Nelson Mandela mtu wa kipekee anayezidi kutukuka

21Jul 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Nelson Mandela mtu wa kipekee anayezidi kutukuka
  • *UN huadhimisha Mandela Day kumuenzi

DESEMBA 5, 2013 ni siku aliyofariki dunia Nelson Mandela, Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini.

Nelson Mandela siku yake inaadhimishwa kila mwaka Julai 18. PICHA MTANDAO.

Ni kiongozi wa kipekee na wa aina yake, hivyo Umoja wa Mataifa (UN) unapomtafakari shujaa huyo, unaitangaza Julai 18, kila mwaka kuwa Siku ya Mandela.

Siku ya Kimataifa ya Mandela imeanzishwa na UN ili kumkumbuka, kumuenzi na kuutafakari kazi zake, utu wake, usawa aliusimamia na mpigania haki za binadamu namba moja.

Julai 18, 1918 ndiyo siku aliyozaliwa Mandela na imepitishwa rasmi na UN mwaka 2009 na maadhimisho ya kwanza yakafanyika mwaka 2010.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, katika ujumbe wake kwa siku hiyo mwaka 2010, anasisitiza dunia kumkumbuka na kumuenzi Mandela kwa kutafakari utu wake, usawa pamoja na haki za binadamu alizozitetea na kuzisimamia.

Anamsifu kuwa alikuwa mstari wa mbele, kupinga ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kwamba kila binadamu akitumia uwezo wake anaweza kuifanya dunia mahala bora pa kuishi kama kiongozi huyo alivyofanya.

"Kila mtu ana uwezo na jukumu la kuibadili dunia kuwa bora zaidi. Siku ya Mandela ni fursa kwa kila mtu kuchukua hatua na kuhimiza mabadiliko. Kila mwaka, katika siku hii ya kuzaliwa ya Nelson Mandela, tunamshukuru mtu huyu wa ajabu ambaye alijumuisha matakwa ya juu zaidi ya UN na dunia.”

“Tumeshuhudia sasa jamii zikizidi kuparaganyika, lugha za matusi na uongo zimeongezeka, habari zinazofifisha ukweli, kuhoji sayansi na kudhoofisha taasisi za kidemokrasia,” anasema Gutteres.

Anasema janga linaloendelea la COVID-19 linachangia kurudisha nyuma maendeleo na vita dhidi ya umasikini, pia katika kipindi cha matatizo waliopo kwenye makundi yenye kuhitaji msaada, wanaoteseka zaidi, na kulaumiwa ingawa hawana hatia kwa yaliyotokea.

“Janga hilo la corona limeonyesha umuhimu wa mshikamano na umoja, maadili yaliyopigiwa chepuo na Nelson Mandela katika kipindi cha uhai wake kwa kupigania haki na usawa.”

“Hakuna aliyesalama mpaka wote tuwe na usalama. Na kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya.” anasema Guterres katika ujumbe wake wa siku ya Mandela, mwaka huu.

Katibu Mkuu wa UN, anasema watu wote wanatakiwa kuhamasika na ujumbe wa ‘Madiba’ kwamba kila mmoja anaweza kuleta mabadiliko katika kutangaza amani, haki za binadamu, maelewano na utu kwa watu wote.

“Katika kuyaenzi maisha ya Madiba, tuheshimu wito wake na kuchukua hatua na kutiwa nguvu na urithi aliotuachia.”

MANDELA NI NANI

Nelson Mandela ndiye Rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini, baada ya kutumikia kifungo cha miaka 27 gerezani katika kisiwa cha Robben.

Pamoja na wapigania uhuru wengine, aliachiwa huru mwaka 1990 baada ya kusota kwa miongo mitatu.

Mandela au Madiba alihimiza mshikamo na kukomesha ubaguzi wa rangi, jambo ambalo sasa lipo hatarini kwani mshikamo wa kijamii duniani unatishiwa na mgawanyiko.

