Ndivyo miji inavyotisha kiudhalilishaji kinamama

10May 2022
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Ndivyo miji inavyotisha kiudhalilishaji kinamama

RIPOTI ya ukuaji miji inayotolewa na Benki ya Dunia inatoa angalizo kuwa miaka 25 ijayo, idadi ya watu wanaoishi mijini na majiji barani Afrika itaongezeka maradufu. Ni kutokana na watu wengi kukimbia kuishi vijijini.

Vurugu za usafiri mijini zinawaathiri zaidi wanawake ambao wakati mwingine wanalazimika kupitia madirishani. PICHA: SABATO KASIKA

Aidha, kufikia mwaka 2040, Tanzania kama yalivyo mataifa mengi ya Afrika raia wake wengi watakuwa wanaishi mijini na majijini na sababu mbalimbali kuelezea hali hiyo zinatolewa mfano, mabadiliko ya tabianchi, ukame, vimbunga yote yakizorotesha kilimo. Pia, mijini kuna matumaini ya kupata kazi, elimu na maisha bora na kwa nchi nyingine migogoro ya vurugu za kisiasa zinahusishwa.

Changamoto kubwa inayoikabili Afrika ni kukua kwa miji kunakoambatana na idadi kubwa ya watu, yote hayo wanawaumiza zaidi wanawake na watoto kwa kuwa masuala ya usawa wa kijinsia na maendeleo ya miji kwenye kutoa huduma za kijamii hayajawajali wanawake na watoto.

MIJI ISIYOWAJALI

Wakati wengi wanahamia mijini na majijini maisha salama na bora kwa wanawake na watoto kwenye maeneo hayo ni kitendawili kigumu.

Licha ya kuujua ukweli kuwa upangaji na utoaji wa huduma za kijamii mijini na vijijini hauna mrengo wa kijinsia kwa miongo kadhaa, mambo yamekwenda tofauti na uwekezaji wa kuboresha huduma unabakia kuwa usio wa haki kwa wanawake na watoto ambao mara nyingi wameendelea kuumizwa.

UNYANYASAJI KIUSAFIRI

Mathalani Dar es Salaam, kubanana kwenye usafiri wa umma daladala na mabasi yaendayo haraka ni jambo linaloweza kusemwa halina tiba.

Kujazana na kubanana kupindukia kunasababisha kudhalilisha wanawake na wasichana kunakofanywa na abiria wanaume.

“Kwenye mwendokasi watu wanabanana kupindukia, kadhalika ndani ya daladala hasa wakati wa matatizo ya usafiri.

Tunajiuliza kwanini sheria hazifuatwi? Anasema Grace Mpole, mfanyabiashara wa rasta Kariakoo- Dar es Salaam.

Malalamiko ya abiria na raia ni mengi na ukiyatazama tatizo linaweza kutokana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kutokusimamia sheria kikamilifu anasema Hassan Mchanjama, Mwenyekiti na mwasisi wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania  (CHAKUA).

Anatoa maelezo hayo, anapoulizwa na Nipashe kuhusu kuangalia eneo la abiria kubanana na wanawake kudhalilishwa ndani ya vyombo vya usafirishaji wa umma ambalo miji inaelekea kushindwa kulitatua.

“Kwa sheria za usafirishaji mhusika anapokwenda LATRA, anaulizwa kuhusu ruti anayosajili kama ni mijini au mkoa upi kwa mabasi ya masafa. Kadhalika idadi ya abiria ni swali analoulizwa anataja ana apewa leseni za usafirishaji akielezwa kuhusu ruti na nauli halali lakini kwenye kuangalia na kusimamia idadi ya abiria LATRA hawaonekani kufuatilia, hata polisi nao hawalitazami hilo,” anasema Mchanjama.

Anawataka LATRA kufuatilia kama wanavyofanya Mamlaka ya Usimamizi wa Maji na Nishati (EWURA) kusimamia gharama za mafuta, bei halali vituoni, kupambana na uchakachaji, vivyo hivyo LATRA nao wawajibike kulinda masuala kama idadi ya abiria, ruti na nauli halali, wasidhani pengine ni jukumu la polisi.

“Tunapata malalamiko ya unyanyasaji na udhalilishaji wa abiria kwenye mabasi ya mwendo kasi kila siku. Tunadhani ni wakati wa kuangalia na kusimamia sheria na kupunguza malalamiko ya abiria na kudhibiti unyanyasaji,” anashuri Mchanjama.

