Naibu Waziri Maliasili apigia debe hifadhi mpya iliyozinduliwa kwao

10Jan 2020
Alphonce Kabilondo
Geita
Nipashe
Naibu Waziri Maliasili apigia debe hifadhi mpya iliyozinduliwa kwao
  • Wakazi furaha ‘mpaka basi’, ombi lao elimu
  • RC Geita aorodhesha neema uchumi kibao
  • Mhifadhi Mkuu: Maajabu kibao, zahanati asili

Hapo aliibua shangwe kubwa na matumaini ya kipato kwa wananchi wa wilaya za Kyerwa, Karagwe, Muleba na Biharamulo, ambazo ni jirani na Chato.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu (wa pili kutoka kulia), akifurahia jambo na wakuu wa wilaya nane, katika Hifadhi ya Taifa Buigiri Chato. picha mtandao

Hapo aliibua shangwe kubwa na matumaini ya kipato kwa wananchi wa wilaya za Kyerwa, Karagwe, Muleba na Biharamulo, ambazo ni jirani na Chato.

Hifadhi hiyo mpya, kijiografia iko Kaskazini Magharibi mwa Tanzania katika mikoa ya Kagera na Geita. Pia, inadaiwa kuwa chachu ya kuinua uchumi kwa wananchi hao jirani, pamoja na pato la Taifa kwa ujumla kupitia utalii.

Hifadhi hiyo ina eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 4707 na inatajwa kushika nafasi ya tatu kwa ukubwa, nyuma ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Hifadhi hiyo inatokana na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuyapandisha hadhi mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo, Kimisi (BBK) na Rumanyika, hatua iliyoidhinishwa kwa uzinduzi wa Rais Magufuli.

Sekta ya Utalii nchini inatajwa kuchangia pato la Taifa kwa takribani asilimia 17, kutoka kwa watalii zaidi ya milioni 1.5 wanaofika nchini kutembelea vivutio mbalimbali.

Baadhi ya vivutio vilivyopo nchini na kutambuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) ni pamoja na Arusha, Gobe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, Serengeti,
Saadan,Tarangire, Uduzungwa, Kitulo, Mkomazi Saanane na Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita hifadhi mpya ya Burigi Chato.

WANANCHI

Wakazi jirani wanaipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Rais Magufuli, kwa kupandisha hadhi mapori hayo kuwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato.

Wakazi wa Biharamulo wanasema mapori hayo kupandishwa hadhi, pia kunawahakikishia usalama wao na kuendesha shughuli za ufugaji wa mifugo pamoja na kilimo bila kufuata taratibu za sheria.

“Tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kutupatia elimu kuhusu utalii kwa makundi ya vijana na wazee, jambo la utalii ni geni Kanda ya Magharibi,” anasema mkazi wa Nyakahura Sizya kupatiwa elimu kuhusu utalii.

Juma Sizya, mkazi wa Nyakahura Wilaya ya Biharamulo, Kagera anaeleza matumaini walio nayo ni kunufaika na kuanzishwa kwa hifadhi hiyo, licha ya kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu masuala ya utalii naye akirejesha ombi kwa wizara mama kuwaelimisha kuhusu utalii.

Mateso Pius, mkazi wa kijiji na kata ya Nyakabango, wilayani Muleba, mkoa Kagera, kilichopo umbali wa kilomita 10 kutoka iliko hifadhi hiyo, anasema kuwa kitendo cha serikali kuyapandisha hadhi mapori hayo kuwa Hifadhi ya Taifa, ni mwarobaini dhidi ya matukio ya uhalifu kwenye barabara ya Mwanza, Geita Muleba Bukoba na Biharamulo.

Mateso anaongeza, ilhali utalii unakuja, kuna faida na hasara zake, kwa ni ajali kuna mashamba na makazi yanayoingia ndani ya eneo la hifadhi, itabidi kuhamishwa.

