Nyota wanaolipwa mishahara mikubwa EPL

26Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Nyota wanaolipwa mishahara mikubwa EPL

HARY Kane ameripotiwa kukubali dili la kulipwa mshahara wa pauni 400,000 kwa wiki na Manchester City baada ya mwenyekiti wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy kukubali yaishe na kumruhusu kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England, EPL.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa mara ya kwanza alidokeza mpango wake wa kutaka kuondoka Spurs Mei, mwaka huu, kabla ya kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya England kwa ajili ya michuano ya Euro 2020.

Ofa ya kwanza ya Man City ya pauni milioni 100 kwa ajili ya kumsajili Kane ilikataliwa na klabu hiyo ya London kaskazini, kwani Levy alitaka mchezaji huyo aende nje ya ligi hiyo.

Wachezaji wenzake na Kane kwenye kikosi cha England waliripotiwa kudai kwamba, mshambuliaji huyo anaweza kukataa kujiunga na kambi ya mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya na Tottenham ili kulazimisha kuondoka hapo Etihad.

Na sasa baada ya kushika nafasi ya pili kwenye michuano ya Euro 2020, Kane yupo tayari kujiunga na Man City.

Hata hivyo, kwa mujibu wa The Sun, hakuna haja tena kwa Kane kugomea mazoezi baada ya Tottenham kuamua kulegeza msimamo wao.

Imedaiwa kuwa fowadi huyo sasa anatarajia kukamilisha uhamisho wa kwenda katika kikosi hicho cha kocha, Pep Guardiola ambapo ada yake inatajwa kuwa ni pauni milioni 160.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Levy amemtaarifu Kane kuhusu kubadilisha kwa msimamo wake na kwamba sasa yupo tayari kumuachia aondoke.

Kane – ambaye alifunga mabao 23 na pasi za mabao 14 kwenye Ligi Kuu ya England msimu uliopita – anatarajia kusaini mkataba wa miaka minne au mitano na mabingwa hao wa EPL.

Mshindi huyo wa kiatu cha dhahabu kwenye michuano ya kombe la Dunia mwaka 2018, anatarajia kwenda kuziba pengo lililoachwa wazi na Sergio Aguero, ambaye alimaliza muda wake wa kukaa hapo kwa muongo mmoja na kujiunga na Barcelona kipindi hiki cha majira ya joto akiwa mchezaji huru.

Ingawa ripoti nyingine zinadai kwamba, taarifa hiyo ni uzushi, na kwamba Spurs haina mpango wa kumuachia nyota huyo, makala haya inaangalia wachezaji 8 ambao wanaolipwa mshahara wa juu za kwenye Ligi Kuu England.

Kama Kane atatua Man City maana yake yeye ndio atakuwa kinara wa wachezaji wanaongoza kwa mshahara mkubwa, lakini ngoja tuwaangalie hawa kwa sasa;

#8 Edinson Cavani – Manchester United

Huyu ni mshambuliaji wa Manchester United ambapo mshahara wake wa sasa analipwa pauni 210,000 kwa wiki na ameongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi kuwachezea mashetani wekundu hao.

#7 Anthony Martial – Manchester United

Mchezaji wa Manchester United anayecheza nafasi ya ushambuliaji, Martial yeye yupo nafasi ya tisa kwa wale wanaovuta mkwanja mrefu akiwa anachukua nyumbani pauni 250,000 kwa wiki.

#6Thomas Partey – Arsenal

Huyu ni kiungo wa kimataifa wa Ghana, Partey ambaye anakipiga pale Arsenal na mshahara wake ni pauni 250,000 kwa wiki.

#5 Pierre-Emerick Aubameyang – Arsenal

Mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya Gabon, Aubameyang analipwa kiasi cha pauni 250,000 kwa wiki na washikabunduki hao wa jiji la London.

#4 Paul Pogba – Manchester United

Kiungo wa Manchester United, Pogba ambaye inasemekana hana mpango wa kuendelea kuwachezea Mashetani Wekundu hao, analipwa mshahara wa pauni 290,000kwa wiki.

#3 Raheem Sterling – Manchester City

Winga wa Manchester City, Sterling ambaye huenda akaondoka klabuni hapo wakati huu wa dirisha la majira yahaya ya joto, analipwa pauni 300,000 kwa wiki.

#2 Kevin De Bruyne – Manchester City

Kiungo wa Manchester City, Bruyne ndiye anayeongoza kwa sasa kupokea mshahara mkubwa zaidi akiwa anachukua pauni 350,000 kwa wiki.

#1 David de Gea – Manchester United

Golikipa huyu wa Manchester United kwa sasa anachukua nyumbani kiasi cha pauni 375,000 kwa wiki.