Ndivyo Mapinduzi Zanzibar yalivyong'arisha wanawake

13Jan 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Ndivyo Mapinduzi Zanzibar yalivyong'arisha wanawake

JANA Watanzania walisherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964. Moja ya malengo ya mapinduzi hayo ni kuleta usawa kwa wanawake na wanaume Wazanzibari.

Dk. Maua Daftari Mshauri wa Rais wa Zanzibar . PICHA: MTANDAO

Ni dhahiri yanapofikisha umri wa nusu karne inadhihirika yalivyosadia kupaza sauti za wanawake hasa katika kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi na sasa wanafurahia matunda ya mapinduzi.

Wanawake wanaona kuwa kwa kiasi kikubwa yamefungua milango kwa kinamama kushika nafasi za juu za uongozi katika wizara, taasisi na idara za serikali. Tena wengine wakivuka mipaka kutekeleza majukumu ya uongozi.

Wanawake viongozi Zanzibar wanasema , mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 uliundwa Umoja wa Wanawake wa Chama cha (ASP) ambacho ndicho kilicholeta ukombozi wa Zanzibar na kilifanya kazi kubwa ya kuishawishi serikali chini ya hayati Abedi Amani Karume, kuwatambuwa wanawake na ushawishi wao wa kisiasa.

WASEMAVYO WANAWAKE

Mwanzilishi wa Umoja wa Wanawake wa Zanzibar na baadaye Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Fatma Karume, anasema alifanya ushawishi mkubwa kuona wanawake na umoja wao wanatambuliwa na kukubalika kwenye jamii.

“Nilifanya kazi kubwa ya ushawishi kuona wanawake wanakubalika na kuingizwa katika nafasi za juu za uongozi kwa bahati nzuri aliyekuwa rais wa Zanzibar alikuwa mume wangu alinisikiliza na kunikubali,’’anasema Fatma Karume.

Fatma mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, anasema katika kipindi cha miaka mitano baada ya Mapinduzi , walipiga hatua kubwa ambapo Umoja wa Wanawake ulikuwa imara huku ukishirikishwa katika majukumu mbalimbali ikiwamo kwenye siasa ambako walikutana na wageni mbali mbali waliozuru nchini humo ambao hufuatana na marais.

Aidha, katika kipindi hicho walifanikiwa kuishawishi serikali kusomesha vijana wa kike katika nafasi mbali mbali kwa ajili ya kuwaandaa kuongoza nchi au kushika madaraka ya uongozi baadaye.

Mama Fatma anawataja wanawake waliopelekwa ng’ambo na waliporudi walishika nafasi mbali mbali za juu akiwemo Dk.Msimu Abrahman ambaye baadaye alishika wadhifa wa Katibu Mkuu wa UWT,pamoja na Dk.Maua Daftari Abeid, ambaye alipata kushika nafasi mbali mbali za Naibu Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’’anasema.

Katibu mkuu mstaafu wa UWT Dk.Msimu Abrahman alichukuwa nafasi ya kukipongeza chama cha ASP pamoja na UWT kwa kufanya kazi kubwa ya kuwasomesha vijana wa wakulima ambao kwa wakati huo hawakuwa na fursa na nafasi za masomo ya nje.

‘’Mimi nilipelekwa Jamhuri ya Watu wa China kwa masomo ya juu fani ya udaktari kwa msaada mkubwa wa Umoja wa Wanawake wa ASP kwa ajili ya kuchukuwa nafasi za uongozi wa nchi,’’anasema.

Dk.Msimu mara baada ya kumaliza masomo yake alirudi nyumbani na kufanya kazi ya udaktari na baadaye kushika nafasi za kisiasa ikiwemo Waziri wa Habari na Utamaduni na Wizara ya Ustawi wa Jamii Wanawake na Watoto katika mwaka 2000.

MAWAZIRI SMZ

Wakati Zanzibar ikiadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa kisultani na wananchi wazalendo kushika hatamu ya kuongoza dola, mafanikio makubwa yamefikiwa kwa wanawake kuwa viongozi.

Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein, anasema amedhamiria kutoa nafasi nyingi zaidi za uongozi kwa wanawake baada ya kuridhishwa na utendaji na ufanisi wa kazi na kwamba katika kipindi cha miaka nane madarakani,amechagua viongozi wanawake kushika nafasi za juu za uongozi wakiwamo mawaziri ambao hawajamuangusha.

Baraza la Mawaziri la Rais Ali Mohamed Shein, lina wanawake watano wanaoongoza wizara ambali mbali nyeti ambao ni Salama Aboud Talib, Waziri wa Maji Nishati na Ardhi wakati Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji ni Dk.Sira Ubwa Mamboya wadhifa wa Waziri wa Biashara Viwanda unashikiliwa na Balozi Amina Salum Ali.

Mawaziri wengine ni Mauldline Castico anayeshikilia Wizara ya Wanawake,Watoto na Vijana wakati Riziki Pembe Juma anaongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Kwa upande wake Waziri Dk.Sira Ubwa Mamboya, anasema Mapinduzi ndiyo yaliyoleta mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi kutoka kutawaliwa hadi kuwa huru katika nchi yao.

Kwa mfano anasema amepata nafasi ya kusoma elimu ya juu nchini Urusi mara baada ya Zanzibar kufanya mapinduzi na kuongeza”Tunaposema Mapinduzi daima maana yake tunataka yadumu kwa ajili ya kuleta mabadiliko zaidi ya kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wetu.”

Nafasi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashikiliwa na Fatma Mohamed Said ambaye anakiri kwamba mapinduzi ya mwaka 1964 ndiyo yaliyomfikisha kushika wadhifa huo.

‘’Nimeshika wadhifa huu kwa ridhaa ya wananchi wa Zanzibar chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ilinisomesha….bila mapinduzi nisingeweza kushika wadhifa huo kwa sababu nchi ilikuwa katika utawala wa kisultani wenye kufuata misingi ya kiukoo’’anaeleza.

Raya Mselem ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi chombo cha kutunga sheria anasema wanawake sasa wanayo fursa kubwa ya kushika nafasi za uongozi kwa sababu nchi ipo chini ya mikono ya Wazanzibari wenyewe.

‘’Nimeteuliwa kushika wadhifa huu mkubwa wa kuwa msaidizi mkuu wa chombo cha kutunga sheria cha Baraza la Wawakilishi ambapo naahidi kamwe sitawaangusha wanawake wenzangu,’’anaeleza.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la CCM, Khadija Jabir ,anasema Mapinduzi ya mwaka 1964 ndiyo yaliyoleta mabadiliko makubwa kiasi cha kuwezesha wanawake kutambuliwa mbele ya jamii na serikali pamoja na taifa.

Anasema kabla ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, hakuna mawazo ya kutokuwapo na mawazo ya kuanzisha jumuiya ya wanawake katika utawala wa Kisultani.

‘’Chama cha ASP mara baada ya kuanzishwa mwaka 1957 kilianzisha jumuiya ya wanawake kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mapambano ya kudai uhuru ingawa mikakati hiyo ilikuwa ikifanywa kwa siri.’’anasema Khadija.

Hata hivyo Khadija anaona kuwa wanawake walianza kupata mwamko wa kisiasa na kujiunga katika jumuiya iliyoanzishwa na ASP mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 na kwamba ndiyo ngazi ya kuwapandisha wanawake juu kisiasa, kiuchumi, kitaaluma na kimaendeleo.

Anasema kuanzia hapo ndipo baadhi ya wanawake wasomi waliomaliza kidato cha nne na sita walipotafutiwa nafasi za masomo elimu ya juu kwa ajili ya kuchukuwa nafasi za uongozi.

‘’Viongozi wengi wanasiasa wanawake wastaafu walikuwa wanachama wetu ambao tuliwatafutia nafasi za masomo nje ya nchi katika nchi rafiki.’’ alisema.

Alizitaja nchi rafiki zilizokubali kutoa nafasi za masomo ya elimu ya juu kwa wanawake kutoka jumuiya ya ASP ni Urusi,Ujerumani Mashariki na China.

Jumuiya ya wanawake ya UWT imeweka bayana mikakati yake na kusema itahakikisha wanawake wanapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ili kuondokana na pengo kubwa la kuachwa nyuma na wanaume.

Habari Kubwa