Pale serikali ilipoelekeza wadau nao wamefunguka

30Jun 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Pale serikali ilipoelekeza wadau nao wamefunguka

BAADA ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi mitatu ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, hatimaye wamerejea shuleni kuendelea na masomo.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.

Shule zilifunguliwa jana huku kukiwa na maelekezo maalum yaliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuhusu ulipaji ada ili asiwapo mwanafunzi atakayezuiwa kuanza masomo.

Wizara inaelekeza ada za shule zilipwe kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo na kwamba kusiwepo na nyongeza yoyote katika kiwango cha ada.

Katika sehemu ya maelekezo yake, wizara inataka wanafunzi wote wapelekwe shule kwa ajili ya kuendelea na masomo bila kikwazo chochote ili kukamilisha muhula na kusiwapo na nyongeza ya ada.

Aidha, wizara inasisitiza, wazazi wanapaswa kuzingatia kuwa kiwango cha ada kinakadiriwa kuzingatia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule, gharama ambazo ziliendelea kuwapo hata muda ambao shule zilikuwa zimefungwa, kama vile mishahara ya watumishi, ankara za umeme na maji na nyingine kadhaa.

Kutokana na maelekezo hayo ya serikali, baadhi ya wazazi wamekuwa na maoni tofauti walipozungumza na gazeti hili ambayo wanaamini yatakuwa na mchango wa kufanikisha watoto wao kusoma bila kuwapo malalamiko kwa pande zote mbili, yaani shule na wao.

Deogratius David ni mkazi wa Morogoro, ambaye anasema, hatua hiyo ya serikali imesaidia kuwaondoa hofu baadhi ya wazazi ambao walidhani huenda watoto wao wakasimamishwa masomo.

“Pamoja na hayo, kila mzazi ambaye hajamaliza kulipa ada ya mtoto wake, afanye juu chini akamilishe, siyo kukaa kimya eti kwa sababu serikali imesema kusiwe na kikwazo," anasema David.

Anaongeza kuwa ni kweli corona imeyumbisha uchumi wa watu wengi, lakini pia ni muhimu kutambua kwamba, mishahara ya walimu na watumishi wengine wa shule binafsi na mahitaji mengine ya shule yanategemea ada zinazotolewa na wazazi.

"Maoni yangu ndiyo hao kwamba, bado wazazi tutimize wajibu wa kulipa ada, kwani katika maisha tunategemeana, yaani walimu wanategemea ada zetu na sisi tunawategemea watufundushie watoto wetu," anasema.

Naye Maua Bakari wa jijini Dar es Salaam, anasema, hatua ya wizara kutoa maelekezo itasaidia wanafunzi kusoma bila usumbufu na pia wazazi watapata muda wa kuhangaikia ada kwa nafasi.

Anasema, tangu serikali kutangaza kufungua shule, wazazi na walezi kila mmoja amekuwa na lake la kusema, kutokana na kwamba uingizaji wa kipato unatofautiana.

"Siyo siri, corona imesababisha biashara au shughuli za baadhi ya watu zimeyumba, zikiwamo zangu ambazo ni biashara ndogo na ninasomesha mtoto wangu katika shule binafsi," anasema Maua.

Anafafanua kuwa wiki iliyopita, alihudhuria kwenye mkutano ulioitishwa na uongozi wa shule kuzungumzia maandalizi ya kufungua shule ikiwamo pia kujadili malipo ya ada hasa baada watoto kukaa nyumbani miezi mitatu.

"Baadhi ya wazazi nikiwamo mimi, tuliomba uongozi wa shule uturuhusu kulipa ada kidogo kidogo kila mwezi badala ya kulipa ada kwa mkupuo, kwa sababu hatuna kitu," anasema.

Anasema, walijibiwa kuwa maombi yao yatafikiriwa kuona kama kuna uwezekano wa kufanya hivyo, na kwamba tangu wakati huo hawakupewa majibu hadi shule zimefunguliwa.

"Ninashukuru kutoa maelekezo, ambayo ninaamini kwamba, kama yatazingatiwa, basi watoto wetu watasoma huku nasi tukijitahidi kutafuta ada na kuhakikisha tunalipa kwa wakati,"anasema.

Kwa upande wake mkazi mwingine wa jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Pendo Ngaka anasema, mtoto wake anasoma darasa la kwanza na amepewa maelekezo kulipa kwa miezi yote mitatu ambayo alikuwa likizo.

"Maelekezo hayo yamenishangaza sana, kwani mtoto alikuwa hatumiwi kazi za nyumbani, sasa nitalipaji Sh. 300,000 wakati wakijua wazi kwamba hawakutoa kazi? Anahoji Pendo.

Anasema, kama walimu wa shule hiyo wamesikia maelekezo ya serikali na kuyazingatia, ana uhakika mtoto wake hatasumbuliwa na badala yake ataachwa aungane na wenzake kuendelea na masomo.

Mbali na hao, mzazi mwingine aliyezungumza na gazeti hili ni Jackson Nackson, ambaye anasema, mtu anapopeleka mtoto wake katika shule binafsi huwa ana uwezo wa kumudu gharama.

Hivyo, anaamini kila mzazi anayesomesha mtoto katika shule binafsi atamlipia ada, ila miezi yote mitatu ambayo watoto walikuwa nyumbani isihesabiwe na badala yake malipo ya ada yaanzie Julai.

"Lakini nisionekane kama niwaumiza wazazi wenzangu wanaosomesha watoto wao katika shule binafsi, bali nieleweke kuwa lengo langu ni kuwahimiza wasilalamike sana,"anasema Nackson.

Aidha, Nackson anawashauri wamiliki wa shule binafsi kutolazimisha wazazi kulipa ada kwa mkupuo, badala yake wawape nafasi na kupokea kile kidogo ambacho wazazi wanakipata ili wawe na nguvu ya kutafuta zaidi.

"Kwa nini ninashauri hivyo? Nina jirani yangu nilimsikia analalamika kwamba shuleni kwa mtoto wake wameambiwa walipe ada ya miezi sita kwa mkupuo badala ya mitatu wanalipa," anasema.

Anasema, shule zikisimamia hilo, zinaweza kusababisha baadhi ya watoto kubaki nyumbani kama serikali haitafuatilia maelekezo ambayo imeyatoa kwa wamiliki wa shule binafsi na kwa wazazi.

"Kutokana na mkanganyiko huo, ni vyema baada ya shule kufunguliwa, serikali izifuatilie ili kuona na kujua nini kinaendelea, ili kama kutakuwa bado kuna malalamiko, basi hatua za kuyatatua zichukuliwe," anasema.

Mkazi huyo wa jijini Dar es Salaam anasema, anaamini kwamba kila upande ukitumiza wajibu, watoto watasoma bila kuwapo malalamiko kutoka kwa wazazi, walezi na wamiliki wa shule.

Habari Kubwa