Nani wa kumfunga pake kengele Z’Bar?

22Jun 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Nani wa kumfunga pake kengele Z’Bar?

SIASA za chuki na uhasama zinaendelea kuvitikisa visiwa vya Zanzibar haswa kisiwani Pemba ambako ni ngome ya Chama Cha Wananchi (CUF).

mti wa karafuu

Uhasama umetokana na wafuasi wa CUF kutoridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kufuta uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kurudiwa Machi 20, mwaka huu.

Kitendo hicho ndicho kilichozaa siasa hizo za chuki na uhasama kwa kuhusisha migomo, hujuma za kukata miti mbalimbali, uchomaji wa moto na kususia mazishi, harusi na shughuli nyingine za kijjamii.

Hivi sasa kisiwani Pemba kumeibuka matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani ikiwamo hujuma dhidi ya mikarafuu, minazi na miti mengine ya matunda; vitendo vinadaiwa kufanywa na wafuasi wa CUF kwa kuhujumu mazao katika mashamba ya wafuasi wa CCM na wafuasi wa vyama vyingine waliyoshiriki katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20.

Kutokana na kushamiri kwa matukio hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Wakulima Tanzania (AFP), Said Soud Said, ambae shamba lake lenye mikarafuu limeharibiwa, amemwomba Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania kuichukulia CUF hatua za kisheria kwa kile alichodai chama hicho kimeanza kupotea mwelekeo kutokana na vitendo vya hujuma zinazofanywa na wafuasi.

Said anasema CUF kimekuwa kikiwashawishi wafuasi wake kufanya hujuma kwa kung’oa mazao ya wakulima pamoja na kugawa matabaka.

Kwa mujibu wa Said, CUF kinawagawa wananchi kikanda, kichama, kijamii na kwamba kufanya hivyo kunadhihirisha chama hicho kimepoteza sifa ya kuwa chama cha siasa.

“Vyama vya siasa sio ugomvi wala mfarakano, vimeletwa ili watu waingie na kuchagua kiongozi ambaye wanamtaka kwa ajili ya kuwaletea maendeleo, lakini ikiwa leo hii, unawaambia watu waanze kutofautiana kwa sababu ya siasa ni kuwa umepoteza sifa na msajili namuomba achukuwe hatua za makusudi za kukifuta,” anasema.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni miongoni mwa waathirika wa matukio hayo na wiki iliyopita shamba lake la ekari moja na nusu likiwa na minazi 16, mikarafuu 165 na mihogo vishina 250 liliharibiwa kwa miti hiyo kukatwa na baadhi kung’olewa.

Analalamika kuwa mambo yanayoendelea visiwani Pemba ni viashiria vya kuanza kupotea kwa amani ya Zanzibar na kumwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuimarisha ulinzi ili amani isipotee.

“Yanayotendeka kwa upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano yanaashiria vita, kwani Burundi, Rwanda na nchi nyingine walianzia hivyo hivyo na sote tumeshuhudia watu wakiuana,” anasema.

Anaongeza: “Namshauri Msajili wa vyama vya siasa Tanzania kwa mara nyingine tena aende Pemba akaangalie mwenendo wa CUF je, kinastahili kuwa chama cha siasa?...haiwezekani Tanzania ni moja kuna hujuma zinafanyika, vyama vya siasa vina utaratibu wake na anaevikiuka anastahili kuchukuliwa hatua.” anasema.

Aidha, anasema uchaguzi umeshamalizika, rais ameshapatikana na Serikali imeshaundwa na kwamba kazi iliyopo ni kujenga nchi kwa maendeleo ya taifa.

“CUF niwaambie ukweli usiofichika kwamba uchaguzi umemalizika na kilichobakia ni kuheshimu sheria za nchi ili kuleta maendeleo,” anasema.

Kuhusu uharibifu kwenye shamba lake, anatoa siku 14 kwa wahusika kujisalimisha kwake kabla hajachukuwa maamuzi ‘mengine.’

Bushura Omar Faki ni mwanachama wa CUF, Micheweni Pemba, anathibitisha kuwapo kwa hujuma mbalimbali ikiwamo suala la migomo huku akisisitiza kuwa hawana njia nyingine ya kufanya na hiyo inaweza kusaidia kuonyesha kukataa yaliofanywa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwa kufuta Uchaguzi wa Oktoba 25.

“Sisi kama wanaCUF na wengine wapenda demokrasia, tumechukizwa sana na yaliofanywa na ZEC na ndio maana hatuna njia nyingine ila ni kutoshirikiana na wanaCCM,” anasema.

Anasema migomo hiyo na kutoshirikiana na wanaCCM ni maagizo rasmi ya Baraza Kuu la chama hicho lililokaa mapema Aprili, mwaka huu.

“Sisi wanachama wa CUF kilichopo ni kutekeleza maagizo ya chama taifa, kwamba tuwadharau na kutoshirikiana na viongozi na wanaCCM kwa sababu wametunyang’anya ushindi wetu,” anasema.

KAULI ZA VIONGOZI WA DINI

Baadhi ya viongozi wa dini wameonyesha kutofurahishwa na hali ilivyo sasa kisiwani Pemba ya watu kushindwa kuzikana na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii kutokana na itikadi za vyama vya kisiasa.

Sheikh Omar Mohamed wa Wete Pemba, anasema lazima jamii ambayo imezaliwa kwenye kizazi cha Kiislamu, waweke mbele maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu, kuliko ya kiongozi mwengine wa chama.

Anasema dini ya Kiislamu inasisitiza waumini wake kupendana, kushirikiana, kuamrishana mema na kukatazana mabaya.

Anasema haipendezi na wala kidini haikubaliki jambo la kususia maiti kwa itikadi za kisiasa au kufanyiana hujuma mbalimbali kwa makusudi kwa lengo la kukomoana.

“Kwa hali ilivyo kisiwani Pemba, watu wamesahau kufuata miongozo ya kitabu kitakatifu cha Qur-an, na sasa wanafuata maagizo na makatazo ya vyama vyao vya siasa,” anasema.

Mchungaji Benjamen Kissanga wa Kanisa la KKKT usharika wa Chakechake Viotongoji Pemba, anasema kitendo cha kumsusia mwezio ni sawa na kupingana na makatazo ya Mungu.

Anasema Biblia Takatifu inasisitiza binadamu kuishi kwa kupendana na kusaidiana na sio jambo zuri kumgomea mwanadamu mwezako.

Anawataka wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kufuata maamrisho ya dini yake akisisitiza upendo, kuamrishana mambo mema na kukatazana maovu.

HATUA ZA KIPOLISI

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kusini Pemba Shekhan Mohammed Shekhan, anasema watu zaidi ya wanane wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo mikarafuu.

Anasema upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Anawataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kuwafichua wahalifu ili kukomesha hujuma zinazoendelea.

Zaidi ya matukio nane ya uharibifu wa miti ya mazao ikiwamo mikarafuu yameripotiwa kisiwani Pemba baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20.

Habari Kubwa