Ndivyo Tanzania ilivyobahatika kuviepuka vimbunga na tufani

04May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ndivyo Tanzania ilivyobahatika kuviepuka vimbunga na tufani

LICHA ya kimbunga cha kitropiki cha jobo kuelezwa kuwa kingepiga pwani ya Tanzania na kusababisha maafa ukanda wa pwani, taarifa za watabiri wa hali ya hewa kimataifa zinasema ni nadra kutokea tufani hizo kwa vile Tanzania si mkondo wa vimbunga.

Athari za kimbunga katika baadhi ya miji duniani. PICHA : MTANDAO.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), jobo ingekumba maeneo ya Zanzibar, Mafia, Dar es Salaam na mikoa ya Kusini ikiwamo Lindi na Mtwara.

Kuhusu kimbunga hicho kutofika nchini, inaelezwa kuwa kinachoiepusha Tanzania na tufani hizo za baharini ni kuwa karibu na Ikweta ambao ni mstari wa ‘kufikirika’ unaoitenganisha dunia katika vipande viwili kizio cha Kaskazini na cha Kusini.

Kitaalamu kuwa karibu na Ikweta huleta faida kadhaa kama mvua nyingi na misimu miwili ya masika na mvua, jua la kutosha na pia kutofikiwa na vimbunga.

Kwa mujibu wa mtandao wa televisheni ya CNN ya Marekani, ni nadra kutokea vimbunga Tanzania na kwamba si taifa la dhoruba wala kimbunga kutokana na ukaribu wake ni mstari wa Ikweta ambako nguvu za uvutano za ‘ Coriolis force’ zinazosababisha kuanzisha upepo mkali na dhoruba ili kuchochea vimbunga kuzunguka na kupata kasi kubwa ni dhaifa au hazina nguvu eneo hilo.

CNN inasema taarifa zilizopo kuhusu historia ya vimbunga vilivyoikumba Tanzania zinaeleza kuwa vilitokea mara mbili tangu karne ya 19 vikionyesha kuwa kulikuwa na kimbunga cha Zanzibar cha mwaka 1872-"Zanzibar Cyclone" of 1872 na cha Lindi mwaka 1952 kikiitwa Cyclone Lindi of 1952.

“Vimbunga hivyo viliikumba Tanzania miaka 80 kuanzia 1872 hadi 1952. Vikitokea Aprili 14, 1872 na kingine kikizuka Aprili 15, mwaka 1952.”

Kwa mujibu wa CNN kuanzia wakati huo hadi leo takribani miaka 70 iliyopita hakuna maafa ya vimbunga tena.

Hata hivyo, kutokana na uelekeo wa kimbunga kutokea baada ya miaka 80 huenda jobo ulikuwa mwendelezo wa tufani zinazoikumba pwani ya Tanzania kila baada ya miaka 80.

Halikadhalika taarifa hiyo inasema vimbunga hivyo vya kihistoria vilivyosababisha maafa makubwa na vifo vya watu wengi Lindi na Zanzibar, havikufika Dar es Salaam lakini mwaka huu jiji hilo lenye takribani watu milioni sita na shughuli nyingi za kiuwekezaji na miundombinu ya kisasa lilikuwa kwenye hatihati ya kuumiziwa na jobo.

Kutokana na utabiri huo, Lindi na Zanzibar yanabakia kuwa maeneo au mikondo ya vimbunga ambavyo hutokea mwezi Aprili ambao ni kilele cha mvua za masika nchini.

Kuanzia mwaka 2019, vimbunga vya kitropikia ‘idai na Kenneth’ viliipiga Msumbiji na kusababisha maafa makubwa na maelfu ya watu kupoteza maisha huku uwekezaji ukiharibiwa kwa kiasi kikubwa tena kupindukia.

Kimbunga jobo ambacho kitaalamu huitwa ‘tropical cyclone’ kinaelezwa kuwa kinapatikana karibu na visiwa vya Madagascar kusini mwa Bahari ya Hindi.

Kimbunga ambacho ni upepo mkali mno wenye kasi na nguvu kubwa mara nyingi ukianzia baharini kuelekea pwani na kuelekea nchi kavu, kinaambatana na mvua kubwa. Wakati mwingine kasi ya upepo inapokuwa kubwa kupindukia na kimbunga hicho huitwa dhoruba.

Jobo ni kimbunga cha kitropiki kinachozalisha upepo mkali na mvua nyingi na kinahusishwa na tropiki au joto kwa sababu huanzia kwenye joto la takribani nyuzi 22 na kwa mwaka huu kikielezwa kuwa kilianzia kwenye nyuzi joto 29 na kwamba hali za kimazingira zingekizuia kisiendelee kuwa na nguvu na athari kubwa zaidi kwa kufika nchi kavu hasa mikoa ya ukanda wa pwani.

Hofu ya kukumbwa na kimbunga hicho kilichotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilikuwa kubwa zaidi kwa wakazi wa mikoa ya ukanda wa pwani ya kusini inayohusika mikoa ya Lindi na Mtwara. Aidha, kilitarajiwa kufika Zanzibar, Bagamoyo pamoja na Dar es Salaam.

Hata hivyo, hofu ilitoweka baada ya kimbunga jobo kiichotarajiwa kilichokuwa kiwasili nchini Jumapili Aprili 25, kutangazwa na TMA kuwa kilitoweka na hakipo tena kutokana na kupungua nguvu na kufifia wakati kilipowasili katika ukanda mkavu wa pwani ya Tanzania.

ATHARI ZA VIMBUNGA

Msumbiji ni jirani na Tanzania na imekuwa na majanga mengi ya vimbunga yakiwamo matukio 46 ya vimbunga na mafuriko katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Majimbo yaliyoathirika ni pamoja na Cabo Delgado, Nampula, Manica, Zambezi na Sofala.

Kwa mujibu wa Taarifa za Umoja wa Mataifa (UN), idadi ya watu waliokufa kutokana na kimbunga idai nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi ilifikia zaidi ya 615.

Taarifa zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la uratibu wa misaada ya kiutu (OCHA) mwaka 2019 zilisema watu 417 walikufa nchini Msumbiji,139 Zimbabwe na 59 Malawi hata hivyo serikali ya Msumbiji ilisema pengine watu 1,000 walihofiwa kufa.

Habari Kubwa