NHIF yaanza mapambano, wajawazito milioni wana bima maalum

20Jan 2019
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
NHIF yaanza mapambano, wajawazito milioni wana bima maalum

ILI kumaliza changamoto ya vifo vya wajawazito, wazazi pamoja na watoto wachanga vinavyotokana na matatizo yanayohusiana na uzazi, serikali imewapatia wajawazito takribani 1,000,000 bima maalumu ya afya, inayowawezesha kupata matatibu wakati wowote.

Meneja Uhusiano wa NHIF Anjela Mziray.

Jitihada hizo zinafanikishwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani , uliowezesha wajawazito kupata bima ya afya ili watibiwe kila wanapohitaji huduma za afya.

Meneja Uhusiano wa NHIF Anjela Mziray, anayasema hayo na kueleza kuwa mpaka sasa wajawazito 1,044,000 wameshafikiwa na mpango huu katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Njombe, Lindi na Mtwara.

Akiwa mwenyeji wa maofisa habari wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, katika kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, waliofika ofisini kwake mkoani Arusha, Mziray, anaendelea kusema:

“Katika kipindi cha miaka mitatu, mafanikio makubwa yamepatikana ikiwamo wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kwenye huduma ya Ushirika Afya kutibiwa huku watoto kupitia huduma ya Toto Afya Kadi nao wakifikiwa na huduma za NHIF”.

Anasema mfuko pia umewezesha upatikanaji wa huduma za madaktari bingwa katika mikoa ya pembezoni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali nyingi.

Mziray anaeleza kuwa serikali inakusudia kuwafikia wananchi wote na kuwapa huduma bora za afya.

Anasema katika kutekeleza hilo NHIF, imewezesha madaktari bingwa wa magonjwa ya mbalimbali kama ya wanawake, watoto, moyo, macho, kinywa na pua na mabingwa wa upasuaji kutoa huduma katika mikoa ya pembezoni kwa kipindi maalum.

“Kwa ujumla watu zaidi ya 20,289 wamefikiwa na huduma hii na kati ya hao watu 938 wamefanyiwa upasuaji wa kitalaam na hii ni katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Lindi, Mara, Manyara, Geita, Njombe na Ruvuma huku baadhi ya mikoa tukienda mara mbili” anaeleza Mziray.

Aidha, katika mafaniko mengine ya kuboresha upatikanaji wa huduma, NHIF inashiriki juhudi za serikali za uwekezaji katika viwanda.

“Mfuko kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi zingine unawekeza katika kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za hospitali zitokanazo na malighafi ya pamba na kiwanda hiko kitajengwa Bariadi mkoani Simiyu huku kikitarajiwa kuzalisha aina 24 za bidhaa hizo,” anasema Mziray.

Anasisitiza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Magufuli, sekta ya afya imekuwa miongoni mwa maeneo yaliyopiga hatua ya mafaniko makubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu na kwa gharama nafuu.

Ili kujipima Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na taasisi zake inafanya tathimini kufahamu walipotoka, walipo na wanapokwenda katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu katika maeneo waliyopo lakini pia kwa wakati.

Anasema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya moja ya taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya, unajivunia kuongeza wigo wa wanufaika kwa kuwafikia wananchi mbalimbali.

TEHEMA

Mziray anaelezea zaidi mafanikio akitaja huduma na matumizi ya teknolojia akisema: “Mfuko huo pia umeweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama),inayowezesha kutambua wanachama katika vituo, kurahisisha ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati, kurahisisha usajili wa wanachama na kuharakisha utoaji wa vitambulisho.

Kwa upande wake, Meneja wa Mifumo ya Tehama, NHIF, Bakari Yahaya, anasema kwa sasa mifumo inamwezesha mwanachama kupata ujumbe mfupi kwenye simu yake mara tu kadi yake au ya mtegemezi wake inapotumika kwa matibabu.