Wakati Nelson Mandela alipokuwa kijana, Wazungu na Waafrika walikuwa hawaishi pamoja chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi uliojulikana kama ‘apartheid’.

Weupe, ambao walikuwa idadi ndogo ya raia, ndiyo walioidhibiti nchi na njia zote za uchumi.

Ilikuwa ni marufuku kwa weusi kwenda shuleni, hospitali na hata maeneo ya kubarizi kama katika fukwe za bahari sawa na watu weupe.

Hali ilikuwa imeimarika zaidi katika shule na hospitali za watu weupe, wakati Waafrika walinyimwa haki msingi, kama kushiriki katika uchaguzi mkuu, lakini Nelson Mandela aliamini kwamba kila mtu anastahili kuchukuliwa kwa usawa.

Mandela alijiunga na Chama cha African National Congress (ANC) na baadaye kuongoza tawi la vijana la chama hicho, akishiriki maandamano kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi.

DUNIA ILIMTOA GEREZANI

Wakati Mandela akiwa gerezani, picha zake zilipigwa marufuku na ilikuwa ni kinyume cha sheria kumnukuu hadharani.

Hata hivyo dunia ilisimama kwa umoja na kufanya kampeni za kutaka aachiliwe, nyimbo ziliimbwa na matamasha makubwa yaliandaliwa kulalamikia kufungwa kwake.

Hatimaye mwaka 1990, Rais wa Afrika Kusini FW de Klerk, alimuachia huru na alipotoka gezani na alipokelewa kama shujaa baada ya kuachiwa huru.

ANASIMAMIA MSAMAHA

Mandela ana sifa na umaarufu wa kuhimiza msamaha, kuvumiliana na usawa baina ya watu.

Utawala wa ubaguzi wa rangi ulifutiliwa mbali mwaka 1991, na miaka mitatu baadaye, Afrika Kusini iliandaa uchaguzi wa kwanza mkuu ambapo watu weusi waliruhusiwa kupiga kura kama weupe.

KUWA RAIS MAARUFU

Nelson Mandela alichaguliwa kuwa Rais mwaka 1994 na akaanza kuleta umoja baina ya watu wa rangi tofauti. Ilipotimia mwaka 1993, alipewa tuzo ya amani ya Nobel- ya kiwango cha juu na ya aina yake.

Hii ni kutambua jitihada zake na mwaka 1995, wakati Afrika Kusini ilipoandaa mashindano ya kwanza ya kombe la dunia la mchezo wa raga (rugby).

Mandela aliiunga mkono timu ya Afrika Kusini, iliyojumuisha zaidi Wazungu, jambo lililosaidia kuiunganisha nchi hiyo zaidi na kusahau yaliyopita.

Mandela ni mmojawapo ya viongozi maarufu duniani, huku wanasiasa na nyota wa aina mbalimbali walikuwa wakipanga msururu ili kupigwa picha pamoja naye.

“Hakuna atakayetulia duniani, iwapo umaskini, ukosefu wa haki na usawa vitaendelea kushamiri,” anasema,” anasema Mandela katika moja ya nukuu zake.

MWANDISHI WA VITABU

Baadhi ya vitabu alivyoandika Mandela ambavyo vinasomwa karibu duniani kote ni pamoja na "I Am Prepared to Die", Long Walk to Freedom, Mandela: The Authorised Biography, Conversations With Myself, Dare Not Linger na The Presidential Years.

FILAMU ALIZOSHIRIKI

Mandela aliwahi kuonekana katika filamu mbalimbali ikiwamo, Death of Apartheid Mandela: Son of Africa, Father of a Nation, Mandela and de Klerk, Goodbye Bafana, Endgame, Invictus na Winnie Mandela.

KIFARIKI DUNIA

Alifariki dunia Desemba, 5 mwaka 2013 akiwa na miaka 95. Angekuwa bado hai leo angefikisha miaka 103.

MTANDAO