshi kusaka jibu la kahawa ‘kudoda’

10Jan 2020
Mary Mosha
Moshi
Nipashe
Naibu Waziri alipotua Moshi kusaka jibu la kahawa ‘kudoda’
  • TACRI wafunguka jitihada zao, wanakoishia
  • Ni ‘madudu’ halmashauri hadi ofisa ugani

MKOA wa Kilimanjaro, ni miongoni mwa mikoa nchini Tanzania iliyokuwa iikisifika kwa uzalishaji wa kahawa bora na yenye kukubalika kimataifa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, akipewa maelezo na mtafiti kutoka Tacri,

Hiyo ilikuwa mbali na kuwa kahawa ilikuwa ikipatikana maeneo ya Uru, Kibosho, Marangu, Machame, Siha, Rombo.

Pia wazee wa Kichaga walilifanya kuwa zao la biashara lililowasaidia baadhi ya watoto kunufaika kwa kupata elimu bora iliyoleta tija katika taifa.

Katika miaka ya 1990, zao hilo lilianza kudorora kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya tabia nchi na mabadiliko ya kiuchumi yaliyochangia dawa kupanda, huku nguvu kazi ya vijana ikikimbilia mijini na kuwaachia wazee zao hilo.

Pia, soko la kahawa kutokana na ukosefu wa mpango mkakati, imekuwa likizalishwa chini ya kiwango na kusababisha kushuka kwa soko la umoja wa kimataifa.

Serikali iliamua kulivalia njuga kilimo cha kahawa, na vyama vya ushirika vilivyokuwa vikisimamia uzalilishaji ikibaini madudu.
Ni mkakati wa serikali wenye mchango mkubwa wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, imeweka msukumo mkubwa.

Katika kulitimiza, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, alitua mkoani Kilimanjaro katika taasisi ya Tafiti ya Kahawa (Tacri), kupata ufafanuzi wa kinachoendelea.

KUTOKA TACRI

Mkurugenzi Mkuu wa Tacri, Dk. Deusdediti Kilambo, anasema wameshafanya utafiti na kubaini aina 23 za kahawa inayokabiliana na magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Dk. Kilambo anazitaja aina 19 za Arabika zenye tija kukabili magonjwa kama chulebuni na kutu ya majani, yenye muonjo mzuri na aina nne za Robusta, zenye ukinzani na minyauko fuzari.

“Katika kulitekeleza hilo, tulishaweka mikakati pamoja Bodi ya Kahawa nchini (TCB), kubadilisha miche zaidi ya milioni 20 kwa kila mwaka, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata miche ya kisasa,” anasema.

Anasema, hadi kufikia sasa, Tacri ina uwezo wa kuzalisha miche milioni sita hadi saba kwa mwaka, hali ambayo haijafikia malengo ya kuondoa miche ya zamani na waliazimia kubadilisha miche milioni 20 kila mwaka.

Anasema, kulingana na takwimu zao hilo, bado kila mwaka tunamzigo wa kuzalisha miche bora zaidi ya milioni 14 au 13 ili tuweze kufikia lengo jambo ambalo limekuwa tatizo ingawa zipo baadhi ya halmashauri zinapewa miche mama, mbegu na wao wanajitegemea katika rasilimali fedha kwa ajili ya uanzishaji bustani.

“Zipo taasisi zinazo tuunga mkono ikiwamo vyama vya ushirika, halmashauri, mashirika binafsi na baadhi ya wakulima wadogo katika vikundi jambo ambalo ikiwa ushirikiano huo utaendelea kwa kasi tutaweza kufikia lengo na kubadilisha miche ya zamani ambayo itaweza kuleta maendeleo kwa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” anasema.

Sophia Malinga ni mtafiti katika kitengo cha Usambazaji, Teknolojia na Mafunzo, anasema sababu za kutokuwapo mwitikio chanya wa miche wanayosambaza, ni baadhi ya wakulima kutokuwa na uelewa wa utunzaji miche hiyo.

