Ni mwaka mpya acha ‘ kuahirishaahirisha’

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ni mwaka mpya acha ‘ kuahirishaahirisha’

IKIWA ni wiki ya kwanza tangu tuingie mwaka mpya, niwatakie wasomaji wangu heri ya mwaka mpya 2019 nikiwaombea baraka tele kwa yale yote mliyoazimia kuyafanya kwa mwaka huu.

MSIMU WA KUWEKA MALENGO MAKUBWA BAADA YA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA KRISMASI

Hiki ni kipindi kifupi toka wengi wetu tutoke kwenye shamrashamra za msimu wa sikukuu za Krismasi, mwisho na mwanzo wa mwaka na kila mmoja anarudi kujipanga kivingine ilimradi aweze kufanya makubwa zaidi ya mwaka uliopita ama kupunguza baadhi ya makosa yaliyomkwamisha na kushindwa kutimiza malengo na maazimio aliyojiwekea.

Kila mwezi Januari ukifika imezoeleka kwa walio wengi huwa ni kipindi kigumu kwa sababu kina ‘hangover’ ya kumaliza na kuanza mwaka huku mifuko ikiwa imechalala kweli kweli.Wakati huu ni kipindi ambacho kinaingiliana na masuala mengine muhimu ya kimaisha kama kodi za nyumba kwa wanaopanga na ada za watoto kwa madarasa tofauti.

Kama masuala haya mawili yanakukabili basi mwezi huu kwako unakuwa mchungu haswaa, hapo ndipo unaposahau ghafla raha zote ulizozipiga mwezi uliopita. Zaidi kinachoumiza kichwa ni namna gani utaweza kupambana na hali yako ili watoto warudi shule na kodi ya nyumba ilipwe. Kwa mantiki hiyo badala ya mwezi huu kuwa Januari unageuka “Njaanuari” kwa sababu ya pochi kukaushwa na sherehe.

Nimeanza kwa kuchangamsha genge tu kuita Januari Njaanuari kwa kuwa wengi wetu hatuna tabia ya kuweka akiba na kuwa na bajeti ya matumizi ya fedha hususani unapofika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, baadhi tunaongozwa na mihemko ya matumizi makubwa ya fedha bila kujua hatma ya kesho . Si unajua tena furaha ya kufika mwisho wa mwaka, basi akili huwaza kula bata lililojaa furaha tele, yaani bata kama lote.

Mara nyingi mwaka unapoanza kila mmoja huweka maazimio, mikakati na malengo kwa ajili ya mwaka husika. Kuna wanaopanga kuhusu afya zao, wengine biashara, familia, ndoa na kazi kutegemeana na hitaji la kila mtu katika kutimiza lengo lake.

Pia ni muda hata kwenye vipindi vingi vya redio na runinga hubeba maudhui juu ya namna ya kuzungumzia malengo na jinsi ya kuyatimiza kwa kuwaalika wataalam wa masuala ya malengo na mipango kwenye nyanja mbalimbali ili kuwachambulia walengwa wao.

Twende mbele,turudi nyuma tena hili unaweza ukalithibitisha kwa kuangalia maisha yako, ni mara ngapi umekuwa ukisema kuwa mwaka huu nitafanya hiki na kile. Lakini inapofika mwisho wa mwaka unashangaa yale malengo yote mazuri uliyokuwa umejiwekea hujayatimiza kwa sehemu kubwa?

Na kuna wakati umekuwa ukijiuliza ninini tatizo ama sababu ya kushindwa kutimiza ndoto zako? Unakosa majibu ya uhakika. Nikumbushe kwenye makala yangu ya kufunga mwaka iliyochapishwa Jumapili iliyopita nilisisitiza juu ya tabia mbalimbali zilivyowakwamisha wengi kutimiza malengo yao na niliweka msisitizo mkubwa juu ya mabadiliko ya tabia ili kufanikisha yale mtu aliyoyakusudia.

Unapaswa kujua kwamba kutimiza malengo kunasumbua kwa asilimia 95 watu wote duniani.

Nakiri wazi kuwa mabadiliko ya kitabia si jambo jepesi lina maumivu makali , kuikana tabia uliyoishi nayo miaka nenda rudi si lelemama inahitaji roho ngumu. Wakati huu ukikaa na watu kwenye vijiwe na maeneo tofauti utasikia viapo vya mabadiliko ya kufanya vitu vikubwa kwa mwaka huu hakuna asiye na mipango kambambe na mizuri. Kila mmoja anakupa mpango na kiapo juu.

