Pius Msekwa aeleza misumari ya siri iliyoshikilia Muungano-3

03Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Pius Msekwa aeleza misumari ya siri iliyoshikilia Muungano-3

MZEE Pius Msekwa (84), ni miongoni mwa wakongwe waliobeba wasifu mkubwa katika kulitumikia taifa, ikiwamo kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),-

-pia ni mshauri muhimu wa serikali na chama (TANU na CCM) kwa mengi.

Vilevile, Mzee Msekwa ana sifa nyingine ya kipekee, kuwa mdau anayefahamu fika picha kamili ya dhana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao mzizi wake kwa hatua, wengi hawaufahamu kwa kina kutokana na umri na si yote yaliyokuwa bayana.

Ili kuliweka hilo wazi kwa kina tangu vuguvugu la kuundwa Muungano huo, ameamua kuandika kitabu alichokizindua siku chache zilizopita, kiitwacho Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kinachoweka undani wa historia kwa hatua. Gazeti hili limeamua kuchapisha maudhui yake kwa hatua, kila siku kama ya leo katika jarida hili la Siasa.

Wiki iliyopita tuliwaletea sehemu ya pili ya mfululizo wa kitabu hiki ambapo tuliishia kipengele cha 2.2 Haja ya kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi hizi mbili. Sasa fuatilia kuanzia kipengere kinachofuata:

2.3. Kuimarisha udugu wa karibu uliokuwapo baina ya wananchi wa nchi hizo mbili

Tukirejea hotuba ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akiwahutubia wabunge wa Bunge la Tanganyika tarehe 25 Aprili 1964, alisema hivi:

“Tanganyika na Zanzibar ni nchi ndugu. Tunashirikiana kwa historia, lugha, mila tabia na siasa. Udugu wa Afro- Shirazi Party na TANU wote mnaufahamu. Udugu wa viongozi wa vyama hivi viwili haukuanza jana. Basi, tunazo sababu zote hizo za kutufanya tuungane na kuwa kitu kimoja. Juu ya yote hayo, kuna shauku ya Umoja wa Bara la Afrika. Basi, kwa kuzingatia yote hayo, mimi, kwa niaba yenu, na Rais Karume kwa niaba ya ndugu zetu wa Unguja na Pemba, tulikutana Unguja siku ya tarehe 22 mwezi huu, tukatia saini mkataba wa umoja baina ya nchi zetu mbili.

Mnao Mkataba huu na mtaujadili. Endapo bunge hili, pamoja na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, yataukubali mkataba huu, nchi zetu zitakuwa nchi moja. Siyo nia yangu kueleza Mkataba wenyewe. Mtaelezwa wakati wa majadiliano. Kazi yangu ni kuwaombeni muukubali Mkataba huu.”

Kutokana na maneno hayo ya Mwalimu Nyerere, tunaona wazi kwamba, kuimarisha udugu uliokuwapo baina ya wananchi wa Tanganyika na Zanzibar, lilikuwa ni lengo mojawapo katika malengo makuu ya kuanzishwa kwa Muungano huu.

3

SURA YA

MAZINGIRA YALIYOTAWALA UJIO WA MUUNGANO HUU

3.1 Mchakato ulivyokuwa hadi Kufikia Kusainiwa kwa Mkataba wa Muungano

kubwa la kuzingatia kuhusu mchakato huo, ni usiri mkubwa uliokuwapo katika mchakato wenyewe. Lakini, usiri huo ulikuwa na sababu nzuri.

3.2 Sababu za Usiri Uliogubika Mchakato huo

Sababu yake ya msingi ilikuwa ni hofu ya mchakato huo kuhujumiwa na maadui wa Muungano huu. Marais Julius Nyerere na Abeid Karume, wote wawili walikuwa na hofu kwamba, endapo lengo lao la kuunganisha nchi hizi mbili litajulikana mapema, maadui wa muungano huo watapata nafasi ya kufanya hujuma za kukwamisha lengo hilo lisifikiwe.

Na kweli, dalili za hujuma zilipata kujitokeza katika siku za mwishomwisho wa mchakato huo, ambapo ilitengenezwa fitina ya maneno ya uwongo yaliyosambazwa wakati Rais Karume alipokuja Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha mipango ya kusainiwa kwa Mkataba wa Muungano. Gazeti la “TANU The Nationalist” lilikuwapo nyakati hizo, lilifichua fitina hiyo katika toleo lake la tarehe 20/04/1964, kwa kuchapisha uvumi uliozagaa kwamba, ‘Rais Karume na familia yake wamekwenda kuishi Tanganyika.’

