Ndizo athari za kuwatusi watoto wenu, mjichunge

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ndizo athari za kuwatusi watoto wenu, mjichunge

NAAMINI utakuwa umesikia au kuona wazazi au walezi wanapokwaruzana na watoto wao na kufikia hatua ya kushikwa na jazba, hamaki na hasira na kuanza kuporomosha maneno makali yenye matusi, kebehi, dhihaka na lawama kwa watoto.

Si hivyo tu hata wazazi na walezi wengine hufikia hatua ya kuwalinganisha watoto wao na wanyama au kitu chochote kibaya na kisichofaa kwa kukisikia au kutazamwa kama njia ya kukanya, kukaripia, kuadhibu ama kufundisha.

Wengine huwaita, wewe mbwa au wee nyani njoo hapa kauli nyingine za majuto kama “najuta kukuzaa” hili ni kutokana na vitendo na tabia za mtoto.

Maneno ya namna hii yanaleta tafakari kubwa hasa pale unapoanza kujiuliza kuwa mwanamke huyu ambaye kwa miezi tisa alimbeba mtoto ilhali akivumilia kero, karaha na kadhia za ujauzito na machungu ya leba iweje ageuke na kumchukia mtoto huyo kumwita mbwa, kima ama kujiapiza na kujuta kumzaa.

Na si majina ya wanyama kama mbwa, ng’ombe, kenge au kima bali wazazi wengine huwatolea matusi mazito ya nguoni watoto wao kama njia ya kuwakanya wanapokosea bila kujali udogo wala ukubwa wa kosa alilolifanya mtoto.

Iko wazi kuwa watoto wanapozaliwa hutofautiana sana baina ya mmoja na mwingine katika malezi na makuzi yao kutokana na sababu tofauti ikiwamo asili ya wazazi wake,mazingira anayolelewa na kukulia,hali ya kipato cha wazazi wake pia namna ambavyo wazazi wake walikuzwa wakati wa utoto huchangia kuleta athari katika malezi na makuzi hayo.

Kuna baadhi ya wazazi ambao huhamisha kila kitu kwa watoto wao kutoka kwenye mtindo wa malezi yake wakati huo akiwa chini ya himaya ya wazazi wake hata kufikia hatua ya kupigia chapuo aina yake hiyo ya malezi kwamba “mimi wazazi wangu hawakunilea hivyo” akiwa analinganisha mienendo,tabia,na hulka za mtoto au watoto wake na wakati akiangalia ukuaji aliopitia.

Hapo kinachotokea kama wazazi wake walikuwa wakimpa zile adhabu kali anapokosea kama kuchapwa viboko,kutukanwa, kukaripiwa hadharani, kufungiwa ndani ama kushurutishwa kwa njia yeyote ile basi na yeye atazihamisha kama zilivyo kwenda kwa watoto wake.

Jiulize kwa umakini kidogo, kama wazazi wako walikulea kwa yale malezi ya bata yaani mtoto mbele mzazi nyuma, mtoto anaamua mzazi anatekeleza, au walikulea ya malezi ya kidikteta, yaani ulikuwa ukimuona baba akirudi nyumbani unajificha chumbani au baba akinywa pombe wote hamlali ndani,atatukana kuanzia mama mpaka dada wa kazi pamoja na majirani na wewe utahamisha kama ilivyo na kulea watoto wako hivyo hivyo?

Si, kitu kibaya kuhamisha malezi ya jinsi ulivyolelewa kutoka kwa wazazi wako na kuyapeleka kwa watoto wako kwa kuwa hakuna mzazi ambaye alikwenda chuo au mafunzo ya kulea watoto kabla ya kuwapata ila kinachotokea ni kuchukua matamanio yake kwa watoto wake aliowapata, namna yeye alivyolelewa na wazazi wake na mahitaji ya sasa ya malezi ndipo hutengeneza mjumuiko wa taratibu, sheria, kanuni na miongozo kwa watoto wako.

Sasa linapokuja suala la wazazi wenye tabia za kuwatusi watoto wao kwa kuwaita majina yasiyofaa, yanayoumiza, yanayokebehi na kuudhi hapa wazazi wenyewe hudhani kwamba maneno hayawezi kuleta madhara kwa mtoto kulinganisha na kumpa adhabu ya viboko, fimbo, mijeledi hivyo wengi wao huamini kutukana au kumwita mtoto kwa jina lenye kuudhi au kukebehi kutamfanya mtoto kujisikia vibaya na kubadilika kufanya vitu vilivyokuwa vizuri.

