Ni vilio, simanzi

03Sep 2016
Abdul Mitumba
Nipashe
Ni vilio, simanzi
  • *Vifo vyaongeza machungu wananchi kijiji cha Kikulyungu, kando ya mbuga ya Selous

SEPTEMBA 21, 2014 ilikuwa siku nyingine ngumu kwa wananchi wa kijiji cha Kikulyungu baada ya kushuhudia aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, Salum Kitonda akiuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori.

Hiyo ni kama ishara ya kukomaa kwa mgogoro wa mipaka ya ardhi kati ya wananchi na askari wa pori la akiba Selous wilayani Liwale.

Kitonda alidaiwa kuuawa na askari hao akiwa pembezoni mwa bwawa la Kiurumila, muda mfupi baada ya kumaliza kuvua samaki, kwa madai kuwa bwawa hilo limo ndani ya eneo la pori la akiba ambako wananchi hawaruhusiwi kuvua samaki bila kibali kutoka Idara ya Maliasili.

Awali, Mei 30, 2012, inadaiwa kuwa mgogoro huo ulisababisha kifo cha mtu wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Rashid Mkumbo ambaye pia inadawai kuwa alipigwa risasi na askari wa pori hilo, miaka mitatu tu tangu kuanza kwa mgogoro huo ambao athari zake zinazoongezeka kila uchao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikulyungu, Miraji Mbutule amethibitisha kijiji chake kumpoteza Kitonda na kusisitiza kuwa kifo hicho ni sehemu ya madhara yatokanayo na mgogoro huo wa mipaka ulioibuka mwaka 2009.

“Nimechaguliwa kuwa kiongozi wa kijiji kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014, lakini kabla nimekuwa nikishiriki harakati mbalimbali zenye lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo,” alisema.

Alisema kufuatia mauaji hayo kijiji kililazimika kuunda kamati maalumu ya watu watatu na baadaye wakafikia saba ili kutafuta hatma ya mgogoro huo.

“Kamati hiyo iliongozwa na Hashim Lupile ambaye wakati Kitonda anafariki ndiye alikuwa mwenyekiti wa kijiji. Wajumbe ni Mussa Magona, Abdallah Kanunga, Rajabu Lijaa, Hashim Mpuguya, Abdallah Mbunju, Mohamed Liungo, Zaina Mkape na Mussa Pange,” alisema.

Mbutule alisema kabla ya kamati yake kuanza kupanda ngazi moja hadi nyingine kutafuta majibu ya maswali yaliyogonga vichwa vya wanakijiji, ilimuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Liwale (OCD) kumjulisha kuwapo kwa mauaji hayo.

Katika barua hiyo ya Februari 24, 2015 pamoja na mambo mengine, ilimtaka OCD kufuatilia kwa karibu matukio ya watu kuuawa ili sheria zichukue mkondo wake na pia yasijirudie.

Aprili 25, 2015, kamati kwa kushirikiana na serikali ya kijiji iliiandikia barua Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ikiomba taasisi hiyo kusitisha mpango wake wa kufunga jalada la kuchunguza mauaji hayo yaliyotokana na mgogoro wa mipaka.

Barua hiyo iliyosainiwa na Mbutule ilitokana na barua ya Mei 28, 2014 ya tume iliyosema ‘kutoshughulikia mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Kikulyungu na pori la akiba Selous, Wilaya ya Liwale’.

Nakala ya barua hiyo inaonyesha kuwa awali, tume iliwataka wajumbe wa kamati kuwasilisha vielelezo vya madai yao ndani ya miezi mitatu lakini kutokana na mawasiliano duni, kamati ilichelewa kufanya hivyo.

Barua ya tume ilisainiwa na maafisa watatu ambao, Kamishna Ali Rajab na Afisa Uchunguzi Mkuu, Shomari Philipo, ambapo ilisema ilijitoa baada ya kubaini bwawa la Kiurumila linalodaiwa lipo ndani ya eneo la kijiji wakati siyo kweli.

Akizungumzia kifo cha Kitonda, mjane Mwajuma Mkape alisema mumewe amemwachia watoto watano anaowalea kwa shida.

Aliwataja watoto hao kuwa ni Aboubakar Kitonda, Fatuma, Fajida, Faudhia na Mayasa ambapo watatu kati yao wanasoma sekondari na hivyo mahitaji yao ni makubwa zaidi.

“Kwa ujumla sina raha hata kidogo, maisha yangu yamekuwa magumu kwa sababu wakati wote nimebaki mpweke. Sijui nani anaweza kunisaidia kukabiliana na changamoto za kulea watoto wangu,” alisema Mwajuma.

Mzee Abdallah Mbunju (77), mkazi wa kijiji cha Kikulyungu alisema kati ya mambo ambayo serikali inapaswa kubebeshwa lawama ni kushindwa kumaliza mgogoro huo.

“Kinachoonekana hapa ni uonevu tu unaofanywa na askari wa wanyamapori dhidi ya raia hasa ikizingatiwa mwaka 1948 serikali ilituhamisha watu kutoka ng’ambo ya mto Matandu na kutuleta upande wa kijiji ili kupisha uanzishwaji wa pori la akiba Selous,” alisema.

Mbunju aliyezaliwa mwaka 1939 anasema waliambiwa na serikali kuwa mwisho wao wa kuwinda wanyama, kuvua samaki na hata kulima ni kwenye ukingo wa mto Matandu kabla ya kuweka mipaka rasmi mwaka 1974 kwa tangazo namba 275.

