Naibu waziri ashtukia ubadhirifu Bilioni mradi wa maji Shinyanga

11Jan 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Naibu waziri ashtukia ubadhirifu Bilioni mradi wa maji Shinyanga
  • Akerwa ahadi aliyotekeleza kuchezewa
  • Aamuru mhandisi kuswekwa rumande
  • Ajitetea ushirikina kijijini unamkwamisha
  • RC, mbunge wanavijiji waorodhesha yao

KIJIJI cha Mwakitolyo kilichopo katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini, kina jumla ya wakazi 10,000 ambao shughuli zao kubwa za kiuchumi ni kilimo na uchimbaji madini ya dhahabu.

Mhandisi wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya Shinyanga Vijijini, Slivester, akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, baada ya kuagizwa na Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kijijini Mwakitolyo, Shinyanga vijijini.

Wananchi hao kwa miaka mingi, wamekuwa wakitaabika kupata maji safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku, ambayo pia yanatumiwa kunywa.

Katika maeneo hayo, yanaelezwa hapako salama kwa ajili ya kunywa na kuna mabwawa yanayotajwa kuwa na hatari ya kemikali, hivyo kutishia usalama wa maisha yao.

Sera ya Maji ya Mwaka 2002 inataka asilimia 85 ya wananchi wa maeneo ya vijijini wawe wamepatiwa maji safi na salama ifikapo mwaka 2020, huku mijini ifikie asilimia 100.

Katika kijiji hicho cha Mwakitolyo, kulianzishwa mradi wa maji wenye gharama ya Shilingi bilioni 1.482. ambao unaonekana kufanyiwa ubadhirifu wa fedha.

Mradi huo wa maji, ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na utakuwa ukitumia maji ya ziwa victoria kupitia mabomba ya maji yanayokwenda mjini Shinyanga, kutoka kwenye chanzo kikuu cha maji Ihelele wilayani Misungwi mkoani Mwanza. ili kuwaondelea adha wananchi wanaotumia maji machafu.

Tangu mwaka huo, 2014, mradi huo haujakamilika na kuanza kutoa maji kwa wananchi hao, huku mkandarasi wa kampuni moja ya jijini Dar es Salaam akiwa wameshalipwa Shilingi bilioni 1.462 na kubakia milioni 20 kinyume na utaratibu.

AWESO ASHTUKA

Kitendo hicho cha Mkandarasi kulipwa pesa zake kwa asilimia kubwa huku mradi wa maji ukiwa bado mbovu na kutotoa maji, kulimfanya Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kutia shaka kuwa huenda kuna mianya shaka ya harufu ya rushwa, akielekeza kidole kati ya Mkandarasi na Mhandisi wa Maji, katika mradi wa maji , kwenye Halmashauri ya Shinyanga Vijijini. (Silvester Mpemba).”

Aweso anakataa kandarasi kulipwa pesa zake takribani, wakati mradi huo bado uko katika hali mbaya na wananchi wanaendelea kutaabika kwa mbaya maji.

“Mwaka jana Februari, nilikuja kwenye mradi huu wa maji Mwakitolyo, nikaagiza hadi kufikia April uwe umeshakamilika, na mhandisi ukasema kuna upungufu wa fedha Shilingi milioni 120 na sisi kama wizara, tukatoa fedha hizo.

“Lakini, leo Januari 2019 nimekuta mradi huu bado haufanyi kazi na pesa zimeshalipwa kwa mkandarasi.Sisi kama wizara ya maji hatutakubali kuwapo na utumbo huu kwenye utekelezaji wa miradi ya maji maeneo haya ya vijijini.

“Hapa lazima kuna namna imefanyika na sitakubali Serikali iendelee kutukanwa na wananchi sababu uzembe wa wataalamu wasiopenda kufanya kazi kwa ufanisi,” anafafanua.

Katika hilo, Naibu Waziri Aweso, aliliamuru Jeshi la Polisi kumkamata Mhandisi wa Maji wa Halmashauri hiyo ya Shinyanga Vijijini, Sylvester Mpemba, ili kulichunguza suala hilo, kwani kuna usimamizi huo mbovu wa miradi mingi ya maji katika maeneo ya vijijini.

Naibu Waziri aliahidi kuwasiliana na Katibu Mkuu wa wizara yake, Profesa Kitila Mkumbo, kupitia wasifu upya, wasifu binafsi (CV) wa wahandisi wote wizara na kwake, pamoja na kuanzisha wakala wa maji vijijini, ili kumaliza tatizo la ubadhilifu huo katika miradi ya maji.

