Ndoa ya kaburi ilivyoacha alama kwa wanawake Serengeti

11Jun 2021
Grace Mwakalinga
MARA
Nipashe
Ndoa ya kaburi ilivyoacha alama kwa wanawake Serengeti

NDOA ya kaburi ni moja wapo ya mila na desturi inayowaumiza wanawake wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, ambapo mwanamke hulazimika kuolewa ili kukidhi matakwa ya kabila la Kikurya.

Chausiku Juma ni miongoni mwa wanawake waliothirika na ndoa za kaburi, anasema akiwa na umri wa miaka 14 baada ya wazazi wake kufariki huku akibeba jukumu la kuwatunza wadogo zake wawili alishawishiwa kuolewa.

Anasema wakati huo akiishi na babu na bibi yake alikuja mzee mmoja ambaye hakuwa tayari kumtaja jina akiomba mwanane amuoe binti huyo huku akiahidi kutoa ng’ombe wengi ili akubali.

Chausiku anasema kutokana na ugumu wa maisha alishawishika kukubali kuolewa na mwanaume ambaye alionyeshwa siku hiyo kwa ng’ombe 31.

Baada ya muda kupita Chausiku alipata watoto watatu ambao alizaa na mwanaume aliyetambulishwa, kadri siku zilivyoenda alianza kuona mambo tofauti mwanaume aliyemzalisha alikuwa hamuhudumii wala kukubali watoto kutumia jina lake.

Alijitokeza wifi yake na kumweleza ukweli kwamba mwanaume aliyezaa nae sio mume halisi badala yake mumewe ni kaburi la kijana ambaye alifariki miaka kadhaa iliyopita.

“Baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wifi yangu, nilisikitika sana na kukusudia kuondoka katika familia hiyo lakini  kutokana na ugumu wa maisha niliendelea kuishi hapo kwani kwa mujibu wa mila na desturi za ndoa za makaburi nikiondoka lazima nirudishe ng’ombe wote na mimi sina uwezo,” alisema Chausiku.

Pili Mkwabe (15) ambaye pia ni mhanga wa ndoa za makaburi anasema ugumu wa maisha ulichochea yeye kuolewa kwenye ndoa ya kaburi, anasema baada ya mama yake kufariki alibaki na baba ambaye ambaye baada ya kumaliza darasa la saba alimlazimisha kuolewa ili apate mahari.

Anasema  baba yake alichangia yeye kuolewa kwenye familia ambayo hakuijua vizuri ili mradi tu apate mahari na kusomesha wadogo zake.

Hakujua kama hakuna mwanaume, alikutana na shemeji yake ambaye  walimdanganya kwamba ndie mumewe, alipozaa mtoto  wa kwanza ndipo aliambiwa ukweli.

“Nilipokuja kuamini kwamba ninaeishi nae sio mume wangu ni baada ya kugoma watoto wasitumia jina lake  na vilevile  alikuwa hatunzi familia na badala yake niliambiwa watoto watatumia jina na marehemu ambaye ndio walisema ni mume wangu,”alisema Pili.

Kutokana na madhila hayo Pili alijifunza mambo kwani kwa sasa anaishi peke yake aliondoka kwenye familia hiyo na anaendelea kufanya vibarua  vya shamba ili kupata fedha ya kujikimu kimaisha.

Anasema isingekuwa ndoa ya kaburi angekuwa mfanyabiashara mkubwa sasa na kwamba anamkumbuka sana mama ambaye anaamini angekuwepo asingekubali kuolewa kwenye ndoa hiyo.

Mchungaji kiongozi Kanisa la Angalican wilayani Serengeti,  Canoni Masatu anasema Wilaya hiyo ni  miongoni mwa maeneo yanatajwa kukithiri kwa vitendo vya ukeketaji, mfumo dume na uendelezwaji wa mila na desturi zinazomkandamiza  mwanamke.

Kutokana na tatizo hilo waliamua kuanzisha kituo cha kuhudumia watoto ambao wanawahudumia kimwili na kiroho pamoja na kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia.

Anasema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho ni miaka mitano sasa wameona mabadiliko  baada ya kuifikia jamii kwa kiwango kikubwa kutoa elimu  ya athari zitokanazo na kuendeleza mila na desturi potofu.

Anasema elimu hiyo imetolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo, serikali na vyombo vya habari na Jeshi la Polisi.

“Kabila la Kikurya na kingoleme wanaamini kwamba kuzaa mtoto wa kike ni utajiri  wa kupata mali hivyo hulazimika kuwazoesha mabinti zao ili kupata mali hizo, kanisa tumekuwa na utaratibu wa kuhubiri wananchi kuacha  tabia hizo za kuendeleza mila na desturi potofu hasa za ndoa za makaburi ambazo ni  kinyume na mpango wa Mungu,” alisema Masatu.

Aliongeza “wanatamani watoto wa kike waendelee kusoma ili kufikia malengo yao anasema ndoa za makaburi sio halali ni ndoa zinazofanywa kwa matakwa ya watu wa jamii husika”.

Mwenyekiti wa Mila na Desturi, Wilaya ya Serengeti, Samwel Kivokola, anasema ndoa za makaburi ziko tangu enzi  na kwamba tangu azaliwe mwaka 1938 alizikuta.

Anasema ndoa hizo ziliheshimika  katika kabila la Wakurya na hakuna yeyote aliyekaidi kwa wakati huo kwani walifanya hivyo ili kudumisha mila na desturi lakini pia kutopoteza undugu au ukoo  miongoni mwa jamii.

Anasema kulingana na elimu inayotolewa na Serikali na wadau mbalimbali juu ya athari za kuendeleza mila hiyo ya ndoa za makaburi sasa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha jamii ya Serengeti inapingana na  utaratibu huo.

Anasema kwa sasa yeye mabinti zake wako shule wanasoma na kamwe hawezi kuwaruhusu watoto wake waingie kwenye utaribu huo wa ndoa za makaburi, wanaendelea kutoa elimu kwa wengine kuachana na hali hiyo.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Serengeti, Maria Peter,  anasema  vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani vipigo kwa wanawake viko kwa kiasi kikubwa.

Anasema  matukio ya vipigo  yanayoripotiwa kwa siku  huanzia tano hadi 10 zaidi na kwamba idadi hiyo inazidi kuongezeka siku hadi siku.

Kuhusu ndoa za makaburi anasema wamekuwa wakiwasaidia wanawake wengi walioathirika ambapo wengi wao hufika ofisini kwake wakilalamika kutopata huduma kutoka kwa familia ya alikoolewa.

Anasema jukumu analolifanya ni kuwaaelimisha na kuwashauri kuachana na hizo ndoa na badala yake wasonge mbele kutafuta maisha ili wawalee watoto badala ya kuishia kulalamika na kuwaharibia watoto ndoto zao za baadae.

Habari Kubwa