Ni zama za kuhuisha uzalendo, na fikra pevu za Muungano

21Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ni zama za kuhuisha uzalendo, na fikra pevu za Muungano

JUBILEI ya miaka   57 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar imewadia wiki ijayo, kwa umoja wao Watanzania na Wazanzibari wanakumbuka tukio hilo la kuunganisha mataifa yao na kutazama mafanikio na changamoto ili kuuimarisha na kuudumisha zaidi.

Waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, wakitiliana saini hati za makubaliano.PICHA: MTANDAO

Licha ya kuvuka mabonde na mito wengi wanautizama Muungano kama ‘mboni ya jicho’ la siasa za Tanzania na kwa ujumla wananchi wanakuwa waoga wa kuuzungumzia na kuelezea hisia zao.

Ni kweli kuwa japo  Muungano umeishi kwa zaidi ya nusu karne unaogopwa kuzungumziwa na kwa miaka ya hivi karibuni sera za vyama vingi pamoja na kuandikwa kwa katiba mpya ambayo hata hivyo ilikwama , ndivyo vitu vilivyofungua mjadala, kuujadili  hasa katika kikao cha Bunge Maalum la Katiba na kwenye kampeni za kisiasa.

Wakati Jumatatu ijayo   Muungano unatimiza miaka 57 ni wakati wa kuufanya Muungano uwe wa wananchi, usiiogopwa wala kuhofiwa kwa kuunda mamlaka maalumu ya kuusimamia na kuuendesha unapoingia kwenye hatua nyingine ya maisha au kufikia miaka mia au Jubilei ya miaka 100.

Leo majukumu ya Muungano yako ndani ya Ofisi ya Makamu wa Rais, eneo linaloshughulikia pia Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, pengine kuna haja ya serikali ya awamu ya sita kuwa na chombo mahsusi cha kuusimamia Muungano na chenye dhamira ya dhati ya kutengeneza mazingira ambayo yatawafanya Watanzania kuupenda, kuuheshimu, kuujadili, kuukubali na pia itakuwa inaangalia matakwa ya wananchi kuhusu umoja huo kwa kutizama kila Wazanzibari na Watanzania Bara wanachokitaka.

Ni wazi kuwa kukiwa na chombo au mamlaka ya kuendeleza Muungano itatekeleza majukumu yake kwa utashi wa kisiasa  na  siyo kufanya mambo kwa mtindo wa mazoea ili kutimiza lengo la kuhakikisha kuwa unadumu na kuuleta karibu na wananchi.

Muungano utadumu na utaendelea kuwapo kwa sababu serikali imetekeleza kile wananchi walichokitaka na hasa kuona umoja na mshikamano wa mataifa hayo, unaboresha maisha yao  au kwa maana nyingine watu hawataki  siasa, wanapenda mabadiliko na maisha bora.

Kazi za chombo hicho endapo kitaundwa ziwe ni kuhakikisha kuwa Muungano unabaki kuwa jicho linalowalinda na kuwanufaisha  mamilioni ya wananchi ambao hawana chama wala hawajui vyama vya siasa vinafanyakazi zipi, bali wanataka kuona maendeleo.

Ndani ya Muungano kinachotakiwa ni kukumbuka kuwa Watanzania wengi wanachotaka ni kupata haki zao za msingi za kiuchumi, kijamii  na fursa za kuendesha maisha yao  kwa mfano, mkulima anataka ardhi ili azalishe.

Wavuvi walioko Kizimkazi, Bagamoyo, Rufiji na Kojani wanapenda kuona miundombinu na teknolojia ikiwawezesha kuvua ndani ya bahari kuu na kuinua maisha yao wakati wafanyabiashara wanapenda kuuza na kununua kutoka Zanzibar, Tanga, Arusha na Pemba bila kusumbuliwa na mamlaka za mapato iwe TRA au ZRB.

Wazanzibari na Watanzania Bara wanataka Muungano uwape haki za kichumi ili kumiliki, kutumia na kunufaika na ardhi, madini, bahari na rasilimali zote za ardhini na majini ili waendeshe maisha yao na wapunguze umaskini.

Mamlaka ya kusimamia Muungano itakayoundwa ihakikishe kuwa unajaa maslahi na wananchi si kuonekana kuwa ni chombo chenye matakwa au maoni ya kundi Fulani na kusababisha imani kuwa wanaonufaika ni upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano.

Watanzania Bara na Wazanzibari wangependa kuona nchi ikisonga mbele kwa kuhakikisha kuwa hakuna mwenye dhamira ya kuvunja Muungano wala kuupinga kwa vile umedumu kwa zaidi ya  miaka 50 wakiukubali na kujivuna kuwa ni watoto wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kuwapo kwa mamlaka ya kusimamia Muungano kutaendeleza umoja na kuepusha hisia za kuujadili kwa itikadi za vyama kwa kuwa chombo hicho kitakachokuwapo kisheria na katiba ndicho kitakachotoa mwelekeo na uhalali wa kisiasa wa kuwapo kwa umoja huo unaoziweka pamoja Zanzibar na Tanzania Bara.

Habari Kubwa