Ni kigugumizi cha lugha

09Dec 2018
Gaudensia Mngumi
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Ni kigugumizi cha lugha
  • Haifahamiki ipi rasmi, Kiingereza , Kiswahili, Kiswakinge?

LEO ni miaka 57 tangu Gavana Richard Tumbull, mwakilishi wa Malkia wa Uingereza, aliposhusha bendera ya mkoloni wa Uingereza na kuipandisha bendera ya Tanganyika huru , yenye rangi angavu nyeusi, kijani na bluu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ernesta Mosha.

Ndiyo iliyokuwa siku ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Wakati mkoloni akiondoka aliliachia taifa lugha ya Kiingereza lakini akiweka mazingira ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Afrika Mashariki.

Inapozungumzwa lugha inayopaswa kutumiwa kama Tanzania ni swali ambalo halijajibiwa.

Hata leo karibu miaka 100 tangu Kiswahili kilipopasishwa na Waingereza na kuanza kufanyiwa utafiti ili kianze kutumiwa kama lugha ya asili ya Afrika Mashariki, hakuna mwenye jibu kwani serikali hajaweka wazi taifa hili linatumia lugha ipi kwa mawasiliano ya kitaifa na kimataifa.

Baada ya tafiti za wakoloni zilizochapisha kamusi ya Kiswahili na kuendeleza lugha hiyo, ni miaka 57 tangu Tanzania Bara ipate uhuru wake, lakini si serikali wala katiba, sheria au sera inayotamka kuhusu lugha rasmi ya mawasiliano.

Ndiyo maana ukiingia mahakamani Kiswahili hutumiwa kusikiliza kesi, lakini sheria nyingi zimeandikwa kwa Kiingereza hukumu nayo huandikwa kwa Kiingereza, asiyekijua inabidi asake mkalimani.

Ukifika hospitalini unaongea kila kitu kwa Kiswahili lakini taarifa na vipimo ni kwa Kiingereza. Hata dawa huandikwa kwa Kizungu unajiuliza hivi tatizo liko wapi?

Kutokana na miaka 57 ya Uhuru lakini taifa likiendelea kukabiliwa na kigugumizi cha lugha, NIPASHE inazungumza na Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ernesta Mosha, ili kupata chanzo cha sintofahamu hiyo na ushauri wake. Anayeanza na kutoa ufafanuzi….

NIANZE kwa kusema kuwa lugha si kitu kinachoishi kwenye maabara au maktaba wala si ndani ya utafiti bali ni kwenye matumizi, kuizungumza na kuitumia kikamilifu ndiko kunakoistawisha.Lugha inapanuka na kukukua kwa jinsi utakavyoipa nafasi ya kutumika.

SWALI: Ni kwanini leo hii miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara tunaona kama taifa hatuna muafaka wa lugha gani tunaweza kutumia, hili unalizungumziaje?

JIBU: Ni vyema nianze kuipongeza na kuishukuru Serikali ya Rais John Magufuli kwani awamu hii imekuwa mstari wa mbele muda wote katika matumizi ya Kiswahili.

Niseme tu kwamba lugha haikuzwi kwenye maabara ni matumizi ndipo inapanuka lakini ni kulingana na utakavyoipa matumizi.

Lakini hata sisi tunajiuliza baada ya miaka 57 tunapata kigugumizi kuhusu matumizi ya lugha kwenye baadhi ya maeneo, kama wataaluma tumemaliza kazi yetu kilibakia ni maamuzi ya serikali.

“Niipongeze awamu ya tano imekuja kivingine ikiithamini lugha yetu. Tumeshuhudia dhifa za kitaifa , shughuli za kimataifa na matukio mengi ambayo yanahusu kujumuika nchi mbalimbali lugha inayotumiwa ni Kiswahili.

Kwa mfano uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , ulifanywa kwa Kiswahili .Tena kulikuwa na mabalozi na wageni wa mataifa mbalimbali.

