Ndivyo changamoto zilivyowaletea  mafanikio wajasiriamali wafugaji

18Nov 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Ndivyo changamoto zilivyowaletea  mafanikio wajasiriamali wafugaji

AMA kweli penye nia pana njia, ndivyo wanavyosema vijana wajasiriamali Ambonisye Ambwene na John Kafyome, wawili hawa licha ya kukwamishwa na changamoto nyingi waliruka viunzi na kuibuka wawekezaji wabunifu wa ufugaji samaki.

Moja ya bwawa la kufuga samaki. PICHA : BEATRICE SHAYO.

Wakiwa na elimu ya kidato cha sita, wanaieleza Nipashe jinsi ilivyokuwa vigumu kufanikisha ufugaji samaki ulioko Kitunda jijini Dar es Salaam, wakati gazeti hili lilipowatembelea hivi karibuni.

Wakianza na walikotoka wanataja mambo yaliyowakwamisha kuwa ni kupata chakula cha samaki jambo wanalolielezea kuwa ni changamoto kubwa katika sekta ya ufugaji wa samaki nchini.

“Wauza chakula si waaminifu, huandaa chakula kisicho na ubora kinachochangia kuua samaki.Baadhi ni wadanganyifu badala ya kuweka dagaa wanatumia mashudu ya pamba. Wanapotakiwa kuweka damu wanaweka udongo mwekundu.” Anasema Ambwene.

Anafafanua kuwa, chakula bora ni mchanganyiko wa mahindi, soya, dagaa pumba za ngano, vitamin C na maji na kuchanganywa zaidi kitaalamu na kukifanya kiwe kama punje zinazoshikamana.

“Ukosefu wa chakula bora unadhuru samaki, lakini wafugaji wengi hawafahamu ,” anasema Ambwene ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Green Fish Investment na kueleza kuwa asilimia kubwa ya wauzaji chakula hicho si waaminifu bali hujali kupata faidi zaidi.

Anapoeleza hasara iliyotokana na chakula kibovu anasema: “Mabwawa matatu yaliyokuwa yamejaa samaki wote walikufa tena ilikuwa imebaki miezi miwili tuwauze. Walikufa baada ya kupasuka vichwa na tukaambiwa tatizo ni kukosa vitamin C kwenye chakula. ”

Anataja umuhimu wa chakula bora kwa kambale kuwa ni utelezi na kinapokosa ubora kinasababisha mwili wa samaki hao kuwa mkavu badala ya kuteleza na samaki kufa. “Ndiyo maana tukalazimika kujifunza kutengeneza chakula.”

Anasema wakati wanajifunza kuzalisha chakula cha samaki walibaini kuwa tatizo liko kwa watengenezaji kwani wanakosa uwiano wanapokichanganya.

“Baada ya kufanikiwa kutatua changamoto ya chakula, tuligundua kuwa samaki hawakui kwa muda unaotakiwa. Tukafuatilia mitandaoni kuona wenzetu wanafanyaje. Tukagundua kuwa ni uduni wa teknolojia sisi tupo nyuma sana ndiyo maana hawakui kikamilifu,” anasema Ambwene.

Anaeleza kuwa iliwabidi watafute wataalamu wa masuala mbalimbali ya ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa na kuanza kuelimishwa kuwa uchafu wa mabwawa husababisha samaki kukosa hewa na wakati mwingine kufa.

UHABA WA VIFARANGA

Ambwene anasema mbali na changamoto ya upatikanaji wa chakula chenye ubora walikuwa na tatizo la kupata vifaranga vya samaki bora na kwa wakati.

Anasema baada ya kugundua tatizo hilo walianza kuzalisha vifaranga , lakini katika hatua kwanza hawakupata chochote japo hawakukata tama, waliendelea kutafuta mbegu ya kutotoa vifaranga vya samaki na mpaka awamu ya nne hawakupata chochote jambo ambalo liliwaumiza lakini hawakukubali kushindwa.

“Wenzetu ambao tulikuwa tunashirikiana nao walikata tamaa mimi na mwenzangu tulibaki tukaendelea, tukafanikiwa katika awamu ya tano tukapata vifaranga vitano kati ya mayai 27. Tukarudia tena tukapata 250, vikaongezeka hadi 1, 000 mpaka tukafika 10,000. Tukaanza kukosa wanunuzi,” anasema Ambwene.

MAFANIKIO

Aidha, anataja changamoto walizozipitia kuwa zimewapa fursa ya kujifunza teknolojia za kisasa kwa kuzingatia mazingira wanayoishi na pia wanaweza kujenga mabwawa ya kuhamishika pamoja na kuweka teknolojia ambayo itawezesha samaki kulishwa chakula ama kupata ujumbe mfupi wa kile ambacho kinaendelea katika mabwawa hata kama wapo nje ya nchi.

