Ni utata au uhalisia gharama na viwango vya elimu nchini?

24Nov 2020
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
Ni utata au uhalisia gharama na viwango vya elimu nchini?

KUNA jitihada miongoni mwa wazazi na walezi wenye uwezo kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma shule zenye elimu bora na mara nyingi ubora hupimwa kwa kuangalia Kiingereza kama lugha ya mawasiliano, ufaulu kitaifa na karo.

Elimu bora ni pamoja na viwango vya taaluma, lugha inayoleta uelewa na ufahamu wa mambo si ukubwa wa ada. PICHA: MTANDAO

Pengine kuna ukweli au haupo ni suala la mzazi au mlezi katika hisia lakini la msingi ni kwamba elimu ya darasa la kwanza, au la sita ni ile ile hata shule ingekuwa inalipiwa ada ya Sh. 1,000,000 kwa muhula na zipo zinazolipwa zaidi ya hapo.

Hata hivyo, wahusika wanaamini na kufurahia kuwa wamefanya jambo la maana.

Ni wazi kuwa kinachotafutwa siyo elimu peke yake ila wazazi na walezi kujiridhisha kuwa wamempeleka mtoto kwenye shule iliyo bora zaidi au anasoma katika shule ambayo kiwango chake ni miongoni ambazo zina ubora wa ngazi hiyo.

Swali hapa ni hili ni kwa kiasi gani inawezekana wanafunzi hao wapate kitu cha ziada ikilinganishwa na waliobaki? Na kama kwa mfano katika ufaulu hali hiyo inajionyesha ipasavyo na kuna thamani halisi ya elimu na manufaa mengine kulingana na fedha zinazotolewa?.

Ukiangalia kwa mazoea au kwa kusikia kutokana na matangazo ya kila wakati ya ufaulu wa shule au mwanafunzi, kuna picha kuwa ni katika shule za msingi ambako kuna ushindani mkubwa zaidi? Wazazi na walezi wanaangalia ni shule ipi iliyo bora zaidi? Viwango vya malipo vikoje?

Kuachilia mbali shule za msingi kwenye sekondari pia kuna tofauti lakini kwa kiasi fulani zinapungua na kiwango cha hisia ya sifa kuhusiana na shule anayosoma mwanafunzi wa ngazi ya sekondari siyo kama mzazi au mlezi anavyojisikia kwa shule za msingi, hali ambayo inaleta utata kimantiki.

Suala ni kuwa kiwango cha ufaulu shule ya msingi halipewi uzito mkubwa kwa vile kinachotazamwa ni kuingia sekondari.

Kinacholeta mantiki hata hivyo ni kuwa elimu ya msingi ni nyeti kwa ukuaji wa mtoto kielimu baadaye kwani kila kitu kinamtegemea mwalimu au walimu kwa jumla na hivyo ubora wa shule unakuwa ni jambo muhimu mno.

Mwanafunzi akishafika sekondari, suala la kujisomea na upana wa kuelewa kutokana na vipaji au mwelekeo fulani kwa mfano katika michepuo ya fani za sanaa, biashara au sayansi, inaanza kuonekana na hiyo haitegemei sana anachopata darasani.

Ukiwapo msingi bora na wa kutosha kumwezesha kufikiri kuhusu tatizo fulani, inawezekana akaanza kuunda hiki au kile na kukitafutia majibu.

Ina maana kuwa wazazi na walezi hawajakosea katika kutoa gharama kubwa kwa watoto wao kupitia shule zenye sifa bora za ufundishaji au mazingira mazuri ya kusoma.

Kwa miaka mingi watoto wamekuwa wakipelekwa shule nchi za jirani ili kuwa katika mazingira ya kuongea na kuandika Kiingereza kila wakati, siyo kuongea tu darasani halafu mtoto akitoka nje anatumbukia katika Kiswahili, hivyo kufifisha uzoefu wake wa lugha.

Ni tahadhari muhimu endapo elimu hiyo itaenda hivyo muda wote hadi amalize chuo, azoee ufasaha huo.

Ndiyo hapo unakuja mkanganyiko ambao unawasibu watoto kwa kiwango fulani, kuwa wakati anaanza shule wazazi au walezi wana pesa kiasi fulani wanampeleka Shule ya Kiingereza.

Wakati hajamaliza elimu ya msingi mazingira ya kipato nyumbani yakibadilika, kwani kupata na kukosa ni majaliwa, hivyo iwe ni budi kumhamisha mtoto kuingia shule za kawaida,
zinazotumia Kiswahili. Mara nyingine mtoto anapata taabu kuanza kuelewa mtiririko wa kile kinachofundishwa, kwani alishazoea maelezo tofauti sana. Yako mazingira, kama ni kutaka tu kupunguza gharama, mzazi au mlezi anamwacha mtoto katika shule ya kulipia inayotumia Kiingereza, ili asivurugwe uelewa wake kwa mtiririko huo.

Ukiangalia hali hii nyingine, unakuta kuwa tofauti mojawapo iliyopo si ubora wa elimu au ngazi yake kitaaluma na kimaisha ila aina ya mazingira ambayo mtoto anaandaliwa kuishi na kwa maana hiyo shule za msingi za kutumia Kiingereza zinamwandaa mtoto kuweza kutumia lugha hiyo wakati wote.

Ni kumwandaa awe na urahisi zaidi wa kufikiri na kujieleza kwa Kiingereza kuliko Kiswahili, licha ya kuwa endapo ataingia sekondari ambayo yenye mazingira hayo ya Kiingereza ataanza kupoteza mazoea hayo ila atajimudu kuongea vyema bila tatizo.

Ndiyo tofauti na waliosoma kwa Kiswahili shule za msingi na sekondari ‘Uswahilini,’ ambako masomo yanafundishwa kwa Kiingereza ambacho wanafunzi wanaendana nayo.

Masomo yakiisha anakuwa kama amekombolewa, aingie kwenye mandhari yake aliyozoea na siyo kulazimishwa kuongea kimombo ambacho hakikai vizuri kichwani, anatumia maneno machache kueleza hisia alizo nazo, masomo tofauti yanakuwa na misamiati inayofahamika haraka, kwa mfano neno ‘process au I mean.’

Siyo mazingira ya kumwezesha kijana asome vitabu tofauti na kujisikia vyema kwani haendani na msamiati wa kitabu, hali inayojenga utegemezi wa ‘past papers,’ mitihani iliyopita, kama msingi wa kujisomea kutafuta kufaulu.

Suala la kufikiri, kutatua changamoto zinazotokea na kuzieleza kwa kina linakuwa halipo, kwani kufanya hivyo lazima ujisikie vizuri katika lugha, ufuatilie kilichotangulia, ndipo uanze kujenga taswira ya kitu kingine.

Ni kushiriki mjadala, siyo kuelewa tu na kuishia katika kujibu na kufaulu mtihani.

Habari Kubwa