“Mfuko huu sasa umefanikiwa kuwa na ofisi zake katika mikoa yote Bara na Zanzibar na tunaboresha mfumo wa mawasiliano kwa kuwa na kituo cha huduma kwa wateja kwa ajili ya kupokea simu za wadau siku zote za juma bila malipo kwa wapigaji. Simu hiyo ni 0800 110063,” anaeleza Yahaya.

Anafafanua zaidi kuwa, mfuko umepata cheti cha ubora wa huduma kwa viwango vya kimataifa ( ISO 9001:2015).

HUDUMA MITAANI

Wakiwa mkoani Arusha, maofisa hao walitembelea ofisi za kanda ya kaskazini zinazohudumia mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na kupata fursa ya kuzungumza na Meneja mkoa wa Arusha, Isaya Shekifu, ambaye anasema mbali na kuwapatia wananchi bima za matibabu pia wanatoa elimu kwa jamii namna ya kujiunga na mfuko huo.

Anaeleza kuwa wanatoa kadi za matibabu ndani ya siku saba lakini pia wanahudumia vituo vya afya zaidi ya 300 vilivyopo katika mkoa wa Arusha.

“Tunatoa elimu kwa kupita mitaani kata kwa kata kuhakikisha tunakutana na jamii moja kwa moja ili kuwaeleza umuhimu wa kutumia bima ya afya,” anasema Shekifu.

Anasema pia mbali na kutoa elimu kwa jamii pia wanatoa huduma ya matibabu bure kwa wananchi kwa kushirikiana na wataalam wa afya ili kuwahamasisha kujiunga na mfuko huo.

Shekifu anasema pamoja na jukumu la kutoa elimu pia mfuko huo una kitengo cha udhibiti ubora wa huduma zinazotolewa katika hospitali ambazo zinahudumiwa na mfuko huo.

Aidha, wanachakata madai wanayowalipa watoa huduma na kuhakikisha wanayatoa ndani ya siku 30 ili mwanachama apate huduma bila kikwazo.

Shekifu anasema katika kuhakikisha wanafikia makundi yote ya wananchi nchini ijulikanao ‘kama afya bora kwa wote’, mfuko huo utaanzisha huduma ya bima ya wananchi ambayo itakuwa ya bei nafuu.

Anasema kwa upande wa mkoa huo wanatarajia kuanza kutoa huduma hiyo kuanzia Aprili mwaka huu ili wananchi wenye kipato cha chini waweze kunufaika.

Sambamba na hilo, anasema katika kuchangia huduma mbalimbali za maendeleo ndani ya jamii, wameikopesha Hospitali ya KCMC Sh. bilioni 1.7 kwa ajili ya kujenga jengo la dharura.

Shekifu anasema baada ya kupata taarifa kuwa hospitali hiyo haona jengo la kisasa la kupokelea wagonjwa wa dharura waliwadhamini kwa kuwapa mkopo na sasa jengo limeshakamilika.

“KCMC ni moja ya hospitali ambayo tunashirikiana kwa karibu, tuliwakopesha Sh. bilioni 1.7 wakajenga jengo la kupokelea wagonjwa wa dharura na sasa wanatoa huduma katika hali nzuri,” anasema.

Mkurugenzi wa Hospitali ya KCMC, Dk. Geleard Masenga, anaipongeza NHIF kwa msaada huo, waliotoa katika kuhakikisha wateja wa mfuko huo na wananchi kwa ujumla wanapata huduma zilizo bora.

Anasema awali wagonjwa walikuwa wakiwekwa kwenye korido wakati wakipatiwa huduma ya kwanza pindi wanapofika hospitalini hapo na waliposhirikisha suala hilo kwa NHIF walitoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo.

“Tunaishukuru NHIF, tumekuwa tunashirikiana nao kwa muda mrefu na tunaendelea kufanya hivyo, wametusaidia kiasi cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura ni jambo la kujivunia,” anasema Dk. Masenga.

Habari Kubwa