Baba mzazi wa marehemu Mkumbo aliyefariki mwaka 2012, Ali Saidi Mkumbo, alisema kuwa tukio la kifo cha Kitonda ni kama limetonesha kidonda chake cha moyoni ambacho kilianza kupona.

Alisema kuwa ni vigumu kuamini matukio yanavyoendelea utadhani nchi haina uongozi, kwa sababu haiwezekani watu wasio na hatia waendelee kuuawa na askari kwa sababu ya mpaka wa ardhi uliopindishwa kienyeji na kikundi cha wachache.

"Hapa kuna kila aina ya ushahidi kwamba eneo ambalo watu wanapigwa hadi kufa ni eneo la kijiji, kwa sababu kuna ramani ya mipaka ya kisheria iliyowekwa na serikali, lakini haieleweki kwa nini mauaji yanaendelea?" aliuliza Ali.

Diwani wa kata ya Barikiwa, Lidini Jafari anasema kuwa mgogoro huo umechangiwa zaidi na wakazi wa Kikulyungu waliopata nafasi ya kuongoza na watalaamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kubainisha mpaka halisi kati ya kijiji chao na pori la akiba.

Anasema maafisa wa wizara ya Maliasili na Utalii walifika kijijini hapo na kuendesha zoezi la kuhakiki mipaka kwa siku mbili mfululizo, lakini cha kushangaza waliowakilisha wanakijiji walishindwa kuonyesha mipaka sahihi.

Alisema Barikiwa ni moja kati ya vijiji vinavyopakana na pori hilo la akiba na kwamba hatua ya Kikulyungu kuondolewa katika Jumuiya ya Magingo imekiathiri kiuchumi.

“Kwa mfano, hivi sasa kijiji kimekosa mapato yanayotokana na asilimia 75 ya malipo ya dola za Marekani elfu 30 kila mwaka zinazotolewa na wizara baada ya kulipwa na wawekezaji wanaowinda wanyama katika vitalu vilivyopo kwenye pori hilo,” alisema.

Jafari amefafanua kuwa, kati ya hizo asilimia 50, vinagawiwa vijiji vilivyo wanachama wa jumuiya ya Magingo na asilimia 25 ya fedha hizo hutumika kwa shughuli za utawala, lakini kwa miaka zaidi ya mitano sasa Kikulyungu haipati kwa sababu ya mgogoro huo.

Aliongeza kuwa, wakati Kikulyungu ikiendelea kukosa pesa hizo mwaka 2013 pekee Kijiji cha Barikiwa kilipata Sh. milioni 10 na kijiji jirani cha Chimbuko kilipata Sh. millioni nane.

Wiki chache baada ya mwandishi kuanza kufuatilia mgogoro huo, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Liwale ikiongozwa na mwenyekiti wake, Sarah Vicent Chiwamba, ililazimika kwenda kijijini Kikulyungu ili kubaini ukweli.

Katika msafara huo, Chiwamba ambaye ndiye mkuu wa wilaya hiyo, alitembelea kijijini Kikulyungi Agosti 13 mwaka huu akiongozana na maafisa kadhaa wa serikali ngazi ya wilaya akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Justine Monko, Afisa Upelelezi Wilaya na Mkuu wa Kikosi cha Kuchunguza na Kupambana na Rushwa Liwale (Takukuru).

Wengine ni Damasa Mumwi ambaye ni Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Mtendaji Mkuu wa Kanda ya Kusini Mashariki wa Pori la Akiba Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Salum Kulunge na askari wanne wa Selous, Liwale.

Upande wa wanakijiji uliwakilishwa na mwenyekiti wa Kijiji, Miraji Mbutule, Afisa Mtendaji Sadick Kiindikwa, wajumbe wawili wa kamati inayoshughulikia mgogoro Musa Magona na Abdallah Kanunga pamoja na Diwani wa kata ya Mfano, Mussa Panje.

Wengine walioingia ndani ya pori hilo ni Afisa Mtendaji wa Kata, Abeid Majumu, wajumbe wa kamati ya maliasili ya kijiji Ayoub Kapindijega, Omari Mbutule, Haji Panja na Hassan Upile.

Akiwa porini, Chiwamba alitoa fursa kwa kila upande kati ya zilizohasimiana kuonyesha mpaka halali na ushahidi, ambapo upande wa wanakijiji ulionyesha kumridhisha.

Wanajijiji hao walionyesha mpaka na jiwe kama alama ya kudumu iliyowekwa na serikali mwaka 1974 pamoja na ramani iliyoonyesha (GN), wakati askari wa pori la akiba hawakuwa na viambatanishi vinavyoonyesha uhalali wa mpaka walioonyesha.

Mwandishi wa makala hii alipomtaka Kulunge azungumzie matokeo ya ziara hiyo na hali ya mgogoro kwa ujumla, alikataa kusema lolote na huo ukiwa ni mwendelezo wa kukataa kushirikiana na vyombo vya habari licha ya awali kuandikiwa barua kuhusu kadhia hiyo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kikulyungu katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua mipaka, DC Chiwamba aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu hadi kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Lindi ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Godfrey Zambi, itakapokwenda kukagua na kujiridhisha juu ya uhalali wa mipaka hiyo.

Msaidizi wa Zambi, Mwinjuma Mkungu, alisema ziara ya kamati kwenda Liwale kukagua mipaka hiyo imepangwa kufanyika Septemba 5 na 6 mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, aliahidi kulitolea maelezo ya kina tatizo hilo baada ya kupata taarifa kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Habari Kubwa