MBUNGE

Mbunge wa Biharamulo, Ossca Mkasa, anasema asilimia 54 ya eneo la wilaya hiyo ni hifadhi. Pia matumaini ya wananchi wake ni kuona uchumi wa wilaya hiyo na Taifa kwa jumla unapaa kupitia sekta ya utalii.

Anasema, wakazi wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya aina mbalimbali, pia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wana wajibu wa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakazi wa wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo.

Mkasa anasema Tanapa wanatakiwa kutoa elimu kwa kuwashirikisha madiwani wa halmashauri za Biharamulo, Karagwe, Muleba, Kyerwa na Chato, ili kuwajengea uwezo wa masuala ya utalii, kwani wengi wao bado hawautambui vizuri utalii.

Anasema, kiu yake kubwa pindi mradi huo utakapoanza rasmi ni kuona Tanapa inawawezesha wakazi wa vijiji hivyo kwenye sekta ya kilimo kupitia fedha ya huduma ya jamii, kwa kuwa wakazi hao wanategemea kilimo cha mazao ya chakula na biashara, hali iyakayosaidia kujenga uhusiano mzuri kwa jamii inayozunguka hifadhi mpya.

Mbunge huyo anakiri, kabla ya mapori kupandishwa hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa, hali ya usalama ilikuwa si shwari sana, kutokana na mapori kukosa ulinzi sahihi, kuna matukio ya magari kukumbwa na uhalifu.

Pia Mkasa anafafanua kwamba halmashauri jirani zilipoteza mapato ya ushuru wa mazao ya misitu.

RC GEITA

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi, anasema Hifadhi ya Burigi Chato, katika ukanda wa Magharibi itachangia kuwepo idadi kubwa ugeni wa watalii kwa hifadhi, kutokana na kuwapo kiwanja kikubwa cha ndege cha kimataifa wilayani Chato.

Alipozinduliwa hifadhi hiyo, Rais Magufuli, alisema inafungua milango ya fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa Geita na mikoa jirani, kuwekeza katika Sekta ya Maliasili na Utalii, ikiwamo ujenzi wa hoteli za kitalii, sambamba na utangazaji utalii.

Mkuu wa Mkoa Luhumbi, anasema mbali na hifadhi hiyo mpya ya Burigi Chato, mkoa wa Geita una Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa Cha Rubondo, ambacho kiko pembezoni mwa Ziwa Victoria.

“Kwa wageni wasiokijua kisiwa hiki, kinaundwa na visiwa tisa vidogo. Kisiwa hiki pia ni makazi na mazingira ya kuzaliana samaki, wakiwamo sato na sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo zaidi ya 100,” anasema Mkuu wa Mkoa.

Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na kiboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi, wanaobadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hiyo kama sokwe, tembo, mbega weusi na weupe na twiga.

WAZIRI KANYASU

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Geita Mjini, John Kanyasu, anaiambia Nipashe kuwa Tanzania inatajwa kushika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii, baada ya nchi ya Brazili.

Kanyasu anasema, hivyo idadi ya watalii hao wanatembelea hifadhi mbalimbali nchini bado haitoshi kutokana na uwepo wa vivutio vingi na anakiri kuwa Sekta ya Utalii.

Anasema, hifadhi hiyo mpya inatarajia kupata watalii wengi hata kutoka nchi za jirani za Kenya, Burundi, Rwanda.

Kanyasu anasema, nchi nyingi duniani zimefanikiwa katika Sekta ya Utalii, kutokana na wananchi wake kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi zao.

Anasema wizara yake, imeanza kampeni ya kuwatumia viongozi wa serikali, kama wakuu wa wilaya na mkoa kuhamasisha wananchi kutalii kwenye vivutio jirani.

Niabu Waziri huyo, anasema viongozi hao wanapotembelea Hifadhi za Taifa, wakaelimishwa fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii watakwenda kuhamasisha taasisi mbalimbali shule za sekondari msingi pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu, hali itakayosaidia kuongeza mapato katika sekta ya utalii.