Ilibidi Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona akanushe uvumi huo kwa kusema kwamba, “Rais Karume alifika Dar es Salaam kuzungumza na Rais Nyerere na kwamba, mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha urafiki wa nchi hizi mbili, pamoja na uhusiano kati ya TANU na Afro – Shirazi Party.”

Waziri Kambona alinukuliwa na gazeti hilo akiendelea kusema kwamba, “Rais Karume anaamini katika Umoja wa Afrika, na Zanzibar itafurahi kuona Serikali ya Afrika hatimaye imeundwa, ambayo ndiyo vilevile ndoto ya Tanganyika.”

Lakini, kwa lengo la kutunza siri, Waziri Kambona alificha ukweli kwamba, mazungumzo ya Marais hao yalihusu kuunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, kwa lengo hilohilo la kutunza siri, hata siku yenyewe ya tarehe 22/04/1964 ambayo Rais Nyerere alikwenda Zanzibar kuweka saini yake katika Hati ya Mkataba wa Muungano, bado gazeti la The Nationalist lilieleza kwamba “Rais Nyerere alikwenda Zanzibar kwa ziara ya kirafiki katika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambako alionana na Rais Karume, ikiwa ni ziara yake ya kwanza Zanzibar tangu Serikali mpya ya Mapinduzi ilipotwaa madaraka.”

Gazeti hilo pia, lilinukuu maelezo ya Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, aliyesema kwamba, “tumemkaribisha Nyerere kuzuru Zanzibar kwa moyo mkunjufu, kwani watu wa nchi zetu hizi mbili wakati wote wamekuwa marafiki na wenye ukaribu mno. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba, ni jambo zuri kwa viongozi wetu wakuu kukutana mara kwa mara kujadili matatizo yetu yanayofanana. Hii ni ziara ya kwanza na nyeti ya Rais Nyerere tangu Mapinduzi.”

Hatimaye siri yenyewe ilikuja kufichuliwa jioni ya tarehe hiyo 22 Aprili, 1964, (baada ya Mkataba wa Muungano kuwa tayari umesainiwa). Siri ilifichuliwa kwa njia ya Taarifa rasmi ya Serikali, ambayo ilitolewa na Ikulu mjini Dar es Salaam, iliyotangaza kwamba:

“Rais Julius Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Abeid Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, leo wamesaini Mkataba wa Makubaliano (Articles of Union ) ya kuunda Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar. Makubaliano hayo ni sharti yaridhiwe na Serikali zote mbili, pamoja na Mabunge ya nchi zote mbili.”

Hata mazungumzo baina ya Rais wa Tanganyika na Rais wa Zanzibar juu ya suala hili, yalibaki kuwa na siri ya Waasisi hao wawili hadi walipofikia hatua ya kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Muungano, kutokana na sababu za msingi zilizoelezwa hapo juu.

Lakini, mchakato haukuishia hapo. Kwani, ili Mkataba huo upate uhalali wa kisheria, na kama ilivyokuwa imeelekezwa katika kifungu kidogo cha (viii) cha Mkataba huo; ilibidi uridhiwe (ratified) na vyombo vya uwakilishi vya nchi hizi mbili, ambavyo wakati huo vilikuwa ni Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar. Kama tulivyokwishakueleza, kazi hiyo ilitekelezwa ipasavyo na vyombo hivyo viwili siku ya Jumamosi tarehe 25 Aprili, 1964; ambapo Baraza la Mapinduzi la Zanzibar lilitangulia kwa kufanya kikao chake asubuhi ya siku hiyo, na Bunge la Tanganyika likafuatia kwa kikao kilichofanyika mchana wa siku hiyohiyo.

Mkataba huo haukuweka sharti lolote la kutaka uthibitishwe na wananchi wote kwa kura za maoni (referendum). Ndiyo sababu zoezi hilo halikufanyika.

