Nini nafasi ya wanawake kutamba uchaguzi ujao?

09Oct 2019
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Nini nafasi ya wanawake kutamba uchaguzi ujao?
  • Profesa ‘m-mama’ ataja kilichoko
  • Wanga’aka dhana ‘hatupendani’
  • Safari ile ‘waliwafunika’ kinababa

UCHAGUZI wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mnamo Novemba 24 mwaka huu, kwa kushirikisha jumla ya halmashauri 185 nchini.

Mpiga kura wa kike akitimza haki yake. PICHA: MTANDAO.

Ni uchaguzi unaofanyika kupata viongozi katika nafasi za ngazi ya mitaa, wanawake wanatajwa kuwa wadau wakuu wa ushiriki.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wananchi katika mji mdogo wa Laela, Mkoa wa Rukwa, Rais Dk. John Magufuli, aliwasisitiza wananchi wajitokeze kujiandikisha utakapofika wakati na watumie fursa ya uchaguzi kuwapata viongozi wanaowafaa, vivyo hivyo kwa wanaowania uongozi wajitokeze.

Kimsingi, ndicho alichokihimza Waziri wa Ofisi ya Rais (Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa- Tamisemi), Suleiman Jaffo, kuwataka wananchi kujitiokezakatika uandikishaji

Mwaka mmoja kutoka sasa, nako kutakuwa kumetimu miaka mingine mitano ya uchaguzi mikuu kufanyika kumpata Rais, wabunge na madiwani.

Kinamama walipo

Katika makundi hayo ya kijamii na kisiasa, kinamama nao wanahimizwa kushiriki katika hilo, kuwania nafasi, pia kujitokeza kupiga kura na kuna baadhi ya vyama vya siasa vimeenda mbali kuliainisha hilo.

Mtaaluma wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bertha Koda, anasema mbali na changamoto zilizopo, wanawake hushiriki katika hatua anazoziorodhesha hizo jumla yake ziko nne.

Msomi huyo mwenye mzizi kutoka Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya UDSM, anazitaja kuwa: Kabla ya uchaguzi; wakati wa upigaji kura; kuhesabu; utoaji matokeo na baada ya uchaguzi.

Akiwasilisha mada kuhusu haki za wanawake katika mchakato wa uchaguzi kwa madiwani wanawake kutoka mikoa tofauti nchini, mwezeshaji huyo wa masuala ya kijinsia, Profesa Koda anasema takwimu zinabainisha asilimia 53 ya wapiga kura za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, zilikuwa za kinamama.

Anaieleza hatua ya awali ni kabla ya uchaguzi, ambako kuna hatua azozitaja kuwa ni: Uchambuzi na maboresho ya sheria, utayarishaji miongozo, ugawaji majimbo, uboreshaji daftari la wapiga kura na uandikishaji wapiga kura

Profesa Koda anasisitiza umuhimu alioutaja, pia kinamama kuwa sehemu ya maandalizi na kushiriki uchaguzi, ambao katika mchakato wake unaanza mapema, suala la jinsia linachukua nafasi kudai maboresho kisheria, maelekezo na miongozo.

Anasema, changamoto mojawapo kabla ya uchaguzi ni mazingira yasiyo rafiki ya kufikia vituo vya kujiandikisha, ambavyo havizingatii majukumu ya wanawake katika kaya.

Msomi huyo anasema tafiti zilizofanywa na mtandao, zilibaini hamasa kubwa waliyo nayo wanawake kutimiza haki yao kwenye uchaguzi, wengi wanakatishwa tamaa na foleni ndefu na umbali wa vituo vya kujiandikisha.

"Mfano tulibaini kuwa katika vituo hivi, wanawake hujitokeza kujiandikisha zaidi majira ya saa nne asubuhi hadi mchana, baada ya hapo huondoka kwenda kuendelea na majukumu katika kaya zao, vituo viwe jirani, tuzingatie usawa wa kijinsia, ili mwanamke huyu akichota maji, akishapikia familia yake arudi tena kujiandikisha," anasema Profesa. Koda.

