Patrick Kahemele: Chini yangu, Simba itafika mbali

27Jun 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Patrick Kahemele: Chini yangu, Simba itafika mbali

SIMBA imemaliza utata wa kukaa muda mrefu bila kuwa na katibu mkuu. Kwa zaidi ya mwaka, klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi haikuwa na mtendaji mkuu kabla ya kuweka mambo sawa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kama timu nyingine zinazoahiriki Ligi Kuu ya Soka Bara, Simba ililazimika kuajiri mtendaji ili kwenda sawa na kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mbali na kuajiri katibu mkuu, kanuni hizo za shirikisho hilo zinazitaka klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara pia kuajiri Mkurugenzi wa Fedha, Ofisa Habari na kiwanja maalumu cha kufanyia mazoezi.

Patrick Kahemele, meneja na mratibu wa zamani wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara 2013/14, Azam FC ndiye aliyepewa rungu la kuwa mtendaji Mtaa wa Msimbazi.

Kahemele amerithi mikoba ya Enock Kiguha aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya Evodius Mtawala na Ezekiel Kamwaga kuachia ngazi.

Kahemele aliliambia gazeti hili kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili na anayafahamu vizuri majukumu yake na hana wasiwasi na ajira yake hiyo mpya Simba.

Katibu huyo alisema ametua Msimbazi, huku akifahamu wazi klabu hiyo ina kiu ya vikombe baada ya kukaa nje bila ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa misimu minne mfululizo.

Alisema katika kuhakikisha Simba inafanya vizuri msimu ujao wa Ligi ya Bara, atahakikisha usajili wa klabu hiyo unafanyika vizuri na maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuanza kwa msimu.

"Nimeshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba, nitaanza kazi rasmi Julai Mosi, naamini kila kitu kitaenda vizuri," Kahemele alisema hayo Ijumaa iliyopita.

Aliongeza kuwa chini ya uongozi wake kwa kushirikiana na viongozi wa klabu hiyo, atahakikisha Simba inajiendesha kwa kujitegemea.

"Klabu inahitaji kujipanga na kuwa na uwezo wa kujitegemea, inawezekana na nitakuwa na mipango ya muda mfupi na muda mrefu," alisema Kahemele.

KUTOKA AZAM KUJA SIMBA
Kahemele anasema hana wasiwasi na wanachama na mashabiki wa Simba ambao ni wengi tofauti na timu ya Azam FC, ambao aliwahi kuitumikia.

Katibu huyo alieleza kuwa wanachama wa Simba ni wastaarabu, hivyo anaamini atapata ushirikiano ili kuipa klabu hiyo mafanikio.

Alisema chini ya uongozi wake atajipanga kushirikiana nao ili furaha waliyoikosa kwa misimu minne na heshima iliyopotea hapa nchini iweze kurejea hapa Tanzania.

APEWA USHAURI
Ezekiel Kamwaga, Katibu Mkuu aliyefanya kazi chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage, amemtaka Kahemele kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye ajira yake hiyo mpya.

Kamwaga alitaja moja ya changamoto alizokumbana nazo ni kufanya uamuzi wa kuridhisha viongozi wenye nguvu ndani ya klabu hiyo.

Kadhalika alimtaka kuwa tayari kuitumikia katika mazingira magumu kama ya kuchelewa kulipwa mishahara.

Kahemele anatajwa kuwa ndiye aliyefanikisha Mcameroon Joseph Omog kutua Azam na kuipa ubingwa wa Bara. Omog anatajwa kufanya mazungumzo na Simba na wakati wowote anatarajiwa kuwasili nchini kuanza kazi.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa