Operesheni vyoo Kagera

16Jan 2020
Lilian Lugakingira
Misenyi
Nipashe
Operesheni vyoo Kagera
  • Mafanikio yaonekana, tatizo ubora
  • Halmashauri Bukoba yashika mkia
  • DC Afande awaanika wasio navyo
  • Umaskini & uelewa bado shida kuu
  • Kujisaidia porini ‘baibai’ taratibu

HIVI sasa kunasikika kila upande, kampeni na operesheni vyoo ndio dai muhimu la maendeleo na ustawi wa umma. Sehemu nyingi kuna kampeni kubwa, kama ilivyowahi kuripotiwa na Nipashe mkoani Shinyanga na wilaya zake.

Choo cha Zahanati ya Ishozi, Missenyi kilivyoathiriwa na tetemeko lililotokea mkoani Kagera.

Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, kuna jitihada zinaendelea kuhakikisha kaya zote wilayani humu zinakuwa na vyoo.

Nia ya msukumo huo ni kutaka kuepusha madhara yatokanayo na kutokuwa na vyoo, yakiwamo magonjwa ya mlipuko ambayo yanachangia udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

MRATIBU LISHE

Mratibu wa Lishe wa Wilaya hiyo Zainath Hassan, anasema kuwa Missenyi ina kaya 43,053 na kuwa hata kama kaya zote zina vyoo, vyoo bora ni 39,608 na visivyo bora ni 3,445.

Zainath anasema kwamba waliamua kupambana na kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo, kuepusha jamii kukumbwa na magonjwa ya kuharisha, kuhara damu, kipindupindu, minyoo ya tumbo, homa ya tumbo, magonjwa ya macho na polio.

Miongoni mwa jitihada wanazozifanya anasema ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa vyoo, kufanya mashindano na kutoa zawadi kwa waliofanya vizuri.

"Tunafanya mashindano ya kaya kwa kata na tunatoa zawadi kwa mshindi, kwa hiyo kata inayoshindwa awamu inayofuata inajitahidi kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo ili ishinde, pia tunatumia sheria ndogo za halmashauri kukabiliana na tatizo la vyoo," anasema.

Anasema, pamoja na mambo mengine pia ukosefu wa vyoo unaathiri afya za watoto, huku akifatanua: "Mfano kinyesi kuzagaa ovyo kinachafua mazingira, na mtoto kila anachookota anaweka mdomoni."

Zainath anawahimizwa kunawa mikono kila wanapotoka chooni na kuwasafisha watoto mikono kwa sabuni, ili kuepuka kula uchafu.

"Wasipofanya hivyo watoto watapata minyoo, wataharisha na lishe itapungua," anasema.

Jitihada zinazofanyika kwa lengo la kuhakikisha wanaepuka magonjwa ya mlipuko, Wilaya ya Missenyi ina watoto 710 wanaosumbuliwa na magonjwa yanayohofiwa kutokana na tatizo la vyoo.

Zainath anasema, wanaendelea na kampeni ya usafi wa mazingira katika vijiji 77 kwa kuhamasisha jamii kujenga vyoo bora na anasema: "Tutashindanisha vijiji kwa vijiji na kutoa zawadi kwa washindi, pia tutafanya ukaguzi na kutumia sheria ndogo za vijiji maana kila kijiji kina sheria zake."

Anataja jitihada nyingine kuwa ni kufanya mikutano ya kuhamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora, kuchukua hatua kali kwa watakaokaidi na kutoa vipindi katika redio kuhusu umuhimu wa kuwa na choo bora na namna ya kukitumia.

"World Vision watafanya mikutano na kutoa vyoo vya mfano 63 ambavyo watavigawa katika shule za msingi na Kituo cha Afya Bunazi," anasema Zainath.

MBINU KUU

Anasema, serikali kupitia mpango wa kampeni za kitaifa za usafi wa mazingira, inaendesha mashindano na halmashauri hiyo imeshika nafasi ya tatu kitaifa.

Zainath anataja baadhi ya njia wanazotumia kufikisha ujumbe kwa jamii ni mikutano, kutoa vyoo vya mfano, kufanya mashindano, kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara na kutumia vyombo vya habari.

Anataja changamoto zao ni ufinyu wa bajeti unaokwamisha baadhi ya miradi ya usafi wa mazingira kutotekelezwa na uwezo mdogo wa kiuchumi kwa baadhi ya wana kaya unaokwamisha ujenzi wa vyoo bora.