3.3 Mazingira ya kuzaliwa kwa Muungano wenyewe

Kama nilivyokwishaeleza, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa tarehe 26 Aprili, 1964. Lakini, kuzaliwa kwake hakukuambatana na shamrashamra au sherehe za namna yoyote. Bila shaka, hii ilitokana na usiri mkubwa uliokuwapo wakati wote wa maandalizi yake, kwani hata yale mapatano yaliyosainiwa tarehe 22 Aprili, 1964, hayakutaja tarehe ya kuanzishwa rasmi kwa Muungano, bali yalisema tu kwamba, maisha ya Muungano huu yataanza rasmi” siku itakayofuata mara baada ya kuridhiwa kwake.” Kwahiyo basi, kwa kuwa taratibu za kuridhiwa kwake zilikamilika tarehe 25 Aprili,1964 , na maisha yake yakaanza rasmi siku iliyofuata , yaani, tarehe 26 Aprili 1964, hapakuwa na muda wa maandalizi ya kufanya sherehe zozote. Ndiyo sababu siku hiyo ilipita kimyakimya tu, bila kuwa na sherehe za aina yoyote za kuadhimisha kuzaliwa kwa Muungano huu. Na kama tulivyokwishakuona, shughuli zote zilizoambatana na tukio hilo, zilifanyika na kumalizikia ndani ya Bunge tu; yaani: Mkataba wa Mapatano ya Muungano ulidhiriwa siku ya Jumamosi tarehe 25 Aprili,1964. Kesho yake, Jumapili tarehe 26 Aprili, 1964, Jamhuri ya Muungano ikazaliwa rasmi, ikiwa ni pamoja na vyombo vipya vya utawala na uongozi wa Jamhuri hiyo mpya. Siku iliyofuata, yaani, Jumatatu tarehe 27 Aprili,1964, ilikuwa ndiyo siku ambapo Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano lilipoanza kazi, kwa kuapishwa kwa Wabunge wapya walioteuliwa na Rais kuiwakilisha Zanzibar katika Bunge hilo la Jamhuri ya Muungano; pamoja na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Mwalimu Nyerere, na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume, kubadilishana HATI zilizosainiwa na Mapatano ya kuanzishwa kwa Muungano huu. Lakini, nje ya Bunge, hapakuwa na sherehe nyingine zozote. Ndiyo sababu mimi binafsi, nikiwa Katibu wa Bunge wakati huo, nilibahatika kushuhudia matukio hayo makubwa, na ya kihistoria, yakitokea ndani ya ukumbi wa Bunge, Karimjee Hall, Dar es Salaam.

3.4 Madai kwamba Zanzibar haikuwahi kuridhia Mkataba wa Muungano

Katika Sura ya Tano, nitazungumzia kwa kina zaidi kuhusu suala la changamoto ambazo zimeukumba Muungano wetu katika nyakati mbalimbali za uhai wake. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba, licha ya changamoto hizo, Muungano wetu haujatetereka kiasi cha kutishia kuendelea kuwapo kwake. Miongoni mwa matatizo yaliyowahi kujitokeza kuhusu Muungano huu, ni madai ambayo yamekuwa yakiibuliwa na baadhi ya viongozi wa Zanzibar, waliopo na waliokwishakustaafu, kwamba, eti hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar liliridhia Mkataba huo wa Muungano.

Madai haya yanashangaza sana kwani, kama ilivyokwishaelezwa, ni kwamba, Kikao cha Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kilifanyika asubuhi ya tarehe 25 Aprili, 1964, kwa madhumuni hayo tu ya kuridhia Mkataba huo. Baadaye, sheria inayoitwa “The Union of Zanzibar and Tanganyika Law” ilichapishwa katika Gazeti la Serikali ya Muungano la tarehe 1 Mei 1964, kama Government Notice (GN) no. 243; ikiwa na maelezo kwamba, sheria hiyo ilipitishwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar tarehe 25 Aprili,1964.

Kwahiyo, kwa muda wote wa miaka zaidi ya hamsini iliyopita ya Muungano huu, tumechukulia sheria hiyo kuwa ni ushahidi tosha unaothibitisha kwamba, Baraza la Mapinduzi liliridhia Mkataba wa Muungano kwa kutipisha sheria hiyo.

3.5. Utengenezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano

Nchi yoyote inayotambulika hivyo, sharti iwe na Katiba yake. Ndiyo sababu kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na Katiba yake, na Zanzibar pia ilikuwa na Katiba yake, ambayo ilitungwa mara baada ya Mapinduzi ya Januari 1964 yaliyoondoa utawala wa Sultani uliokuwa umewekwa mwezi Desemba 1963, wakati Zanzibar ilipopata uhuru wake.

