Ni lazima kumkanda maji makali aliyejifungua?

19Mar 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe Jumapili
Ni lazima kumkanda maji makali aliyejifungua?

JUZI Nipashe iliulizwa swali na mama aliyejifungua hivi karibuni akiomba kama inawezekana asaidiwe kupatiwa anuani za mtandao ili kufahamu iwapo mwanamke anapojifungua analazimika kula chakula cha moto kinachounguza na pia kukandwa na maji makali ya moto yanayomchoma.

Ushauri wa awali aliopewa ulikuwa akamuulize daktari wake, lakini pia kumtumia anuani za mitandao akajisomee mwenyewe.

Kwa kuwa pengine ni suala linalowahusu wanawake wengi , inaelezwa kuwa hakuna sababu ya kumuadhibu aliyejifungua kwa kumlisha vyakula vinavyochoma na kumkanda kwa maji yanayoungaza pia.

Mtandao wa ‘voanews.com na newshealthguide.og’ unaeleza kuwa kutumia maji ya moto kwa mama aliyejifungua kunaweza kuleta madhara baadala ya manufaa.

Kuwakanda wazazi kwa maji ya moto makali ni jambo linalofanyika kwa jamii nyingi lakini si tiba njema kuiendeleza kwa mujibu wa taarifa ya kitaalamu iliyoandikwa na Sauti ya Amerika (VOA).

Inasema japo wengi wanafanya huduma hiyo lakini, hakuna uthibitisho kuwa maji yanaponya mwili, tumbo na sehemu za siri baada ya uzazi.

Mtandao unasema maji ni lazima lakini yawe ya uvuguvugu unaoweza kustahimili joto la mwili lakini si ya kumchoma mzazi. Wapo wanaowarushia wazazi suka la moto kuwachoma kwa vile hata wenyewe hawawezi kulikamua na kuwakanda kwani wataungua. Ndiyo maana wanasema huko ni kumchoma aliyejifungua siyo kumsaidia.

Lakini utafiti wa mitandao hiyo unaeleza kuwa inawezekana mama akakaa kwenye beseni lenye maji ya moto na dawa pengine miti dawa ama za hospitalini kama detol na savlon ili kujitibu lakini asijmwagie maji makala sehemu za siri kwa kuwa ngozi yake ni laini na itaungua na kuchubuka zaidi kutokana na shuruba alizopitia wakati wa kujifungua.

VOA inamnukuu bingwa wa uzazi na daktari wa magonjwa ya wanawake huko Cameroon Dk. Robinson Mbu, akieleza kuwa maji makali ya moto wanayokandwa wanawake hayana umuhimu wowote kwa mujibu wa utafiti uliofanyika kisayansi mbali na kusababisa vidonda.

“Kukanda tumbo kwa maji yanayochoma ni hatari kunaweza kusababisha kizazi kutanuka na mama kutokwa na damu nyingi ambayo ni hatari kupindukia . Nisema kuwa lolote linalosababisha mzazi kupoteza damu nyingi akishajifungua si jambo jema” anaonya Dk Mbu.

Kwa baadhi ya wanawake iwe mijini na vijijini wanapenda kutumia maji makali siyo tiba njema. Ni vizuri kumkanda kwa maji yenye joto la kawaida lakini ambalo haliunguzi mtu baada ya kujifungua.

VYAKULA VYA MOTO
Kwa upande wa chakula haina maana kumchoma mzazi midomo na ulimi kwa kumpa supu, uji, mtori, maziwa na chai inayounguza, kisa eti ni kuongeza kasi ya kusukuma damu mwilini na kuondoa vitu vyote vilivyoko kwenye nyumba ya uzazi kwa haraka.

Wanaowahudumia wazazi wanaweza kusabisha kifo cha mama iwapo ana tatizo la shinikizo la juu la damu kwa vile kula vyakula hivyo vinavyochoma vinaweza kuongeza kasi ya mzunguko na msukumo wa juu wa damu na kusababisha matatizo au kifo.

Lakini pia ikumbukwe kuwa chakula kikiingia tumboni mwili (ubongo) hurekebisha joto lake ili lilingane mahitaji ya mwili ambayo ni sentigrade 37, kwa hiyo, hakiwezi kubakia na joto ambalo watu wanadhani linasaidia kusukuma damu na kusafisha kizazi baada ya mama kujifungua.Japo inashauriwa mzazi kula vyakula vya moto siyo vya baridi ili kusaidia uchakataji na uchukuliwaji wa chakula mwilini.

Kwa ujumla ili kulinda afya na kufahamu ukweli kuhusu ustawi wa mwili wako unatakiwa kuuliza maswali wataalamu . Wasomaji waulize na kutafuta ukweli kwenye magazeti , mitandaoni na kwa wataalamu badala ya kubakia kuishi maisha ya kimapokeo au kwa mazoea, kama kutumia maji ya moto kwa mzazi na kumlisha vyakula ambavyo vinaweza kumsababisha mzunguko mkubwa na wa kasi wa damu.

Habari Kubwa