Pius Msekwa aeleza misumari ya siri iliyoshikilia Muungano-5

17Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Pius Msekwa aeleza misumari ya siri iliyoshikilia Muungano-5

MZEE Pius Msekwa (84), ni miongoni mwa wakongwe waliobeba wasifu mkubwa katika kulitumikia taifa, ikiwamo kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Katibu Mtendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), -

MZEE Pius Msekwa (84).

-pia mshauri muhimu wa serikali na chama (TANU na CCM) kwa mengi.

Pia, Mzee Msekwa ana sifa nyingine ya kipekee, kuwa mdau anayefahamu fika picha kamili ya dhana ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao mzizi wake kwa hatua, wengi hawaufahamu kwa kina kutokana na umri na si yote yaliyokuwa bayana.

Ili kuliweka hilo wazi kwa kina tangu vuguvugu na kuundwa Muungano huo, ameamua kuandika kitabu alichokizindua siku chache zilizopita, kiitwacho Historia YA Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kinachoweka undani wa historia kwa hatua. Gazeti hili limeamua kuchapisha maudhui yake kwa hatua, kila siku kama ya leo katika jarida hili la Siasa na leo hii tunaendelea kutokea tulipoishia wiki iliyopita. Endelea na sehemu hii ya tano ya kitabu hicho.

4.2.3 Sababu za kuwekwa kwa Kipindi cha Mpito

Sababu kubwa ya kutaka vifungu hivyo vitumike katika kipindi cha mpito tu ilikuwa ni kuwapo kwa hayo matumaini kwamba hadi kufikia wakati wa kutunga Katiba ya kudumu, ile hofu ya Zanzibar kumezwa itakuwa imeondoka, kwa hiyo, itawezekana kuwa na katiba ya serikali moja.

Tumekwishakuona kwamba, kipindi hicho cha mpito baadaye kiliongezwa kwa sheria ya Bunge iliyotungwa mwezi Machi 1965, ambayo iliondoa kikomo cha mwaka mmoja. Madhumuni ya kuondoa kikomo hicho yalikuwa ni kujipa muda zaidi ili kuwezesha Muungano kutengamaa zaidi, na faida zake kuonekana wazi zaidi; hali ambayo ilitegemewa kuwa ingesaidia kuondoa hofu hiyo ya Zanzibar kumezwa, na kwahiyo, kutuwezesha kurejea kwenye muundo wa serikali moja.

Lakini, hata hivyo, hatimaye Katiba ya kudumu ilitungwa mwaka 1977, (yaani, miaka 13 baadaye), kwa kuwa hofu hiyo ilikuwa bado haijaondoka, ilibidi Katiba ya Kudumu iendeleze muundo huu wa serikali mbili.

(a)Kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi

Hatua ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi mwaka 1977 pia, ilileta matumaini mapya kwa upande wa Mwalimu Nyerere, ya kwamba chama hiki kipya kingeweza kufanikisha upatikanaji wa muundo wa serikali moja. Matumaini haya mapya yalitokana na kutambua kwamba, Chama hiki kipya kilikuwa na madaraka kamili ya kufanya maamuzi makubwa yanayohusu pande zote mbili za Muungano. Hii inathibitishwa na kitabu chake kiitwacho “Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania” (Zimbabwe Publishing House). Mwalimu aliandika hivi:

“Muundo wa Muungano ni suala la sera, siyo amri ya Mungu. Vyama vya siasa mbalimbali vinaweza kuwa na maoni mbalimbali kuhusu muundo unaofaa wa Muungano…muundo wa serikali mbili ni Sera ya TANU na ASP, na kwa sasa CCM.

Lakini, Chama Cha Mapinduzi kikipenda kinaweza kubadili sera hiyo ya muundo wa serikali mbili…kinaweza kufanya hivyo kwa kuhisi kwamba, hivyo ndivyo wananchi wengi watakavyo, lakini pia kinaweza kufanya hivyo kwa sababu ya kuamini chenyewe kuwa inafaa kufanya hivyo, hata kama wananchi wengi hawakudai mabadiliko … Chama Cha Mapinduzi kitakapobadili sera yake ya muundo wa Muungano wa serikali mbili, sera yake mpya itakuwa ni muundo wa Muungano wa serikali moja.”