UDHALILISHAJI KILA KONA

Mchanjamana anataja kuwapo malalamiko ya kubanana na kudhalilisha wanawake kwenye meli, vivuko, treni mathalani ya Dar es Salaam hadi Mpanda.

Mwenyekiti wa CHAKUA, anasema malalamiko mengine ni wanawake kuibiwa, kukaa muda mrefu vituoni wakati wanaume wanapandia madirishani na kujaza nafasi wakiwaacha wanawake, watoto na wanafunzi kukesha muda mrefu vituoni.

‘KULIPISHWA CHOO’

Ukosefu wa usawa wa kijinsia ambalo ni tatizo la kihistoria lipo kwenye vyoo, ambayo ni huduma muhimu lakini haitoshi wala haijasambaa kufikia watu wengi na choo kinatumiwa kwa kununua huduma hiyo. Katika dunia yenye usawa huduma ya choo inatakuwa kupatikana bure.

Wanawake wanaweza kuwa wahitaji wakubwa wa huduma hiyo kutokana na maumbile, lakini miji mingi haijalitambua hilo.

Wakati kinababa wanaweza kumaliza haja zao kwenye ukuta wa uzio, chini ya mti, ndani ya mitaro ya barabara au kwenye nguzo za TANESCO wanawake hawana pakukimbilia.

Ni ukweli kuwa kukosekana vyoo vya kutosha mijini na vinavyotoa huduma bure ni changamoto kubwa zaidi kwa kinamama na wasichana.

Wanawake wanaotembea na watoto wagonjwa wanaohitaji kujisaidia, inapotokea yuko Mbezi stendi ya daladala ni wazi wengi hataweza kumpeleka mtoto anayesumbuliwa na tumbo chooni kutokana na gharama kubwa za Shilingi 500 ili kuingia.

Ili kuondoa tatizo hilo Halmashauri za Miji zijenge vyoo vya watoto wakiwamo wanafunzi wanaokuwa vituoni ambao wazazi wao wanawapa Shilingi 1,000 pengine kwa Dar es Salaam ili kulipa nauli ya 250 kwenda na kurudi na 500 kununua chochote cha kula.

“Haiwezekani kuingia chooni hata kama unabanwa na haja ukiwa kwenye kituo cha mabasi hatuna Shilingi 300 au 500 za kulipa huduma ya choo “ anasema Jessey Tesha mwanafunzi wa Sekondari ya Kibweheri anayeishi Mbezi Lousi.

Wanafunzi wanataka huduma bure za choo kwa sababu dharura za kutumia choo zinaweza kutokea wakati wote hata kama mtumiaji hana hela, akibanwa na tumbo, kwa mabinti wakipata changamoto za hedhi yote hayo yanahitaji suala hilo kuangaliwa upya.

Upangaji wa miji na utoaji wa huduma zikiwamo za usafiri ulikosa usawa wa kijinsia kihistoria tangu wakati wa ukoloni na sasa umekuwa ukichangiwa na sera za uliberali hasa mijini ambako kila kitu kinategemea nguvu ya soko na huduma karibu zote zinauzwa.

Mfano huduma zilizoanzishwa kikoloni ni za treni ya abiria ikiwa na mabehewa ya wasafiri wenye fedha nyingi wa daraja la kwanza, la pili na la tatu hubeba mafukara wanaobanana muda wote.

Hata leo miaka 62 ya Uhuru hakujawa na mabadiliko ya huduma ya mabehewa mfumo ni ule ule hivyo ni wakati kufikiria kuwa na mabehewa ya wanawake na watoto kwenye treni hizo.

Bidhaa (huduma) za umma ni adimu katika miji na majiji ni duni mifano wanawake wengi wanaishi katika makazi yasiyo rasmi, wanafanya kazi maeneo hatarishi, hasa katika sekta isiyo rasmi lakini wanaporwa, kujeruhiwa kila siku kutokana na kukosekana ulinzi na usalama wa kijamii kwenye mitaa mingi mijini.

Wanaoathirika ni wale wanaoishi kwenye maeneo hatarishi kama mabondeni, vitongoji vya wahalifu na mitaa yenye wakazi maskini wakiwamo vijana wanaotumia mihadarati, pombe za kienyeji na dawa za kulevya zinazoandaliwa kwa kutumia mchanganyiko wanaoifahamu wenyewe.

Habari Kubwa