Nyota wa5 wenye nafasi kubeba Ballon d'Or 2019

17Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Nyota wa5 wenye nafasi kubeba Ballon d'Or 2019

NYOTA wa Real Madrid, Luka Modric alivunja utawala wa muongo mmoja wa Ronaldo-Messi wa kutwaa tuzo ya Ballon d'Or mwaka jana.

Raia huyo wa Croatia alimaliza utawala huo wa wawili hao kwenye soka baada ya kuiongoza Croatia kumaliza nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

Ballon d’Or inabakia kuwa tuzo kubwa zaidi kwa mchezaji binafsi wa mpira wa miguu, anayotunukiwa mchezaji ambaye anatajwa kuwa ndiye bora zaidi duniani.

Wachezaji wengi wamekuwa na misimu ya kuvutia kama vile Kylian Mbappe, Sergio Aguero, Raheem Sterling, Lionel Messi, Mohamed Salah, Sadio Mane, Bernardo Silva, Cristiano Ronaldo, Virgil van Dijk, Eden Hazard na wengineo wengi.

Hapa tunawaangalia wachezaji watano ambao wana nafasi kubwa ya kuitwaa Ballon d'Or mwaka huu, twende pamoja...

5. Sadio Mane

Sadio Mane alikuwa na msimu mzuri zaidi kwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kiatu cha Dhahabu kwa kumaliza kama mmoja wa wafungaji bora kwenye Ligi Kuu ya England.

Mchezaji huyu wa kimataifa wa Senegal alifunga mabao 22 kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu na kuitwaa kwa pamoja tuzo hiyo pamoja na mchezaji mwenzake, Mohamed Salah na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal.

Mchezaji huyo, Mane mwenye umri wa miaka 27, alikuwa mmoja ya nguzo muhimu kwa Liverpool wakati ikitwaa taji la sita la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati akifunga mabao manne na kutoa pasi ya mwisho moja katika mechi 13 alizoichezea huku pia akisababisha penalti iliyozamishwa kimyani na Salah katika mechi ya fainali dhidi ya Tottenham.

Kiwango chake dhidi ya Bayern Munich kitabakia kuwa kwenye kumbukumbu baada ya ‘kumtesa’ golikipa Manuel Neuer kabla ya kufunga bao.

Mane alikuwa akiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya England, PFA, lakini ikachukuliwa na mchezaji mwenzake, Virgil van Dijk na sasa itakuwa nafasi nyingine wakati huu akiiongoza nchini yake kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika, (Afcon) 2019.

Senegal ipo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo na hilo linaweza kumsaidia mshambuliaji huyo wa Liverpool kuwa na nafasi ya kuitwaa tuzo hiyo mwaka huu.

4. Mohamed Salah

Mshambuliaji huyu wa Liverpool baada ya kuwa na msimu mzuri zaidi wa kwanza akiwa na 'Wekundu' hao, sasa umekuwa bora zaidi kwake. Mohamed Salah aliisaidia timu yake kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa na Real Madrid mwaka jana, na kumuacha akiondoka uwanjani na machozi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri msimu huu alifunga mabao 22 na kumfanya atwae kwa mara ya pili mfululizo tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwa ufungaji bora, akiitwaa sambamba na mchezaji wa Arsenal, Aubameyang na Mane ambao wote walifunga mabao 22.

Nyota huyo wa Liverpool alikuwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo mwaka jana, lakini alishika nafasi ya sita nyuma ya Lionel Messi aliyeshika nafasi ya tano.

Mchango wa Salah kwenye kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya pia unaweza kuchangia yeye kuibeba tuzo hiyo. Mabao yake matano kwenye ligi hiyo yalikuwa muhimu kuisaidia timu yake na muhimu zaidi alilolifunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya pili kwenye fainali dhidi ya Tottenham ambapo ‘alimtawanya’ golikipa Hugo Lloris.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ataiongoza nchi yake kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 yanayofanyika katika ardhi ya nyumbani kwake na hivyo kama akilibeba taji hilo ana nafasi kubwa ya kutwaa Ballon d’Or.

3. Cristiano Ronaldo

Cristiano Ronaldo alifanya maamuzi yake ya kuihama Real Madrid kwenda Juventus msimu uliopita.