4.3 Mwisho wa matumaini ya kupata serikali moja

Hata hivyo, matumaini hayo vilevile hayakufanikiwa kutimizwa, kwani siyo tu kwamba hofu ya Zanzibar kumezwa na Tanganyika ilikuwa bado ipo, lakini, pia, ilikuwa imeongezeka na kupata nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Ndiyo maana Utawala wa Rais Aboud Jumbe ulianzisha madai ya muundo wa serikali tatu.

Ripoti ya Tume ya Warioba inaeleza kwamba, kumekuwapo na malalamiko kutoka Zanzibar yanayodai kwamba, “Tanganyika imevaa koti la Muungano.” Madai hayo yalianza kujitokeza wakati huo, yakifuatiwa na madai mengine ya kudai “usawa wa nchi zetu mbili zilizoungana.”

Bila shaka ni katika jitihada za kutafuta huo usawa wa nchi mbili zilizoungana, ndipo Rais Aboud Jumbe alipoibua mkakati wa kutengeneza Katiba mpya ya serikali tatu mnamo mwaka 1983. Lengo lake lilikuwa ni kuirejesha Serikali ya Tanganyika ambayo ilidhaniwa kuwa imejificha kwenye koti la Muungano. Juhudi hizo za Rais Aboud Jumbe zitaelezwa baadaye.

Huo ndio ulikuwa mwisho kabisa wa matumaini yaliyokuwapo ya kupata muundo wa serikali moja. Badala yake, sasa zikaanza juhudi kubwa za kudai muundo wa serikali tatu.

Tutarejea kuzungumzia juhudi hizo katika Sura ya Sita. Ushahidi unathibitisha kuwa matumaini ya kuwa na muundo wa serikali moja hayapo tena, upo katika takwimu za Tume ya Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano, ambapo inaonesha wazi kwamba, kwa upande wa Tanzania Bara, katika jumla ya maoni 684,303 yaliyopokelewa, ni maoni 3,564, au asilimia 0.5 tu, ndiyo yaliyopendekeza muundo wa serikali moja.

Na kwa upande wa Zanzibar, katika jumla ya maoni 49,671 yaliyopokelewa, ni maoni 25, au asilimia 0.05 tu, ndiyo yaliyopendekeza muundo wa serikali moja!

SURA YA 5 CHANGAMOTO ZA MUUNGANO

Katika nyakati tofauti za uhai wake, Muungano wetu umekumbwa na changamoto nyingi za aina mbalimbali, kuanzia changamoto za kidiplomasia; zikifuatiwa na changamoto za kifedha; changamoto za hujuma kutoka kwa maadui wa Muungano; na changamoto kubwa zaidi ya ubishi usiokwisha juu ya muundo uliopo wa serikali mbili, ambao unaendelea hadi sasa.

5.1 Changamoto za kidiplomasia

5.1.1 Kuathirika kwa Uhusiano na Ujerumani

Kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwezi Januari 1964, nchi ya Ujerumani Mashariki (ilivyokuwapo wakati huo), ilifungua ubalozi wake Zanzibar. Kabla ya Muungano, Ujerumani Magharibi (kama ilivyokuwa wakati huo) ilikuwa na ubalozi wake nchini Tanganyika.

Katika kipindi hicho kulikuwa na uhasama mkubwa baina ya Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi, kiasi kwamba, ilikuwa haiwezekani kwa nchi hizo mbili kuwa na Mabalozi wao katika nchi yoyote ya kigeni.

Kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozifanya kuwa ni nchi moja, nchi hizo zote mbili za Ujerumani zikajikuta zina Balozi zao nchini Tanzania, jambo ambalo kumbe lilikuwa ni mwiko kwao. Ujerumani Magharibi ikajaribu kumshinikiza Rais Nyerere afunge ubalozi wa Ujerumani Mashariki uliokuwa Zanzibar.

Rais Nyerere alikataa shinikizo hilo. Matokeo yake yakawa ni kwamba, kwa hasira zake, Ujerumani Magharibi ikasimamisha utoaji wa msaada waliokuwa wanaendelea kuutoa kwa Tanganyika kwa ajili ya kuunda Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Mashinikizo hayo yalimuudhi sana Rais Nyerere. Akaitaka Ujerumani Magharibi iondoe mara moja misaada yake mingine yote iliyokuwa ikiitoa kwa Tanzania, na siyo kuondoa msaada kwa jeshi peke yake. Tukio hilo liliathiri mahusiano baina ya Tanzania na Ujerumani Magharibi.