Hata hivyo, anasema lengo la Wizara ya Maliasili na Utalii, ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 idadi ya watalii wanaofika kutembelea hifadhi za Taifa inaongezeka na kufikia zaidi ya milioni mbili kwa mwaka, ili kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.

Naibu Waziri Kanyasu akatumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wakazi wafanyabiashara wa mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza pamoja iliyopo jirani, wabuni kuwekeza kwenye hifadhi mpya ya Burigi Chato.

Anasema, baada ya hifadhi hiyo kutangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa Julai 5 mwaka juzi, Tanapa walitengeneza miundombinu ya barabara na viwanja vidogo vya ndege hifadhini, ikiwa ni hatua mojawapo kuweka mazingira mazuri kwa watalii.

Pia anaongeza, wizara hiyo huzingatia sheria kwa kuwapa kipaumbele ajira za muda na wakazi wanaoishi kuzunguka katika hifadhi.

VIVUTIO

Ofisa Mhifadhi Mwandamizi, Hera Haima, anasema Hifadhi ya Burigi Chato, inasifiwa kuwa ‘Serengeti ya Pili’ kutokana na wanyama wengi pamoja na mazingira mazuri ya kuvutia watalii, yanafanana.

Mhifadhi huyo anaelezea ndani ya Msitu wa Rumanyika, kuna kivutio cha maji moto kinachotumika kutibu magonjwa mbalimbali; Msitu wa Mutagata uliopo katika kijiji cha Kamuli Wilayani Kyerwa na kivutio cha maajabu cha kutibu tiba asilia.

“Msitu wa Rumanyika kuna kivutio cha maji moto kinachotumika kutibu magonjwa mbalimbali, pia katika Msitu wa Kijiji cha Mutagata, una kivutio cha maajabu kinachotumika kutibu watu wagonjwa pamoja na waliovunjika miguu,” anasema Mhifadhi Mwandamizi Haima.

Anaongeza kuwa, wagonjwa mbalimbali wakiwamo watu waliovunjika miguu na wenye kifafa, wamekuwa wakifika kutibiwa na kupona kivutio hicho kimekuwa kimbilio kwa wagonjwa lukuki misiri ya hospitali ya rufani kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu.

Tabibu Rubanda Kayanda, anasema kabla ya mgonjwa kupatiwa matibabu, ni lazima kufuata masharti yanayotakiwa, ikiwamo kufunga jiwe kwenye jani la mgomba na kisha kuliweka juu ya kisima na kunawa maji usoni mara tatu na kunywa mara tatu, kisha kuanza matibabu.

Kayanda anasema, chanzo hicho cha maji kinatibu watu magonjwa mbalimbali eneo hilo kuna nyoka mkubwa ambaye amekuwa akitokea kwa nyakati tofauti, kutumia maji hayo na hairuhusiwi kumjeruhi wala kumuua kwa kuwa hana madhara kwa binadamu.

MHIFADHI MKUU

Mhifadhi Mkuu wa Burigi Chato, Damiani Saru, anataja vivutio vya wanyama ambao ni twiga pofu, pundamilia, nyati, swala, pala, nyemera, tohe,kuro,chui ,fisi pamoja na aina ya ndege wenye rangi za kuvutia wakiwemo ndege mwarabu ,hondohondo, tai, bata maji.

Aidha, anataja wanyama wa majini kama samaki, mamba na kiboko walioko ndani ya hifadhi hiyo, huku akiwahakikishia wawekezaji watalii usalama wao.

DC ZIARANI

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mkoa Morogoro Siriel Shaidi, aliyekutwa na Nipashe hifadhini, anaishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha ufugaji nyuki kwenye hifadhi hiyo, kutokana na kuwa na eneo kubwa na mandhari ya kuvutia kwa watalii.

Habari Kubwa