"Missenyi pia kuna tatizo la baadhi ya makazi kujaa maji na udongo, kichanga unaosababisha vyoo kubomoka, lakini pia kuna tatizo la baadhi ya wanajamii kuhama hasa wafugaji," anasema Zainath.

Kwa mujibu wa mratibu lishe huyo, mipango ya baadaye iliyopo katika kufanikisha ujenzi wa vyoo bora, ni kuboresha na kukarabati vyoo vya jumuiya, mfano katika vituo vya usafiri, akitaja baadhi maarufu, Mutukula na Soko la Bunazi.

Zainath anahidi wataendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, ili kuhakikisha elimu inawafikia walengwa ipasavyo.

"Kuna mipango ya muda mrefu ikiwamo kuhamasisha wananchi kutumia mabampa na vyoo vya ‘Smart Toilet’ ambavyo viko kama plastiki na ni rahisi kuvisafisha," anasema mratibu lishe huyo.

USHINDANI

Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, imepanda kutoka kuwa na asilimia 37 ya kaya zenye vyoo bora mwaka 2015 na kufikia asilimia 92 kwa mwaka 2019.

Anatoa wito kwa jamii kuendelea kutambua kuwa matumizi ya vyoo ni muhimu, maana yanaweza kuimarisha afya za umma na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri, lengo ni kuinua uchumi wa mwananchi na taifa kwa ujumla.

Nipashe ilitembelea kijiji cha Bugorora na kupata maoni ya wakazi na viongozi wao kuhusu umuhimu wa kutumia vyoo bora, mkazi mmojawapo, John Kalikawe wa kijiji hicho, anakiri zamani hakuona umuhimu wa choo, lakini baada ya elimu, sasa anazingatia.

"Kwa sasa nina choo hata kama si bora, lakini kinanisaidia kutunza mazingira na kuepuka kukumbwa na magonjwa ya mlipuko," anasema.

Anasema, zamani alipohitaji kujisaidia alichimba shimo shambani alilolifukia baada ya kutumia, hali iliyosababisha kinyesi kusambaa shambani, hasa msimu wa mvua.

"Nina mpango wa kujenga choo bora, naendelea kujituma ili nipate fedha kwa ajili ya kujenga choo hicho, maana nimekwishaona umuhimu wake baada ya kupata elimu kupitia kwa mwenyekiti na mhudumu wa afya ngazi ya jamii," anasema.

MHUDUMU AFYA

Odiro Adrian, mhudumu afya ngazi ya jamii katika kijiji cha Bugorora, anasema wanapotembelea kaya miongoni, mwa masuala wanayozingatia na kuyapa kipaumbele, ni kuweka uchafu mbali na watoto.

Anasema, uchafu ikiwamo kinyesi unapozagaa, kuna hatari mtoto anaweza kushika na kula au kuweka vidole vichafu mdomoni, endapo hatagundulika haraka na kusafishwa kwa sabuni.

Odiro anasema, kijijini Bugororoa hadi sasa wamepiga hatua, familia zote hadi mwaka huu zina vyoo, ingawa baadhi si bora, hali inayosababisha wakati wa mvua baadhi hutitia na kusababisha kinyesi kusombwa na maji, kisha kinazagaa ovyo.

"Hali hii inahatarisha afya za wananchi, hasa watoto. Kinachofanyika sasa ni kuendelea kutoa elimu, ili angalau wajenge vyoo imara kidogo ili kuepusha kutitia," anasema Odiro.

Anasema tatizo linalochangia baadhi ya wananchi kushindwa kujenga vyoo bora, ni hali ngumu kiuchumi na Odiro anfafanua:" Mwaka jana kulikuwa na kaya nne hazikuwa na vyoo kabisa, lakini kwa mwaka huu zimejenga vyoo hata kama si bora."

Pia, anasimulia ulipofayika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya, Kanali Denice Mwila, alizitaja hadharani kaya zisizo na vyoo na baada ya huo mkutano waliona aibu, walienda kujenga vyoo.

"Kuna familia nyingine utakuta wanaishi katika nyumba iliyojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi. Unawezaje kumwambia atafute matofali na mabati kujenga choo bora?" Anaeleza kwa kuacha tafakari ya kutafakari.

Anasema, watu wa namna hiyo huambiwa wajenge choo kulingana na uwezo wao, kwa kutumia mabanzi ambayo hutakiwa kuzibwa vizuri isiwepo nafasi ya wazi.