5.1.2 Kuathirika kwa Uhusiano na Marekani

Baadaye tena mnamo mwezi Novemba 1964, Waziri wa Mambo ya Nje Oscar Kambona alitangaza kugunduliwa kwa njama aliyodai kuwa ilikuwa inasukwa na Marekani kwa lengo la kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kambona alidai kwamba, sababu ya Marekani ya kutaka kufanya hivyo ni kutokana na hofu yao kwamba, kwa kupitia Zanzibar, nchi za kikomunisti zilikuwa zinajiandaa kuongeza nguvu zake katika eneo lote la Afrika Mashariki na Rais Nyerere alikuwa anaelekea kuwanyamazia!

Serikali ya Marekani ilikanusha madai hayo, lakini, tukio hilo liliathiri mahusiano ya nchi yetu na Marekani.

5.2 Changamoto za ndani (Kero za Muungano)

Changamoto za ndani ya nchi zinajulikana zaidi kwa jina la “kero za Muungano,” ambazo zimesababisha malalamiko mengi kutoka pande zote mbili za Muungano, hali ambayo imeweka doa katika Muungano wetu. Zifuatazo ni baadhi ya kero hizo. Tayari nimekwishakuelezea ile changamoto ya ubishi uliojitokeza kwamba, Zanzibar haijawahi kuridhia Mkataba wa Makubaliano ya Muungano. Hii ilikuwa ni changamoto kubwa, kwa sababu, kama nilivyokwishaeleza, kutoridhia Mkataba huo, ni jambo linalobatilisha kuwapo kwa Muungano wenyewe.

Ni jambo la kushukuru sana kwamba, hatukufika kwenye hatua hiyo. Changamoto nyingine zilizowahi kujitokeza, ni pamoja na hizi zifuatazo:

5.2.1 Zanzibar kukosa uhusiano wa kiuchumi na nchi za nje

Malalamiko yanayoitwa ‘kero za Muungano’ yamekuwa yakitolewa na pande zote mbili za Muungano. Kubwa zaidi, kwa upande wa Zanzibar, ni madai kwamba, kuwapo kwake katika Muungano huu kumeikosesha Zanzibar fursa ya kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na nchi za nje katika masuala ya kiuchumi; kama vile fursa ya kupata misaada na mikopo kutoka nchi za nje, au kutoka katika mashirika ya kimataifa. Lalamilo hili lilijitokeza kwa nguvu sana wakati Zanzibar ilipozuiwa kujiunga na chombo kinachoitwa Organization of Islamic Conference (OIC). Maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Mnamo mwezi Desemba mwaka 1992, vyombo vya habari vilitangaza kwamba, Zanzibar ilikuwa imejiunga na chombo hicho cha kimataifa, kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Tatizo la kikatiba lilitokana na kwamba, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haikuwa na sifa ya kujiunga na chombo hicho, ambacho uanachama wake uko wazi kwa nchi zile tu ambazo zinawakilishwa katika Umoja wa Mataifa (Sovereign States). Ndiyo sababu Zanzibar haikuwa na sifa ya kujiunga na OIC.

Kwa upande wake, Serikali ya Zanzibar haikuridhishwa na hoja hiyo, ikidai kupitia kwa Waziri Kiongozi wa Serikali hiyo, Dk. Omar Ali Juma, kwamba, Zanzibar ni nchi kamili ambayo ina Rais wake, Serikali yake, Bunge lake na pia, Mahakama zake.

Haioni kwa nini isiwe na sifa za kujiunga na OIC. Kutokana na msimamo wake huo, ilikuwa ni kazi ngumu kuishawishi Serikali ya Zanzibar ijiondoe katika uwanachama wa chombo hicho. Lakini, hatimaye Serikali ya Zanzibar ilikubali kujiondoa; kwa mategemeo kwamba, Serikali ya Muungano ingejiunga na chombo hicho. Lakini, Serikali ya Muungano haikupeleka maombi ya kujiunga na OIC.

ITAENDELEA WIKI IJAYO…