Nidhamu ya kliniki, kujifungua nyumbani shida kuu Shinyanga

14Nov 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Nidhamu ya kliniki, kujifungua nyumbani shida kuu Shinyanga
  • Mitishamba yapasua vizazi, muuaji mkuu
  • Hospitali Kahama imeelemewa majirani
  • Wagonjwa 1000 kwa siku; Tabora, Geita
  • Upanuzi bn 3.2/-; zahanati mpya kibao

UTUMIAJI mitishamba kwa wajawazito hasa walioko katika maeneo mbali na huduma rasmi, pindi wanaponuia kutibu ugonjwa kama wa minyoo katika kipindi cha ujauzito, unasababisha kupasuka mfuko wa uzazi na kuvuja damu nyingi, inayompotezea maisha mtoto na hata mama yake.

Mwandishi wa gazeti hili akizungumza na Mratibu wa huduma ya uzazi na mtoto kutoka Halmashauri ya Mji wa Kahama, Caroline Maliseli, ofisini kwake. PICHA: MPIGA PICHA WETU.

Wengi wamekuwa wakitumia dawa hizo katika dhana ya ‘kuongeza uchungu’ wakati anapokaribia siku ya kujifungua, lakini kuna madhara nayo kwa mtoto tumboni. Dawa hizo ni kali na inamsababishia mtoto kupoteza maisha kabla ya kuzaliwa.

Mjamzito anapotumia dawa aina yoyote bila ya kuruhusiwa na daktari, ni tendo la kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Kuna dawa mjamzito anaweza kuzitumia katika kipindi chake, hasa pale anapofika kiliniki na kupewa ushauri na uangalizi wa kitalaamu.

Pia, kuna wengine wamepoteza maisha kutokana na uamuzi wa kujifungua nyumbani na anahudumiwa katika mchakato huo na mtu ambaye sio mtalaamu.

Daima anaishia kuvuja damu nyingi na wakati mwingine mtoto anayezaliwa anakunywa maji ya mama machafu na kuishia kupoteza maisha.

Mwanamke mjamzito anapozalishwa na mtu asiye mtalaamu, huambukizwa ugonjwa kupitia bakteria (Puerperal Sepsis), unaosababishwa na kushikwa na mtu huyo anayemzalisha.

Hata hivyo, ni ugonjwa unaotibika, endapo mama huyo anawahi kufika hospitalini kwa matibabu dhidi ya madhara hayo.

Kutokana na vifo vya wajazito na watoto kuongezeka kila mwaka, serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Afya (MMAM), imechukua jukumu la kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali nchi nzima, lengo ni kusogezea huduma walipo wananchi, waondokewe na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kujifungua.

MITI SHAMBA

Caroline Maliseli ni Mratibu wa huduma ya uzazi na mtoto kutoka Halmashauri ya Mji Kahama, anasema matumizi ya dawa za miti shamba kwa kinamama wajawazito wanapotibu ugonjwa wa minyoo husababisha kupasuka kwa mfuko wa uzazi na kuvuja damu nyingi.

Anasema, wajawazito wengi wanapoteza maisha na watoto wao, wanapotumia dawa hizo, kwa lengo la kuongeza uchungu wakati anapokaribia muda wa kujifungua na kusababaisha mfuko wa uzazi kupasuka, mtoto anakunywa maji machafu.

“Dawa za miti shamba ambazo zinatumiwa na baadhi ya kinamama wajawazito kutibu minyoo au kuongeza uchungu ni kali sana na hazifai kuendelea kutumiwa. Zinafanya mfuko wa uzazi kupasuka haraka sana na mtoto kunywa maji machafu tumboni,” anaeleza.

Maliseli anasema, kinamama wengi Kahama wanajifungulia majumbani na kuhudumiwa na mtu ambaye si mtalaamu rasmi wa utabibu na baadaye wanapata maambukizi kupitia bakteria yanayosababishwa na kushikwa na kumfunga mtoto kitovu vibaya.

“Mwaka jana kuna mama aliletwa hospitalini akiwa tayari mkono wa mtoto umekatika…ulikatika wakati akijifungua na mtoto kutanguliza mkono ukavutwa na mtu aliyekuwa akimzalisha ambaye hana ujuzi wowote wa kitabibu,” anasema Maliseli.

”Tulimfanyia oparesheni na kumtoa mtoto akiwa ameshafia tumboni na mama huyo alipona, japo alipata maambukizi ya bakteria (Puerperal Sepsis) baada ya kushikwa na asiye na utalaamu.

VIFO KAHAMA MJI

Maliseli anasema hali ya vifo vya kinamama wajazito na watoto, kwa sasa imepungua tangu mwaka 2017, kutoka vifo vya wajawazito 18 hadi wanane mwaka huu, kati ya Januari na Oktoba.

Anarejea takwimu za vifo mwaka 2015, vifo wajawazitio 16; watoto wachanga 312; chini ya mwaka mmoja 461; na chini ya miaka mitano vilikuwa 840, huku vizazi hai vikiwa 11,142.

Pia, anasema mwaka 2016 vifo vya kinamama vilikuwa 23; watoto wachanga 463; wenye umri chini ya mwaka mmoja, 121 na chini ya miaka mitano vilikuwa 298; huku vizazi hai vilikuwa 12,062.

Maliseli anaendelea kusema kuwa, mwaka 2017 vifo vya akinamama vilikuwa 18, watoto wachanga vilikuwa 334, watoto chini ya mwaka mmoja vilikuwa 213 na watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 483 na vizazi hai vilikuwa 13,047.