RC SHINYANGA

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, katika hilo anaeleza mkasa kwa upande wake kwamba, alipoenda kutembelea mradi huo wa maji, alikuta haupandishi maji kwenye tanki na alipoomba majibu kutoka kwa mhandisi huyo wa maji, Mpemba, akapewa majibu yasiyoridhisha, sambamba na mradi huo kuhusishwa na mambo ya kishirikina.

“Naomba wataalamu wetu acheni kuchezea fedha za serikali za walipa kodi. Msifanye kazi kwa mazoea, huu ni utawala mwingine.
“Tunataka miradi ya maji inayosuasua yote mwaka huu iishe, ikiwa tunakwenda kwenye kipindi kigumu cha uchaguzi. Sasa wananchi tutawaeleza nini?”analalamika Telack.

MBUNGE SOLWA

Ahmed Salumu, ni mbunge wa Solwa, anayesema mradi huo wa maji katika kijiji hicho cha Mwakitolyo, umekuwa ukimuumiza kichwa, kutokana na kushindwa kukamilika kwa wakati, kwani wananchi hao ambao ni wapiga kura wake, wamekuwa wakimsumbua kuhusu upatikanaji huduma ya maji safi na salama.

“Mradi huu mimi nimeufuatilia, una tatizo kubwa na unaohitajika kupangwa upya ( kitaalamu re - designing) kwa sababu umeshakosewa na siyo kufanyiwa marekebisho,” anaeleza Salumu na kuongeza;

“Ikiwa utatia gharama kubwa na matokeo yake kutofanya kazi tena na kuwa mradi hewa na wote waliohusika hapa wawajibishwe.”

WANA KIJIJI

Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mwakitolyo, Ruhi Shomi, anasema wamekuwa wakipata adha ya kutafuta maji safi na salama kutoka umbali mrefu katika vijiji jirani, ikiwamo Chan’gombe ambako ni wastani wa kilomita mbili hadi tatu, na wananchi wasio na uwezo wa usafiri, hutumia maji ya mabwawa ambayo ni hatari kwa afya zao.

“Eneo hili shughuli zetu kubwa ni kilimo na uchimbaji wa madini ya dhahabu na mabwawa ambayo hutumia watu kuchota maji yana hatari sababu ya kuwepo na ‘makemiko’ (kemikali) ya kuchenjulia dhahabu na ndio maana tunataka maji safi na salama ili kuokoa afya zetu,” anasema Shomi.

Saada Ally, ni mwana kijiji hicho cha Mwakitolyo, anayesema adha hiyo ya maji imekuwa ikiwaathiri shughuli zao za kiuchumi, kwa kupoteza muda mrefu wa kufuata maji safi na salama katika vijiji jirani, hivyo wanaanguka kimaendeleo.

“Maisha yetu sisi hapa kijiji ni ya gharama sana, tukiamua kutokwenda kufuata maji katika vijiji jirani inatubidi tununue maji ndoo moja kwa Shilingi 1,000 ambayo huletwa na wafanyabiashara wa magari. Hivyo, tunaomba serikali ifungue mradi huu wa maji na kutupatia afadhali ya maisha,” anasema Ally.

MHANDISI AJITETEA

Mhandisi wa Maji wa Halmashauri hiyo ya Shinyanga Vijijini, Mpemba, anasema mradi huo umekwama kutoa maji kutokana na kuwapo kwa imani za kishirikina akidai “Mabomba usiku yanapaa juu na mchana yanatulia na kugoma kutoa maji.

“Ni kweli mradi huu fedha zake tulipewa na wizara na tumeshampatia mkandarasi Shilingi bilioni 1.462 na kubakia Milioni 20, na gharama za mradi ni Shilingi bilioni 1.482.

“Nilikagua nikaona ni nzima, lakini tatizo ni ushirikina wa kuzuia mabomba kutotoa maji, ambao tunahitaji ‘booster’ kifaa cha kusukuma maji) ili kupandisha maji kwenye tanki,”anasema Mpemba.

PROFESA MKUMBO

Profesa Kitila Mkumbo, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, akizungumza kwa njia ya simu na Naibu Waziri wa Maji, Aweso, anasema atalazimika kutuma wataalamu kutoka wizarani kubaini tatizo na kulifanyia kazi, ili wananchi waweze kupata maji.

Habari Kubwa