Kilichofanyika ni kuweka mkalimani kutoa tafsiri. Na wote ambao hawajui Kiswahili walipewa vifaa vya maawasiliano vilivyowawezesha kusikia lugha iliyotafsiriwa kwa wakati huo kilitumiwa Kiingereza na Kiswahili.|”

SWALI: Unaweza kuwafafanulia wasomaji ni kwa namna gani Kiswahili kilikuwa kimetambuliwa na kukubaliwa na wakoloni hata kabla ya uhuru?.

JIBU: Mwaka 1925 Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki iliyoanzishwa na mkoloni alipoona kuna haja ya kuwa na lugha ya pamoja, ilianza mchakato wa kukirasimisha Kiswahili.

Ilibaini kuwa kina lahaja 26 zikiwamo Kimvita, Kilamu, Kimakunduchi na Kingazija, hivyo walikaa kuona ni ipi wanaweza kuisanifisha au kuifanya rasmi (standardise).

Ilipofika mwaka 1930 wajumbe wakakutana tena wakati huo ilikuwa ni Tanganyika Zanzibar, Kenya na Uganda wakaunda kamati na miongoni mwa mambo ya msingi yaliyofanyika ni kuandika kamusi ya Kiswahili Sanifu ambayo toleo la kwanza lilitoka mwaka 1938.

Lakini kamusi imeendelea kufanyiwa kazi na kuna matoleo kadhaa ambayo hata leo yameendelea kuandikwa na kuongezwa istilahi (maneno mapya, misamiati).

SWALI :Tuambie jinsi kazi za Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki zilivyochangia kukuza Kiswahili hata sasa?

JIBU: Kazi za chombo hicho kilichoundwa mwaka 1930 zimeendelea kuenziwa na kuboreshwa, na hata leo Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) imetokana za kamati hiyo.

Kwa hiyo zimeendelezwa hadi sasa na katika mabadiliko majukumu hayo yalihamishiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikawa Idara ya Kishwahili baadaye iliboreshwa zaidi na kuwa Taasisi ya Uchunguzi Kiswahili (TUKI) miaka ya 1970 , lakini ilipofika 2009 ilibadilisha muundo wake na kuwa Tataki.

Kwa hiyo muendelezo wa kamusi hiyo leo umefikia toleo la tatu tangu kamati ilipobuniwa mwaka 1930,  lakini karibuni tutatoa toleo la nne kwa sababu maneno mapya yanaibuka. Tunatarajia wakati wowote kuanzia sasa litapatikana.

Leo tuna kamusi tatu toleo la kwanza ni la 1938, kuna Kamusi ya Kiswahili Sanifu, na Kamusi ya Kiswahili Kiingereza zote ni za Tataki. Hata hivyo tunazo nyingi.

Mfano ipo kamusi ya tiba, ya historian na kamusi ya kompyuta. Niseme pia kuwa wadau wa lugha wameandika kamusi nyingi na za kutosha zenye istalahi za kutosha.

SWALI: Kama hiyo ndiyo hali halisi kwanini bado lugha hiyo haijapewa mamlaka?

JIBU: Lugha hii ambayo msingi uliwekwa kwa miaka mingi karibu 95 au karne nzima ni kweli bado haijapewa mamlaka. Hilo ni suala la viongozi wa serikali.

Sisi wanataaluma tumefanyakazi yetu. Tafiti zimeeleza bayana kuwa huwezi kumfundisha mwanafunzi kwa lugha ambayo hawezi kuitumia kufikiria.

TUJIHOJI

“Lakini tu nikuulize swali hili mwandishi umewahi kuota ndoto kwa lugha ya kigeni mathalani Kiingereza ? Unatumia lugha hii kama lugha ya kujifunzia , lakini umeshalala na kuota njozi za Kiingereza? Jibu ni hapana.