Vilevile anasema, mwaka 2018 vifo vya akinamama vilikuwa 15, watoto wachanga vilikuwa 309, watoto chini ya mwaka mmoja vilikuwa 178 na watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 236 na vizazi hai vilikuwa 18,360.

Aidha, Maliseli anasema huu kati ya Januari na mwezi uliopita, kulikuwapo vifo vya kinamama wanane; watoto wachanga 281; chini ya mwaka mmoja 35; na watoto chini ya miaka mitano 189; na vizazi hai vilikuwa 16,320.

WAUME NA KLINIKI

Maliseli anasema, bado kinababa kwenye familia wana uelewa mdogo kutoshiriki kliniki na wake zao na wanashindwa kuzitambua changamoto au dalili mbaya zinazoweza kutokea wakati wa ujauzito na namna ya kukabiliana nazo.

Analalamika, asilimia kubwa ya wajawazito wanahudhuria kliniki wenyewe bila ya waume zao, hali inayotoa changamoto wakati wa kuwahudumia, hasa wakati wa upimaji wa virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Vilevile, anasema wajawazito kutoka katika Halmashauri za Msalala na Ushetu, wana kawaida ya kuchelewa kuanza kliniki na hufika katika vituo vya afya kujifungua, bila ya hata ya kadi inayoonyesha maendeleo ya mtoto kabla ya kujifungua.

Pia, anasema, vituo vya afya vya Halmashauri za Msalala, Ushetu, Nzega, Tabora Ishishimula, ni kawaida kinamama kuchelewa kuwahudumia wajawazito na wanawaleta katika Hospitali ya Mji wa Kahama wakiwa na hali mbaya.

SHIDA WAHUDUMIAJI

Maliseli anasema, upungufu wa watoa huduma kwenye wodi ya wajazito na watoto, pia inachangia kuongezeka vifo na anaiomba serikali kuongeza watoa huduma katika eneo hilo.

Anasema, katika Hospitali ya Mji wa Kahama, wajawazito wanaojifungua ni wengi, kila siku kuna watoto 45 hadi 60 na kuwapa wakati mgumu watoa huduma kushindwa kutoa huduma kutekeleza majukumo yao.

Maliseli anasema, ili kutokomeza vifo vya kinamama wajawazito na watoto ni kuacha tabia ya kujifungulia majumbani na kuanza kliniki mapema hasa pale unapojihisi mjauzito na kujifungulia katika vituo vya afya.

Anasema kuna baadhi ya kata za Halmashauri ya Mji Kahama, imekuwa kawaida matukio ya kinamama wajawazito hujifungulia majumbani na kuhatarisha usalama wa maisha yao na mtoto.

Maliseli anazitaja kata hizo ni: Malunga, Nyihogo na Mhungula. Inaelezwa wanafika hospitalini wakiwa hawajapatiwa chanjo na watoto wao, hawana kadi za kiliniki, wengine ni siku chache kujifungua.

MKURUGENZI MJI

Anderson Msumba ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, anasema katika kupambana na vifo hivyo, wamejenga vituo viwili vya afya; Iyenze na Mwendakulima na zahanati 13 katika maeneo yaliyo pembezoni mwa mji, lengo ni kuwasogezea huduma wananchi waliko.

Pia, anasema wanatarajia kujenga zahanati katika kata za Nyasubi, Chapulwa na Ngulu zitakazokuwa na huduma ya mama na mtoto na kuwataka wagonjwa kuanza kupatiwa huduma ngazi ya zahanati na kituo cha afya, kabla ya hawajafika wilayani.

Msumba anasema, Hospitali ya Wilaya ya Ushetu itakapokamilika, itasaidia kupunguza wimbi la wagonjwa wanaotoka katika Halmashauri za Urambo na Kaliua mkoani Tabora, kwani watapatiwa huduma mahali hapo.

Aidha, anafafanua lengo la ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ni kuwaondolea adha wajawazito kutembea umbali mrefu kuifuata hospitali ya wilaya na wakati huo huo, inapunguza msongamano wa wagonjwa, ambao kwa siku Hospitali ya Mji Kahama, inahudumia wagonjwa 800 hadi 1000.

OPD YAELEMEWA

Msumba anasema, kwa sasa wanajenga jengo la kupumzikia wagonjwa wa nje (OPD) linalogharimu kiasi cha Sh. bilioni 3.2, ni fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri na inatarajia kukamilka Februari mwakani, kwa kumhudumia mama na mtoto.

Anasema, Hospitali ya Mji wa Kahama inahudumia wagonjwa kutoka Halmashauri za Msalala, Ushetu, Mbogwe, Shinyanga Vijijini, Geita, Nyang’wale, Samuye, Urambo na Kaliua mkoani Tabora na mkoa Geita, hali inayosababisha msongamano mkubwa.

“Mazingira yaliyopo sio mazuri, wagonjwa wanalundikana, hakuna nafasi na endapo mvua ikinyesha wagonjwa wanaosubiria huduma wanaweza kunyeshewa. Hii ndio imetusukuma kujenga jengo jipya la kupumzika wagonjwa wa nje,” anasema Msumba

Vilevile Msumba, anafafanua kuna wakati wodi ya watoto wadogo, wanalazimika kulala watatu hadi wanne kwenye kitanda kimoja na wagonjwa wanapopungua, hulala wawili.

Mtazamo mkuu unaosimama ni kwamba, ili kutokomeza vifo vya kinamama na watoto, ni vyema wajawazito kujifungua katika vituo vya kutoa huduma, kuhudhuria kliniki, hasa mtu anapojihisi mjamzito na kuacha kutumia dawa za kienyeji kutibu magonjwa mbalimbali, hasa kwa mjamzito.

Habari Kubwa