Nigeria ilivyofufua uhusiano na taifa la Afrika Kusini

09Oct 2019
Mashaka Mgeta
Dar es Salaam
Nipashe
Nigeria ilivyofufua uhusiano na taifa la Afrika Kusini

OKTOBA 3, mwaka huu, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amekuwa kiongozi wa kwanza wa Nigeria kuzuru Afrika Kusini katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa (kushoto) akiteta neno na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, wakati rais huyo alipofanya ziara nchini Afrika Kusini. PICHA: MTANDAO

Ziara hiyo ilifanyika takribani mwezi mmoja baada ya raia wake kuwa miongoni mwa walioathirika kwa vurugu, uporaji na uharibifu mali za raia wa kigeni.

Buhari alifanya ziara ya kiserikali huku kukiwa na kumbukumbu za namna nchi mbili hizo zilivyoingia katika mzozo na ‘vita ya maneno’ kiasi cha kutishia uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati yao.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akampokea Rais Buhari huku kukiwa na kumbukumbu zinazohusu raia kadhaa wa kigeni kuuawa kikatili na baadhi ya wananchi wa Afrika Kusini.

Hakuna kiongozi kutoka Nigeria aliyefanya ziara rasmi nchini Afrika Kusini, kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Peter Fabricius wa taasisi inayotathmini masuala ya usalama jijini Pretoria, amekaririwa akisema uhusiano kati ya Afrika Kusini na Nigeria, sio mzuri kabisa ingawa marais hao wawili wanahusiana kwa namna inayofaa.

Kwa mujibu wa Fabricius, uhusiano wa nchi mbili hizo zenye uchumi mkubwa barani Afrika, unakabiliwa na ukinzani wa muda mrefu.

Kabla ya ziara hiyo, Serikali ya Nigeria ikatangaza kuwa Rais Buhari na mwenyeji wake Rais Ramaphosa watajadili usalama wa raia wa Nigeria nchini Afrika Kusini wakati Nigeria ikiamini kuwa miongoni mwa maeneo yanayolengwa katika vurugu na machafuko dhidi ya raia wa kigeni ni yale yanayomilikiwa na wanigeria.

Nigeria iliishutumu Afrika Kusini kwa machafuko yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wa Taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi Kusini mwa Afrika, waliwashambulia, kuwapora, kuwajeruhi na kuwaua raia wa mataifa mengine ya Afrika wanaofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na biashara.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa kuwa chanzo cha vurugu hizo ni madai kuwa raia wa kigeni waliopo Afrika Kusini, wanachukua ajira na fursa za kiuchumi zilizowastahili wenyeji, hivyo kuwasababishia maisha magumu na kadhia nyinginezo.

Katikati ya machafuko hayo, Afrika Kusini ikazifunga ofisi za ubalozi wake nchini Nigeria huku kukiwa na ulipizanaji visasi wa Wanigeria kwa raia wa Afrika Kusini waliokuwa wamewekeza nchini humo hususani katika jiji la Lagos.

Lunga Ngqengelele, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, akawaambia waandishi wa habari kuwa hatua ya kuzifunga ofisi hizo ilitokana na kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya Wanigeria katika miji ya Abuja na Lagos.

Wakati hali ikizidi kuwa mbaya kwa mataifa hayo, Tanzania ambayo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ikaelezea kusikitishwa na mashambulizi hayo.

Hata hivyo, Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi, ikatangaza kuunga mkono karipio lililotolewa na Rais Ramaphosa kulaani mashambulizi hayo.

Profesa Kabudi akasema Tanzania inaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na Afrika Kusini, kama ilivyo kwa nchi nyingine barani Afrika na kwingineko duniani.

Lakini mvutano wa kidiplomasia ulipoongezeka kati ya Nigeria na Afrika Kusini, taifa hilo la Magharibi mwa Afrika likatangaza kususia Kongamano la Kiuchumi Duniani kuhusu Afrika lililofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Kongamano hilo lilitarajiwa kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo pamoja na viongozi wengine kadhaa wa Afrika.

Wakati Afrika Kusini ikizifunga ofisi zake hizo, Nigeria ikamuita nyumbani Balozi wake nchini Afrika kwa mazungumzo, kisha ikatangaza nia ya Rais Buhari kupeleka mjumbe kwa Rais Ramaphosa, kuelezea kusikitishwa kwake na mashambulizi hayo.

Kwa upande mwingine, Afrika Kusini ikaonekana kufifisha dhana ya uhusiano wake mbaya na Nigeria, ambapo kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Naledi Pandor, ikasema maofisa wa Nigeria na Afrika Kusini wamekuwa kwenye mawasiliano ya mara kwa mara wakijaribu kuituliza hali ya mambo.

Prisca Cornel, mmisionari mtawa aliyesomea masuala ya uhusiano wa kimataifa anasema ziara ya Rais Buhari nchini Afrika Kusini ilitoa tafsiri nyingi, miongoni mwa hizo ni kuirejesha hadhi ya raia wa nchi hiyo, walioonekana kuwa wakatili na wasiokuwa na upendo kwa Waafrika wenzao.

Cornel anasema machafuko ya Afrika Kusini yaliashiria mbegu ya chuki iliyopandwa kwa baadhi ya raia wake tangu nyakati za utawala wa makaburu, na hivyo kuonekana kwamba inaendelea hata baada ya kuondoka kwa watawala hao waliopingwa katika ukanda wa Afrika na kwingineko duniani.

“Unajua kwa historia, Afrika Kusini ina matukio mengi yenye taswira ya ukatili dhidi ya ubinadamu, hivyo hata matukio yaliyotokea, yaliendeleza hisia hizo na hivyo kuwafanya raia wake kuonekana kuwa tofauti na wengine,” anasema.

Cornel anasema hali ilivyo kwa nchi hiyo (Afrika Kusini) ilipaswa kufananishwa na Ujerumani kwa namna ilivyoathiriwa kwa ‘chembechembe’ zilizoachwa na utawala wa Adolf Hitler.

“Kwa hiyo Rais Buhari alipofanya ziara yake nchini humo, inaweza kuwa sehemu ya kuionyesha dunia kwamba pamoja na kuwa Nigeria iliingia katika mzozo mkubwa na Afrika Kusini, lakini bado nchi hiyo inapaswa kuheshimika na sehemu kubwa ya raia wake wanathamini utu wa binadamu,” anasema.

Kwa upande wake, Kasmir Masawe ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya ukuzaji uchumi wa kikanda anasema, Nigeria inatambua umuhimu wa Afrika Kusini katika mukhtadha wa ukuzaji uchumi na biashara kwa watu wake, hivyo ziara ya Rais Buhari ni moja ya ushawishi utakaofanikisha kujenga mazingira salama kwa raia wake nchini humo.

Anasema, hivi sasa Nigeria ni miongoni mwa nchi ambazo raia wake wameenea kwenye mataifa mengi ndani na nje ya Afrika, hivyo kinachofanyika kwa nchi hiyo iliyopo Magharibi mwa Afrika ni kuhakikisha yanakuwepo mazingira bora kwa watu wake.

“Hata kama vurugu zile zingedhibitiwa kwa haraka na vyombo vya dola na hivyo kujenga imani kwamba serikali ya Afrika Kusini ilichukizwa na hivyo kuchukua hatua, lakini bado serikali ya Nigeria inapaswa kuchukua hatua zenye kuwanufaisha raia wake wanaofanya kazi na biashara kwenye mataifa mengine ikiwamo Afrika Kusini,” anasema.

Habari Kubwa