Anafafanua kuwa elimu duni ya uraia kwa wapiga kura isiyozingatia mengi ya kijinsia, ikiwamo ukatili wa kijinsia kwenye kampeni, ni mambo yanayopaswa kukomeshwa.

Pia, mtaaluma huyo anafafanua kwamba katika michakato inayofuata hatua hiyo, kama vile upigaji na kuhesabu kura, pia kutangaza matokeo, itakwenda sawa baada ya maandalizi kabla ya uchaguzi kutekelezwa ipasavyo.

"Usalama wa wanawake wagombea wakati wa upigaji kura, wasimamizi wa zoezi la kupiga kura kuelimishwa namna ya kutambua matukio ya udhalilishaji ni muhimu, ni sehemu ya maandalizi kwa wanawake kuondolewa vikwazo kabla ya uchaguzi," anasema Profesa Koda.

Takwimu zikoje?

Katika hilo Profesa Koda anasema, ongezeko la asilimia 4.4 la wapiga kura wanawake kati ya asilimia 95 waliojiandikisha mwaka 2015, lilitokana na wadau wanawake kutambua kuwa kura zao ni turufu ya ushindi.

Anaeleza takwimu za Tume ya Uchaguzi (NEC), zilibaini ongezeko hilo, huku uchambuzi uliofanywa na Mtandao wa Wanawake na Uongozi kupitia Mfuko wa Wanawake (WFT), unabaini uchache wa viongozi wanawake kwenye ngazi za maamuzi licha ya kwamba ni wapiga kura wazuri.

"Tunaweza kutafsiri kuwa, ushiriki wa wanawake katika kupiga kura au mchakato wote, unatokana na wao kujitambua, kuelimishwa, kushirikishwa, lakini bado wanawake hawajaandaliwa au kuondolewa vikwazo kufikia uongozi," anasema Prof. Koda.

Mdau muhimu

Gema Akilimali ni kati ya washiriki waliochangia mada katika warsha hiyo, anasema uchache wa wanawake kwenye ngazi za maamuzi kunachelewesha kufikiwa kwa masuala ya kijinsia kikamilifu.

Anasema changamoto za huduma ya afya ya uzazi, maji safi na salama, hususan kwa maeneo yaliyo pembezoni, zinatokana na msukumo hafifu katika vipaumbele vya kijinsia na kupitishwa bajeti finyu.

"Anayefahamu maana halisi ya tatizo la upatikanaji wa maji umbali mrefu wa zaidi ya mita 400 ni mwanamke ambaye anaamka alfajiri kufuata maji, wanawake haohao ndio wachache kwenye uongozi, nani atawatetea," anasema Akilimali.

Diwani, Anna Mgella kutoka Kata ya Singisa, katika Manispaa ya Morogoro, anasema kuna dhana kutoka kwa baadhi ya wanawake kwamba ‘hawapendani’ jambo linokwamisha kujiamini na uthubutu kwa viongozi watarajiwa.

"Kauli kwamba wanawake ‘hatupendani’ si sahihi na dhana hii ifutwe. Ni vizuri kuwaandaa wanawake watarajiwa kwenye uongozi ili tuongezeke katika ngazi za maamuzi nchini na kufikia malengo," anasema Mgella.

Mkakati ulivyo

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Ngerengere, Kibena Nassoro, anasema mkakati wa wanawake ni kwamba ifikapo 2025, idadi ya wenyeviti kwenye halmashauri iongezeke.

Kibena ambaye pia ni mwenyekiti wa Wanawake wa Serikali za Mitaa (Wasemi), anasema wataendelea kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea na kushinda, bila kukata tamaa.

"Mimi ni miongoni mwa wanawake watano wenyeviti wa halmashauri nchini, kati halmashauri zote 180, hapa mtaona bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunafika ngazi za maamuzi hususan wenyeviti wa halmashauri ili kuhimiza masuala ya kijinsia kwenye jamii," anasema Kibena.

+ Mwandishi anatumikia Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB).

Habari Kubwa