“Ni kweli hakuna ufuatiliaji wowote kitaalamu unaofanywa na halmashauri, baada ya kutoa miche hiyo hali inayowafanya baadhi ya wananchi kutoipanda au kupanda bila uangalizi maalumu unaoleta matokeo chanja,” anasema Mtafiti Sophia.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri huyo anasema, mbali na kuwapo kwa mipango mikakati iliyoonyeshwa na taasisi hiyo, lakini bado matokeo hayaonekani kwa mkulima mmoja mmoja na taifa.

"Kwa miaka 10 mfululizo serikali inazalisha kati ya tani milioni 48 hadi 60 licha ya jitihada za serikali kuongeza mikakati katika kuongeza uwezo wa uzalishaji kwa watafiti wake kugundua miche bora ya kahawa inayostahimili magonjwa," anasema.

Anafafanua kuwa, inaonyesha kuwapo tatizo la usimamizi na ufuatiliaji wa miche hiyo mara baada ya kuzalishwa na Tacri kwenda kwenye halmashauri na vyama vya msingi, vinavyopewa bila malipo na kufanya miche hiyo kutotunzwa na kuleta matokeo yanayoweza kuleta mabadiliko kiuchumi.

Anafafanua: "Zipo taarifa za ndani zinazoonyesha kuwa miche hii ya kahawa bora pamoja na mbegu zinazotolewa hazitunzi ipasavyo licha ya kutolewa bure.

“Serikali haitakubali kwani malengo yake ni kutoka kwenye tani elfu 48 hadi 68 tuliyopo kwa sasa hadi tani 200,000 ya kahawa safi kwa mwaka baada ya miaka 5 ijayo.

"Naziagiza halmashauri kote nchini pamoja na vyama vya msingi na vikundi vyote vinavyopokea miche kutoka Tacri, kuhakikisha zinaboresha kitengo cha usimamizi na ufuatiliaji wa taarifa ya miche ya kahawa kule inapokwenda ikiwa ni pamoja na kufahamu, kitongoji, kjiji kata pamoja na namba za simu za mkulima wanaopewa mche hiyo, na ukubwa wa maeneo wanayopanda.”

Agizo lake ni kwamba, mawasiliano hayo yasiishiwe kuweka kwenye halmashauri na vikundi, kwani zipo taarifa halmashauri nyingi zinakiuka malekezo ya Tacri, jambo ambalo serikali haitakubali.

Ushauri wake ni kuwapo kikosi cha ufuatiliaji kwa kila baada ya miezi mitatu hadi sita, kukagua matokeo ya upandaji na ushauri, kila kunakolimwa kahawa nchini.

“Tumepokea matatizo ya Tacri kuwa inakabiliwa na ufinyu wa bajeti na ukosefu wa eneo la uzalishaji (eneo lenye miundombinu rafiki ya kukuzia miche), tunayachukua kama serikali na tutayafanyia kazi,” anasema.

WAKULIMA & VYAMA

Mkulima wa Kibosho wilayani Moshi, Agustino Kishumbuo, anasema serikali itafuatilia uhakika kufahamu maeneo miche hiyo inakoenda, kusaka mabadiliko katika uzalishaji wa zao hilo.

“Zipo baadhi ya halmashauri huchukua miche hiyo bila kufahamu hali ya halisi ya wakulima katika maeneo yao na kutokana na uzembe mkubwa unaofanya na maofsa ugani katika kila halmashauri, kwani hawana muda na kilimo.

Anasema, bado taasisi Tacri haina nguvu kubwa ya usimamizi kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha na vitendea kazi. Anaendelea:

“Tunaiomba serikali kuangalia uwezekano wa kufanya usimamizi wa kutosha kutoka kwenye Tacri na mpaka kwa mkulima mwenye pia kuwepo na motisha kwa Mkulima atakayeweza kufanya vyema katika usimamizi na utunzaji wa kahawa.”

Agustino Mlay, mkazi wa Old Moshi, anasema vipo baadhi ya vyama vya msingi viongozi wao huchukua miche na kuiacha kukauka au kuwapa wakulima bila ujuzi wa namna ya kulima na kuipanda.

Anasema mpango wa serikali wa kuzalisha kwa tija zao hili la biashara, unaweza kuleta matokeo bora ikiwa haitafanywa kwa ubabaishaji.

Habari Kubwa