Baada ya kuunganisha nchi hizi mbili na kuunda nchi moja mpya, ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilibidi itungwe Katiba mpya ya nchi hiyo mpya. Utekelezaji wa kazi hiyo uliongozwa na Mkataba wa Makubaliano ya Muungano, uliokuwa umetoa maelekezo yafuatayo:

Kwamba, kuwe na kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kabla ya kutunga Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano.

Kwamba, katika kipindi hicho cha mpito, Jamhuri ya Muungano itatawaliwa na Katiba ya muda.

Kwamba, Katiba ya Tanganyika itakuwa ndiyo Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano, ikiwa imefanyiwa marekebisho ya kuwezesha kuwapo kwa;

Serikali ya Zanzibar, pamoja na Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar, kwa ajili ya kushughulikia mambo ya ndani ya Zanzibar ambayo siyo mambo ya Muungano;

Makamu wa Rais wawili, mmoja akiwa ni mshauri mkuu wa Rais kwa mambo yanayohusu Tanganyika na mwingine akiwa ni mshauri mkuu wa Rais kwa mambo yanayohusu Zanzibar.

Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano; na

Mambo yoyote mengine ambayo yataonekana kuwa yanafaa na yanahitajika kwa ajili ya uendeshaji bora wa Jamhuri ya Muungano.

3.6 Suala nyeti la ‘Serikali mbili’

Kifungu kidogo cha (iii)(a) cha Mkataba huu wa Makubaliano ya Muungano ndicho kilichoweka mfumo wa Serikali mbili, yaani, Serikali ya Muungano, na Serikali ya Zanzibar. Jambo hili lilikuja kuwekwa wazi zaidi na sheria inayoitwa “The Interim Constitution of the United Republic of Tangayika and Zanzibar, 1964” iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 1 Mei, 1964, kama Government Notice (GN) no. 246, ambapo, kifungu chake cha 4 kiliweka sharti kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na madaraka juu ya mambo ya Muungano katika Jamhuri nzima ya Muungano, yaani, upande wa Tanganyika na pia upande wa Zanzibar; na vilevile, juu ya mambo mengine yote yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika. Huu ndio unaitwa “Muundo wa Serikali mbili,” ambao baadaye uliingizwa kwenye Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipotungwa mnamo mwaka 1977; lakini, kama tutakavyoona baadaye katika Sura inayofuata, umesababisha mjadala usiokwisha hadi sasa.

3.7 Kipindi cha mpito chaongezwa

Kifungu kidogo cha (vii) cha Mkataba wa Makubaliano ya Muungano kilikuwa kileelekeza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, ndani ya kipindi hicho cha mpito cha mwaka mmoja kuwa;

atateua Tume ya Katiba itakayopewa jukumu la kuandaa mapendekezo ya Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano, na

ataitisha Bunge maalum la Katiba (Constituent Assembly), lenye wajumbe kutoka Tanganyika na wengine kutoka Zanzibar, kwa ajili ya kutunga Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano.

Wahenga walisema kwamba “mpango si matumizi” na kweli hivyo ndivyo ilivyotokea kuhusu jambo hili. Kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kilikuwa kinamalizika tarehe 26 Aprili, 1965. Lakini, tathmini ya Marais hao wawili ilibainisha kwamba ulihitajika muda zaidi wa kipindi cha mpito, kabla ya kufikia hatua ya kutunga Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano. Kwahiyo, mnamo mwezi Machi mwaka 1965, yaani, mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi hicho cha mpito, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha Sheria iliyoruhusu kuahirishwa kwa utekelezaji wa masharti yaliyotajwa katika kifungu kidogo cha (viii) cha Mkataba wa Makubaliano ya Muungano, “hadi wakati mwingine baadaye, ambao utaamuliwa na Marais hao, kama watakavyoona wenyewe kuwa inafaa.”

Kwahiyo, Jamhuri ya Muungano iliendelea kutawaliwa na Katiba ambayo awali ilikuwa ni Katiba ya Tanganyika, kama ilivyorekebishwa kulingana na maelekezo ya Mkataba wa Mapatano ya Muungano, na kama ilivyorekebishwa tena mwaka 1965, kwa kuifanya iwe ni Katiba ya Chama kimoja cha siasa, hadi kufikia mwaka 1977, ilipotungwa Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

ITAENDELEA