WANAPOKOSEA

Dhana hii ya kutusi ina upotofu mkubwa kwa sababu wazazi huchukulia namna ambavyo wao wanahisi maumivu pale wanapoitwa majina hayo ya kuudhi na kuumiza ndivyo hivyo hivyo hata watoto wanavyohisi. Ilhali kwa watoto wao ni tofauti namna ambavyo wanatafsiri kwa sababu kauli hizi huchafua roho za watoto, kuwafanya kuwa duni, huchochea chuki na hofu baina yao na wazazi.

Kingine kikubwa kibaya ni kwamba jambo lolote baya huwa na nguvu zaidi kwenye akili ya mtu aidha iwe kwa mtoto mdogo au mtu mzima kuliko kitu au jambo zuri ndiyo maana Waswahili husema baya moja linaweza kufuta mema 100 kwa wakati mmoja hili huchangiwa zaidi na tabia ya ubongo ilivyo.

Akili inakua makini zaidi pale unapopata taarifa hatarishi na mbaya kuliko taarifa nzuri au zenye kusifia kwa sababu ubongo unapopata taarifa hatarishi au mbaya unalazimika kutafuta suluhu ya taarifa husika ili ifanye maamuzi.

Pale ambapo mtoto mara kwa mara anapata taarifa mbaya zenye matusi,vitisho,kebehi,kumdhalilisha kama njia ya kumfundisha au kumkanya matarajio ya mzazi ni mtoto kubadilika na kuwa mwenendo mzuri basi unapaswa kujua kwamba unaufanya ubongo wake kuwa katika sintofahamu ya kujua aamue kipi na kwa wakati gani kwa sababu akilini kunakuwa kumejaa matukano ya wee kenge, tumbili au mbwa.

Kibaya zaidi haya ya makovu ya kihisia hayaishii utotoni tu bali kadri watoto wanavyokuwa na wanakua nayo na wengine hayafutiki mpaka uzeeni, hili si utani hata kidogo na tafiti zinaonyesha kwamba watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 60 walio wengi wanapoelezea simulizi za maisha yao ya mapito ya kimaisha mara nyingi hukumbuka maumivu waliyoyapata kwenye vipindi tofauti vya maisha yao bila kusahau manyanyaso waliyoyapitia utotoni.

Kwa mantiki haishangazi kuona mzazi mwenye kutumia kauli zenye maneno makali kwa watoto zikazalisha watoto wenye haiba, tabia, matendo na mienendo tofauti kwenye jamii kinyume na matarajio ya wazazi wenyewe.

MAKUNDI MABAYA

Wala hupaswi kushtuka, hivi unadhani makundi ya kihuni kama ya kina komando yoso, wakorea weusi ,panya road yanazalishajwe, naweza kusema ni sisi wenyewe tangu wakiwa watoto wadogo ila tunachokiona ni matokeo ya uzalishaji wetu wenyewe huku tukijiuliza na kutafuta chanzo cha yote tunayoyaona.

Watoto si tu kwamba huingia kwenye makundi yasiyofaa bali ni kwa namna gani wazazi huzalisha watoto wasiojiamini, wasioweza kujiongoza au kujaribu vitu tofauti hali ambazo hudumu akilini mwao mtoto kwa muda mrefu mpaka kuja kufikia hatua ya mtoto kubadilika.

Kitaalamu kutokana na malezi na makuzi ya mtoto anayopitia athari wanazozipata huishi nazo muda mrefu kiasi kwamba ukubwani zinaweza kuleta madhara kwa mtoto mwenyewe lakini kibaya zaidi watu wengine huathirika japo hawakustahili kupata malipo ya athari hizo.

ATHARI UKUBWANI

Hivi unayoyafanya kwa mtoto wako unajua na yeye atakuwa mtu mzima na kujitegemea? Je unamfikiria bosi atakayemuajiri kwa sababu atakuwa na tabia tofauti na kumwachisha kazi, ulilifikiria hilo? Mume atakayemuoa binti yako au unafikiria kuwa binti yako atakuja kuwa mke wa mtu utajisikiaje wanandoa wakatengana halafu wajukuu wakalelewa na wazazi tofauti?

Kama yote haya unayafikiria kwanini unaendelea na kulea kwa mtindo usiofaa katika jamii ambao mwanao anakuwa na tabia tofauti akiwa nyumbani, kanisani au madarasani anakuwa na sura zisiofanana?
Wazazi, walezi tafakarini.