Baada ya kuwa na mwanzo mgumu pale, Mreno huyo hatimaye akafunga mabao 21 katika mechi 31 alizowachezea Bianconeri hao kwenye Ligi Kuu ya Italia, Serie A. mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, alibeba taji la Ligi Kuu ya Italia, Scudetto, na akatwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka katika msimu wake wa kwanza nchini Italia.

Mfalme huyo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya alishindwa kuivusha Juve kwenye michuano hiyo. Ingawa 'Kibibi Kizee' hicho cha Turin kilimaliza kwenye hatua ya robo fainali, ilikuwa ngumu Ronaldo kulaumiwa. Kiwango cha Mreno huyo kwenye mchezo dhidi ya Atletico na dhidi ya Manchester United kilikuwa cha kuvutia. Dhidi ya Rojiblancos, kilipindua matokeo wakati akifunga mabao matatu ‘hat-trick’ na kuiwezesha Juve kutinga nane bora. Lakini licha ya kuonyesha kiwango cha juu, Juve iliondolewa na Ajax na mabao yake hayakutosha kuiokoa.

Nafasi ya Ronaldo kuitwaa tuzo hiyo sasa imeongezeka baada ya kutwaa Kombe la Ligi ya Mataifa ya Ulaya. Ureno walitwaa taji la ligi hiyo mpya kwa Mataifa ya Ulaya baada ya kuifunga Uholanzi bao 1-0.

2. Lionel Messi

Hii ni alama ya Barcelona. Lionel Messi kwenye orodha hii anashika nafasi ya pili kama inavyoonekana. Mchezaji huyu wa kimataifa wa Argentina alikuwa katikati ya msimu bora zaidi kwake na hivyo kuwa kwenye nafasi kubwa zaidi ya kuibeba tuzo hiyo mwaka huu.

Messi alifurahia wakati bora zaidi katika msimu huu, akifunga mabao 36 kwenye Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, katika mechi 29 alizoanza kwa miamba hao wa pale Catalunya na alitwaa tuzo ya mfungaji bora kwa ligi zote za Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo.

Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 31, pia alimaliza akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akifunga mabao 12. Kiwango chake dhidi ya Tottenham, Liverpool na Manchester United kilikuwa cha kuvutia zaidi.

Nyota huyu wa Barcelona nafasi ya kulitwaa taji la Ligi ya Mabingwa zilizimwa na Liverpool wakati walipofungwa pale kwenye dimba la Anfield mabao 4-0 na hivyo kutolewa hatua ya nusu fainali. Wakati huo huo, Barca wakifungwa na Valencia kwenye fainali ya Kombe la Mfalme ['Copa Del Rey'].

Matumaini ya Messi kunyanyua tuzo ya Ballon d'Or kwa mara ya sita sasa yamebakia kwa kiwango atakachokionyesha kwenye michuano ya mataifa ya Amerika Kusini, Copa America. Argentina inapewa nafasi ya pili kuwa na nafasi kubwa ya kulibeba taji hilo nyuma ya Brazil, na kama Messi akilibeba, hakutakuwa na wa kumzuia kuitwaa tuzo hiyo.

1. Virgil van Dijk

Baada ya Fabio Cannavaro kuitwaa tuzo hiyo mwaka 2006, Virgil van Dijk anaweza kuwa beki wa kwanza kushinda Ballon d'Or. Mholanzi huyu ana ndoto baada ya kuwasaidia 'Wekundu' hao kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakimaliza kusubiria kwa kipindi cha miaka 14.

Van Dijk alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu ya England, PFA, mbele ya Mane, Raheem Sterling, Sergio Aguero na Bernardo Silva baada ya kuimarisha vizuri safu ya ulinzi ya Liverpool.

Ukuta wa chuma wa Liverpool uliwasimamisha washambuliaji kama Aguero, Sterling, Messi na wachezaji wengine wengi ambao walishindwa kabisa kuipita ngome yao.

Kiwango cha Mholanzi huyo kwa kipindi cha msimu huu kimemsaidia golikipa wa Wekundu hao, Alisson Becker kuwa imara zaidi. Kiwango chake dhidi ya Tottenham kwenye fainali dhidi ya Barcelona katika mchezo wa pili, ndicho kinaweza kuwa bora zaidi kwenye michuano hiyo.

Mholanzi huyo pia aliiongoza nchini yake kwenye fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya, ambapo walipoteza dhidi ya Ureno walioshinda kwa bao 1-0.