“Pia tunatengeneza mitambo ya kisasa ya kutotolesha vifaranga vya samaki kutegemea na idadi mteja anayotaka,” anasema Ambwene na kuongeza kuwa mabwawa yao yana uwezo kuchukua vifaranga vya samaki 3,000,0000 kwa mwezi.

Mkurugenzi huyo anasema wanategemea kuanza kutotoa vifaranga 200,000 vya kambale vitakavyouzwa Sh 100 hadi 150 kwa kila mmoja.

Aidha, pamoja na vifaranga wanatarajia kuanza kuuza chakula cha samaki chenye ubora kulingana na uzoefu walioupata.

Anasema umuhimu wa teknolojia katika ufugaji wa samaki ni changamoto kwa watu wengi, wanatumia mifumo duni katika ufugaji huo lakini wao wamejizatiti .

“Tuna uwezo wa kutengeneza kifaa ambacho kinaonyesha usafi wa maji iwapo yamechafuka ama hewa imepungua na kufikisha ujumbe kwa simu ya mfugaji kumweleza abadilishe maji.”

Ofisa Uzalishaji, John Kafyome, anataja ubunifu waliojifunza akisema wameweka mashine kwa ajili ya kuzalisha vifaranga na kwamba mfumo waliouweka katika mabwawa unachuja maji kila yanapochafuka ikilinganishwa na mfumo wa zamani ambao ni wa kubadilisha maji kila wiki.

Anasema unapomwaga maji kila wiki ni gharama kubwa ikilinganishwa na anayemwaga maji baada ya miezi miwili.

ULISHAJI

Kafyome anasema, unapowalisha chakula samaki kinatakiwa kielee juu ya maji ili yasichafuke.

“Chakula kikikaa kwa muda mfupi ndani ya maji kinaoza au kuchachuka na kuwa pombe na kuumiza samaki. Tena wanaweza wakafa. Ni lazima kulishwa mara nyingi kwa siku hasa jamii ya kambale ambao wakiwa na njaa hula wenzake.”

“Ukisababisha waanze kulana bwawani inamaanisha idadi ya samaki inapungua, usitoe nafasi ya kusikia njaa ndiyo maana tunasisitiza walishwe mara kwa mara badala ya kuwapa chakula mara tatu kwa siku,” anasema.

Anasema kwa sababu samaki hao ni wa biashara kadri wanavyolishwa kwa wingi unapunguza muda wa ‘kuendelea kuwatunza bwawana.

Mkurugenzi wa Ufugaji Samaki katika Wizara ya Kilimo na Uvuvi, Dk Charles Mahika, alipowazuru wajasiriamali hao anasema wamefanya ubunifu ambao utasaidia kutoa ajira na kuwataka kuwashirikisha wengine, wanatakiwa kuiga mfano wao ili wajiajiri badala ya kulalamikia kukosa ajira.

Akinukuu taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ya mwaka 2016, anasema mtu mmoja anatakiwa kula kilo 18 za samaki kwa mwaka, lakini Watanzania hula pungufu mtu mmoja anakula kilo 8 kwa mwaka na hilo huchangiwa na uhaba wa samaki.

Aidha, Dk. Mahika anasema kumekuwa na changamoto katika kodi kwenye vifaa vya kilimo cha majini kinachohusisha ufugaji samaki, jambo ambalo ana imani serikali italishughulikia.

Abraham Mndeme, Mkurugenzi wa kampuni ya Big Fish na mwakilishi wa sekta binafsi, akiwa kwenye ziara ya kutembelea kazi hiyo ya ufugaji samaki, anasema uwekezaji huo una changamoto tatu nazo ni mbegu bora ya samaki , chakula cha samaki na utaalamu katika ufugaji wa samaki.

Anasema wahitimu waliomaliza shahada kwenye vyuo vya ufugaji wakiambiwa waende kufuga samaki hawawezi licha ya kwamba wamepatiwa ujuzi huo darasani.

“Ule utaalamu wa kumwezesha aingie kwenye bwawa na kuzalisha unakosekana, hii ni changamoto katika elimu zetu tunatakiwa kuliangalia jambo hili,” anasema

Anaongezea kuwa, ubora wa bidhaa zinazouzwa ili kuzalisha chakula cha samaki pia ni tatizo:” Kuna siku nimeagiza dagaa kilo 100 kati ya hizo kilo 60 ni dagaa nyingine ni mchanga sasa hapo utatengeneza chakula chenye ubora gani?”

Anasema chakula ni muhimu kwani ukiwalisha kambale chakula kikamilifu unapata faida kwa kuwa hawana usumbufu ikilinganishwa na ufugaji wa kuku kwani samaki hao hawana magonjwa mengi wala mahitaji makubwa kama mifugo mingine.”

Habari Kubwa