Kwenye kupanga malengo ugonjwa mkubwa unaowasumbua wengi ni kuahirishaahirisha mipango waliyopanga. Kuahirisha huko kwa kimombo wanaita ‘procrastination’, ni tabia ambayo inamfanya mtu kusogeza mbele mambo ambayo angetakiwa kuyafanya sasa.

Msuala yanayosogezwa mbele ni mambo muhimu na ambayo mtu angetakiwa kuyafanya kwa wakati huo ili aweze kutekeleza majukumu yake au kufikia malengo. Na hata pale anapopeleka mambo hayo mbele, kwa wakati huu anakuwa hafanyi vitu muhimu kama vile aliyoyasogeza mbele.

Tabia ya kusogeza mambo mbele inamuathiri kila mtu. Hata uwe unatunza muda kiasi gani, kuna wakati utajikuta unakwepa baadhi ya majukumu yako au kuyasogeza mbele.Tabia ya kuahirisha mambo ni kikwazo kikubwa sana kwenye kufikia mafanikio makubwa. Sababu kubwa mpaka sasa bado hujaweza kufikia malengo na mipango yako kwa asilimia kubwa ni tabia ya kuahirisha baadhi ya vitu vya msingi unavyotakiwa kufanya.

Tafiti zinaonyesha kwamba watu wenye tabia za kuaihirisha aihirisha kufanya masuala waliyopanga mara nyingi huwa na hali ya kushindwa kujisimamia wenyewe, kutofuata matumizi ya muda na kushindwa kuweka mikakati huku hali hiyo ikisababishwa na kuwepo na mwanya kwenye dhamira na matendo ya mhusika.

Kinachokufanya kukamilisha au kutofanya jambo lolote ni dhamira ilhali matendo yako yanasaidia mno kukamilika kwake kwa wakati. Katika kuweka msisitizo juu ya dhamira na matendo wanasaikolojia Alex Grund na Sten Faries kutoka Chuo Kikuu cha Biekland , Ujerumani kwenye utafiti wao kuhusu kuelewa kuhusu kuahirisha aihirisha malengo wanasema tabia hii ya haiathiri dhamira ya kufanya jambo bali hushikilia dhamira ya kutofanya kitu hicho kwa wakati.

Utaona kuwa dhamira ndiyo msingi mkubwa katika kufanikisha mambo yako lakini kwanini unakwama? Ni kwa sababu kuisimamia dhamira inakuwa kitu kinachohitaji uimara wa nafsi. Wenye tabia hii malengo mbalimbali tafiti zinaonyesha kwamba wanakuwa na kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo na afya duni.

Hivyo unapoona kuna kukwama kwama kwenye malengo kuna uwezekano mtu huyo hayuko sawa kiakili na kimwili. Pia unaweza kuwa unaahirisha mambo bila kujui kwamba unafanya hivyo. Hii inatokana na kwamba tabia hii imeshakuwa sehemu ya maisha na hivyo kwako unaona ni kawaida.

Ikishafikia hatua tabia inakuwa imekuingia mwilini hivyo hukuondolea hofu na kutokuogopa tena jambo lolote lile lionalokuja mbele yake, hapo sasa unakuwa mteja wa uahirishaji.

Kitu kingine kinachojitokeza wakati unapoahirisha malengo yako hujisikii vibaya kwa wakati ule kwani hujipa moyo kuwa una nafasi ya kufanya wakati mwingine na kinachotokea hapa ni ile hali ya kujipa tumaini na kuiridhisha roho yako kuwa ‘nitafanya tu’ huku akili ikiwa na amani ya kuona umefaulu kukabiliana na jambo hilo.

Ila muda ukifika wa kuonekana matokeo kwa jambo hilo uliloliahirisha ndipo hali ya hatia, fedheha na wasiwasi hujitokeza huku majuto yakikupa maumivu ya nafsi.

Pamoja na yote ukweli unabaki kwamba kwenye kutimiza malengo siyo kila mtu anaweza kuyafikia makusudio na maazimio aliyoyapanga kwa wakati huo, kama umejaribu mara kadhaa na kuishia ‘kupiga marktime’ unapaswa kutafuta msaidizi mtaalam ili akusaidie.

Msaidizi mtaalamu anayehusika na kukusimamia malengo na kukusaidia kupunguza tabia hizo anaitwa “accountability partner” ambaye kazi yake yeye ni kioo cha kujitazama kwenye kila hatua ambayo unapiga mpaka pale unapokamilisha yale yote uliyoyapanga.

Tukiwa kwenye mwezi wa kwanza wa 2019, ikifika Desemba tupigiane simu kufurahia malengo yaliyotimia epuka kuahirishaahirisha kumbuka ni maradhi yatibu.

    

 

Habari Kubwa