Hii inatueleza kuwa huwezi kuwa mbunifu au mgunduzi kwa sababu ubunifu na ugunduzi ni zao la yale ambayo unaweza kuyatafakari kwa kina kwa kutumia lugha na mazingira unayoyafahamu.”

“Mimi niseme ukweli ninaungana na baadhi ya wadau wakubwa ambao walieleza kuwa elimu ya Watanzania wengi ni ya kupapasa kwa sababu badala ya kufikiria kile unachotaka kukieleza unaanza kuwaza utakisemaje kila unachotaka kukieleza.

Ndiyo sababu mara nyingi kufaulu kwa wengi kunatokana na kukariri na wala si kwa kuelewa kikamilifu kile tunachojifunza.”

SWALI: Kwa hiyo ni nini hasa chanzo cha kigugumizi hiki cha lugha?

JIBU: Ni kazi ya serikali kuamua. Sisi wataaluma tumefanyakazi yetu na tumeishauri. Maamuzi yanabaki kwa watunga sera, sheria na miongozo.

Sisi tumeeleza yale yanayotakiwa. Ukweli ni kwamba maarifa yanapatikana kwa lugha unayoifahamu.

HALI HALISI

“Kwa mfano tukiangalia leo mgonjwa anakwenda kwa daktari iwe zahanati au hospitali ya rufani daktari unamsikiliza unamwandikia kila kitu kwa Kiingereza , hivi ni Watanzania wangapi wanaelewa? Pengine ni asilimia zaidi ya 90.

Kwa hiyo kuamua hatma ya lugha ipi itumike ni maamuzi ambayo serikali itayafanya.”

Nataka kuwaambia Watanzania kuwa na lugha yako si kujitenga na dunia:“Nimefundisha Kiswahili Korea ya Kusini miaka miwili. Hakuna sehemu utakayofika ukute jambo limeandikwa kwa Kiingereza.

Hivi wale wamejitenga na dunia kwa kuipa lugha yao uzito unaostahili? Chuo nilichokuwa nafundisha kinafundisha lugha 36 za kigeni na hufundishwa na wazawa au wazungumzaji wenye asili ya lugha hiyo.”.

CHA KUFANYA

Kama taifa tunahitaji kuandaa watu wanaofahamu lugha kikamilifu , kwa mfano zamani kulikuwa na vyuo vya walimu vikiandaa wasomi katika fani mbalimbali mfano Chuo cha Ualimu Korogwe kilikuwa mahususi kwa waalimu wa Kiswahili, Marangu kililenga kuwandaa walimu wa Kiingereza , nafikiri na Chang’ombe kilikuwa cha walimu wa Kifaransa.

Utaona kulikuwa na malengo ya kupata wataalamu wa hizi lugha tatu, kwa wenzetu Ulaya , wanafunzi wanapomaliza sekondari mbali na lugha yake mfano kama ni Muitaliano lazima usome lugha nyingine mbili.

Kwa Tanzania si lazima lakini kwao ni wajibu kwa sababu wanataka  raia wao wachangamane kwa urahisi na wengine wa mataifa mbalimbali duniani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wanalenga wapate maarifa zaidi, kutokana na ukweli kuwa ukiwa na lugha nyingi unaweza kujifunza maarifa zaidi ambayo hayajaandikwa katika lugha yako ya asili.

Na sisi pia tunahitaji kufanya wanayofanya wenzetu , taifa linahitaji watu wanaofanyakazi nyingi zaidi, mfano mbali na wakalimani tunahitaji wafanyabiashara wanaokwenda sehemu mbalimbali.

Watu wa ,masoko watakaotangaza utajiri wa kitalii uliopo. Wafanyakazi kwa ajili ya kutumika kwenye ushirikiano na jumuiya za mtangamano.

Nitoe mfano wa biashara na uwekezaji ninaamini ukiwa mfanyabiashara ukizungumza na mbia wa taifa jingine anayefahamu Kiswahili biashara itakwenda vizuri zaidi.

