Oktoba 28 mwananchi unaachaje kupiga kura?

16Sep 2020
Reubeni Lumbagala
Dar es Salaam
Nipashe
Oktoba 28 mwananchi unaachaje kupiga kura?

OKTOBA 28 ni siku ya uchaguzi mkuu ambayo wananchi waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura watapata fursa ya kuchagua viongozi kuanzia, rais, wabunge na madiwani ili kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo inayoanza Novemba 2020 hadi Oktoba 2025.

Mchakato wa uchaguzi ukiendelea katika moja ya vituo vya kukusanya na kuhesabu karatasi za kura. PICHA: MTANDAO.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, uchaguzi mkuu hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano.

Kwa hiyo kutokana na umuhimu wa uchaguzi katika kuleta maendeleo ya nchi wananchi wamekuwa wakielimishwa kuhusu umuhimu wa kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia, lakini wakitakiwa kwanza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, wanasikiliza sera za wagombea na hatimaye kupiga kura kwa wagombea wanaokidhi vigezo ili kushirikiana na wagombea hao katika jitihada za kujiletea maendeleo katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kwa muda mrefu, wadau wa kisiasa, viongozi wa dini na wananchi wamekuwa wakipendekeza mabadiliko ya siku ya kufanyika uchaguzi ambao kwa miaka mingi, umekuwa ukifanyika Jumapili.

Kuchagua viongozi siku hiyo kulikuwa kukiwakwamisha baadhi ya wananchi walioshindwa kuchagua viongozi kutokana na kushiriki ibada hasa kwa wapigakura Wakristo.

Kukipa heshima na umuhimu na kuhakikisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu lakini pia serikali kutambua na kuheshimu imani za dini za wananchi na mapendekezo yaliyokuwa yakitolewa na wadau mbalimbali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliitangaza Oktoba 28, 2020 ambayo itakuwa siku ya Jumatano kuwa ndiyo iliyotengwa kwa ajili ya kupiga kura.

Jumatano pia itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa ili kuondoa kikwazo kilichokuwa kikikwamisha wananchi kupiga kura.

Kufanyika kwa uchaguzi siku ya Jumatano na ambayo pia haitakuwa na kazi kunatoa nafasi kwa wafanyakazi kuwahi kwenye vyumba vya kupigia kura.

Hatua ya NEC kubadili ratiba na mazoea ya miongo kadhaa ya kupiga kura Jumapili inaonyesha namna ambavyo uchaguzi ambao ni mchakato wa kidemokrasia ulivyopewa heshima ya aina yake ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu. Ndiyo maana swali hili ni kwa kila mmoja unaachaje kupiga kura Oktoba 28, 2020?

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika uongozi wake alitaja mambo manne ambayo yanachangia nchi kupata maendeleo nayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Uongozi bora unapatikana kwa kuwa na uchaguzi wa kumchagua rais, mbunge, mwakilishi na diwani ili kuliongoza taifa katika kupata maendeleo hivyo wananchi wana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kupiga kura ili kupata viongozi bora.

Hawa ndiyo wanaohitaji ili pamoja na watu, ardhi na siasa safi Tanzania isongembele na kuondokana na maadui watatu ambao ujinga, umaskini na maradhi.

Kwa sasa Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati ni kazi ya uongozi bora na jitihada ya kuondoa umaskini, ujinga na maradhi na kulipandisha chati taifa.

Itakuwa ni jambo la kushangaza kama wananchi wanahitaji uongozi bora bila kushiriki kuwachagua kupitia sanduku la kura siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, 2020.

Njia pekee ya wananchi kupata viongozi bora na hatimaye kutamalaki kwa kazi wanayoitaka ni kuwapigia kura wagombea bora wenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko na ustawi wa wananchi badala ya kuendeleza siasa za kuchumia tumbo.

Uchaguzi Mkuu huu unatarajiwa kugharimu bilioni 331.7 ambazo zitagharamiwa na serikali kwa asilimia 100 katika kuandaa na kuendesha mchakato huo unaowahusu Watanzania wote.

Kwa mujibu wa NEC takribani wananchi milioni 29.2 wanatarajiwa kupiga kura za kuchagua madiwani, wawakilishi, wabunge na rais.

Bilioni 331.7 ni fedha zinazotolewa na serikali kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina kwa kuzingatia kifungu cha 122 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi. Hizi ni fedha nyingi ambazo wananchi wanapaswa kuzithamini kwa kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi bora.

Taarifa za NEC zinasema vituo 80,155 vya wapiga kura vimetengwa huku kituo kimoja kikitarajiwa kuhudumia wananchi 500.

Kero zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali kama vile ukosefu wa maji, upungufu wa vyumba vya madarasa, changamoto za nishati ya umeme, miundombinu mibovu na ukosefu wa masoko ya bidhaa zinaweza kutatuliwa wakiwapo viongozi bora wenye wito wa kuwatumikia wananchi na wapigakura wao.

Hivyo basi, ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi bora ni njia ya kuelekea kuzipatia ufumbuzi kero hizo. Lawama na malalamiko dhidi ya viongozi hazitasaidia kupata uongozi makini badala yake wananchi washiriki kupiga kura Oktoba 28 ili waweze kupata wa kuwaongoza wanaokidhi matakwa ya Watanzania.

Kutokana na Oktoba 28 kutengwa kuwa siku ya kitaifa, itashangaza kama wananchi watashindwa kuitumia fursa hiyo muhimu kuhakikisha kuwa wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua vongozi.

Wagombea wanaoendelea kujinadi kuomba kura kwa wananchi, wahakikishe kuwa agenda ya kutetea na kusimamia maslahi ya wananchi inakuwa ni namba moja. Watu wanataka maendeleo, hivyo bila kusimamia maslahi ya wananchi, maendeleo hayawezi kufikiwa.

Kila mwananchi aliyejiandikisha aweke ratiba zake ili Oktoba 28, aweze kushiriki zoezi muhimu la kupiga kura. Ikumbukwe kuwa uchaguzi mkuu unafanyika mara moja katika kipindi cha miaka mitano.

Kama huo ndiyo utaratibu kufanyika katikati ya Juma huku siku hiyo ikifanywa kuwa ya kitaifa na ya mapumziko, Watanzania wasipange kukosa kupiga kura ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lao.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Sekondari ya Mlali iliyoko Kongwa mkoani Dodoma.

Maoni: 0765-409249.

Habari Kubwa