"Inabidi kuachwa tundu dogo kwa ajili ya kupitisha haja ambalo hushauriwa kutengeneza mfuniko, ili kutoruhusu wadudu kama inzi kuingia na kubeba uchafu na kuusambaza," anasema.

Odiro watu wanashauriwa kuweka kidumu chirizi na sabuni, ili wanapotoka chooni, wanawa mikono kwa sabuni na mtu asiposafisha mikono vizuri, anaposhika vyombo au kuandaa chakula cha mtoto, anaweza kumlisha uchafu na kuathiri afya yake.

Anasema kuwa baada ya elimu hiyo, watu wanatumiaji vyoo vya wastani, angalau kwa kutumia ‘mabampa’ ambayo yanauzwa kwa bei rahisi akitaja wastani wa Sh. 10,000.

MTENDAJI KIJIJI

Herman Clonery, ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bugorora, anayesema kijiji chake kina jumla ya kaya 568 na anafafanua:"Kaya 98 zina vyoo bora, kaya 470 hazina vyoo bora na hakuna kaya hata moja isiyo na choo."

Clonery anasema wanaendelea kufanya mikutano ya kuhamasisha wananchi, ili kuhakikisha kaya zote zinakuwa na choo bora.

"Kwa kushirikiana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wenyeviti wa vitongoji na viongozi wengine wa kijiji, huwa tunaweka mikakati na maazimio kupitia halmashauri ya kijiji, mfano kufanya ukaguzi na kupanga tarehe ya lini tupite kukagua," anasema.

Anasema muda waliopanga ukifika huwa wanaenda kukagua, pia kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutunza usafi wa mazingira, unaojumuisha vyoo na uchimbaji mashimo ya kuhifadhia uchafu.

Anasema kijiji cha Bugorora, hakina sheria za kuhifadhi mazingira, lakini kupitia mikutano wanayoifanya wanaweka maazimio yanayotumika kama sheria, kutekeleza yaliyoazimiwa.

"Kwa wanaokaidi wanawajibishwa kwa mujibu sheria ndogo za uhifadhi mazingira zilizotungwa na halmashauri," anasema Ofisa Mtendaji huyo.

OFISA AFYA

Nelson Rumbeli, Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, anasema asilimia 99.7 ya kaya zote 600,000 mkoani Kagera zina vyoo, na asilimia 0.3 tu ndizo hazina vyoo kabisa.

Rumbeli, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba inaongoza kwa uchache wa vyoo bora ambavyo ni asilimia 36 ya vyoo vyote, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo yenye asilimia 39.2 na Ngara, asilimia 47.2.

Aidha, anasema, Halmashauri zenye vyoo bora, Missenyi inaongoza kwa asilimia 92.4, ikifuatiwa na Manispaa ya Bukoba yenye asilimia 84.5 na Karagwe asilimia 74.3.

Rumbeli anasema, kuwapo vyoo bora katika kaya kimkoa ni wastani wa asilimia 58.9 na takwimu hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya kuanzia Julai hadi Septemba mwaka jana na lengo lililopo, ifikapo Juni 2020, mkoa unalenga kufikia asilimia 75 ya kaya zenye vyoo bora.

"Ili kufikia lengo hilo tunaendelea kuhamasisha jamii kupitia viongozi wa dini wa serikali na vyombo vya habari. Pia, tutafanya ukaguzi wa ‘nyumba kwa nyumba’ kwenye makazi ya watu na taasisi, ili kuhakikisha zinaboresha vyoo" anasema.

Anasema mkakati ni kufanyika ukaguzi kwa kufuata sheria ndogo za mamlaka za serikali za mitaa katika halmashauri husika.

"Wakati tunafanya ukaguzi tutaongozwa na Sheria ya Afya kwa Umma ya Mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2012," anasema.

Rumbeli anasema, hadi sasa serikali imetoa fedha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya uboreshaji vyoo na kuwezesha upatikanaji majisafi na salama, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Mkoani Kagera, kunaelezwa kaya zenye vyoo bora zimeongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2018 hadi asilimia 58.9 mwaka jana.

"Namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Katibu Tawala wa Mkoa, Profesa Faustine Kamuzora, wakuu wote wa wilaya na wakurugenzi, ambao kwa jitihada zao wamewezesha kuongezeka kwa kaya zenye vyoo," anasema.

Habari Kubwa