Hiyo ni mikakati tunayotakiwa kuanza sasa kuelewa na kutumia zaidi lugha yetu yao.

Kama taifa tuna mambo mawili ambayo tunahitaji kuyatofautisha .Kuwa na lugha ambayo ni kibebea maarifa ili watu waweze kuelewa na kujifunzia.

Jambo la pili tunahitaji lugha kama chombo cha mawasiliano.Kuongea na kuwasiliana ndani na nje ya mipaka.

SWALI: Unadhani ni nini changamoto kubwa inayokikabili Kiswahili?

JIBU: Ni Watanzania walio wengi kuwaza kuwa ukizungumza Kiingereza umeelimika au una maarifa. Hivi ni vitu viwili tofauti. Wazazi wengi wanaamini na wangependa watoto wao wafundishwe na wazungumze Kiingereza.

“Hakuna lugha bora zaidi ya nyingine , Kiingereza ni lugha ya dunia lakini hali ilivyo sasa Kichina kina wazungumzaji wengi duniani , kinafuatiwa na Kihispaniola na Kiingereza ni cha tatu.

Watanzania walio wengi Kiingereza ni lugha wanayoiamini kwa sababu wamekuzwa kukiona Kiingereza kuwa ni bora zaidi.

Lakini kama mwanataaluma na mtafiti naamini hakuna nchi yeyote iliyoendelea kiuchumi wala kiteknolojia kwa kutumia lugha ya w engine au ya kuazima…”

SWALI : Kwanini Tanzania hata baada ya miaka 57 ya Uhuru inaendelea kuamini kuwa Kiingereza kitawezesha kupiga hatua kimaendeleo?JIBU: Sisi wanataaluma hatuhusiki. Ni jukumu la watunga sera, wabunge wanaosimamia serikali na kutunga sheria kuamua la kufanya.

Ila kutokana na kasumba tunaendelea kuamini kuwa Kiingereza ndicho kibebea maarifa ndiyo maana tunasisitiza kuwa tuwe na lugha nyingi na zifundishwe vizuri tena kikamilifu lakini tuwe na lugha ya kutolea maarifa ambayo sisi sote kama taifa tutaelewa nayo ni Kiswahili.

Kuanzia shuleni mwalimu na mwanafunzi, madaktari kwenye tiba za daktari na mgonjwa, kortini hakimu na mlalamikaji na mshitakiwa.

Sisi wanataaluma tunaendelea kusisitiza lugha haiwezi kukua ikiwa maabara watu ndiyo wanaotakiwa kuikuza.

SWALI: Unazungumzia ukosefu wa vitabu? Tumesikia malalamiko kuwa Kiswahili hakina vitabu tumeandika vitabu vya kufundishia na seti yote imekamilika ya kufundishia kidato cha kwanza kuanzia Fizikia , Kemia, Jiografia, Hisabati na Bailojia kwa ajili ya kidato cha kwanza kozi zote zimekamilika.

Ni hatua ya kwanza kwa sababu hakuna mtoto anayezaliwa na kutembea.

Ni kwa taratibu kwani hata miaka 500 iliyopita Kiingereza hakikuwa kwenye ramani ya lugha , kwa hiyo tutaendelea.

Tunapoanza kuendeleza Kiswahili hatua moja tunayochukua ni ya msingi na iwe kama mtoto, tusiseme hivi mpaka niwe na kila kitabu, jarida au kamusi ndipo tuanze.

Kumbuka hata mtoto unayemuona leo anatembea mama alianza na mimba.

Hatuwezi kuandika vitabu vyote kwa wakati mmoja ndiyo maana tumeamua tuanze na kidato cha kwanza ili wanaoanza na Kiswahili waanze hadi kukamilisha, lakini wale walioanza Kiingereza waendelee hadi kukamilisha, kama taifa tuipe nafasi lugha ambayo Watanzania wanaielewa.

Habari Kubwa