Prof. Ndulu: Hii hapa miradi 10 ya kubeba uchumi wetu

16Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Prof. Ndulu: Hii hapa miradi 10 ya kubeba uchumi wetu

“Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hali ya ukuaji uchumi wa Tanzania imeendelea kuwa ya kuridhisha.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji Pato la Taifa unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 katika kipindi hicho cha mwaka jana,” anasema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu.

Anataja sekta zilizochangia katika ukuaji huo ni Kilimo, Biashara, Uchukuzi, Fedha na Mawasiliano.

Hata hivyo, taarifa ya BoT inaonyesha mafanikio ya sasa katika ukuaji uchumi, hayafikii kiwango cha kati ya miaka 2011 na 2014.

Kwa mujibu wa Profesa Ndulu, wakati sekta hizo zilizotajwa zikiwa zinakua kwa wastani wa asilimia 10, yaani katika asilimia 10 na 11, sekta za fedha na mawasiliano zilikuwa kwa kiwango kikubwa zaidi, kwa maana ziliongezeka kufikia wastani zaidi ya asilimia 13.

MIRADI INAYOINUA UCHUMI
Profesa Ndulu anataja miradi mikubwa iliyoinua uchumi nchi kuwa ni ya miundombinu inayoendelezwa kupitia mipango ya serikali.

Anaiorodhesha kuwa ni miradi inayohusu: Ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard gauge); Bomba la mafuta kutoka nchini Uganda hadi Jijini Tanga, ambako inahamasisha upanuzi wa bandari; Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na hasa kituo chake kinachojengwa Kurasini.

Mingine ni Mradi wa Kuzalisha Umeme Megawati 240 Kinyerezi II unaoendelea; na upanuzi wa viwanja vya ndege kama vile wa Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.

“Ujenzi wa maghala ya taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350 yatakayojengwa kwa msaada wa serikali ya Hungary katika sehemu mbalimbali nchini, hususani katika mikoa inayozalisha nafaka kwa wingi,” anasema.

Pia viwanda kipya cha kuzalisha saruji kilichopo mkoani Mtwara na cha kuzalisha mbolea kinachojengwa mkoani Lindi vimekuwa na mchango wake.

Taarifa inataja mkoa wa Pwani ambako kuna viwanda vya kutengeneza marumaru na cha bidhaa za chuma, ni vichocheo vya ukuaji uchumi wa taifa.

“Ni dhahiri kwamba hali ya uchumi wa Tanzania ni nzuri na inatoa matumaini makubwa kwamba shughuli halali za kiuchumi zinaendelea kutekelezwa kama inavyotarajiwa hapo awali, hivyo lengo la ukuaji pato la taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016 litaafikiwa,” anasema Gavana wa BoT.

SEKTA YA FEDHA

Gavana wa BoT anasema hali ya mfumuko wa bei nchini si mbaya sana na iko katika wastani wa asilimia tano 5.5 hadi mwezi Juni mwaka huu na inabashiriwa kufikia wastani wa asilimia tano, ikiwa nafuu zaidi kulinganisha na asilimia 6.8 ya mwezi Desemba mwaka jana.

“Hii ni kutokana na matarajio ya hali nzuri ya hewa utakayochangia kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa bei ya vyakula, pamoja na ongezeko dogo la bei ya mafuta nchini inayotokana na mwenendo wa bei ya mafuta katika soko la dunia na utulivu wa thamani ya shilingi,” inaeleza taarifa ya BoT kuhusu hali ya uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pia kuna tahadhari ya kuzingatia kwamba upungufu wa chakula unaojitokeza katika baadhi ya nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika unaweza kuongeza mfumuko wa bei baadaye.

Profesa Ndulu anafafanua kuwa, sera nzuri za kiuchumi nchini, ndizo zimechangia utulivu katika thamani ya shilingi ya Tanzania.

“Katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2016, Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kiasi cha Shilingi 2,180 hadi 2,190 kwa Dola moja ya Marekani. Hali hii ya utulivu wa thamani ya shilingi kwenye soko huru la fedha, inadhihirisha kuwa sera thabiti za uchumi na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha.”

SEKTA YA BENKI
Gavana wa BoT anazungumzia sekta za kibenki kuwa nazo zina maendeleo mazuri katika miezi sita ya mwanzo wa mwaka huu, hasa kwa kuzingatia kuanzishwa kwa benki mbili.

Aidha, benki za biashara nchini zimesifiwa kwa kasi kubwa ya kuendelea kutoa mikopo ambayo kwa jumla imefikia Sh. bilioni 1,167.2 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka kutoka Sh. bilioni 1,577.5 ya kipindi kama hicho mwaka jana.

Profesa Ndulu anasema maendeleo katika sekta ya fedha yamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na hasa kutoa mikopo inayoibua shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.

“Mikopo mingi kwa sekta binafsi ilielekezwa kwenye shughuli za biashara kwa wastani wa asilimila 19.3,” anafafanua Profesa Ndulu, aliposoma taarifa ya hali ya uchumi iliyoandaliwa na ofisi yake.

Pia, mikopo ya shughuli binafsi za watu ilichukuliwa katika kiwango kinachofanana na ya biashara, ambayo ni asilimia 19.

Sekta zinginezo zilizochukua mikopo na kiwango chake katika mabano ni Viwanda (10.6), Uchukuzi na Mawasiliano (7.9) na Kilimo (7.8).

Kuhusu amana zilizopo kwenye benki, Profesa Ndulu anasema zilipungua katika kipindi cha nusu mwaka inayoishia Juni mwaka huu, kutoka Sh. Trilioni 20.52 hadi Trilioni 20.24, ambayo ni wastani wa upungufu wa asilima mbili.

Lakini katika sura nyingine, mikopo kutoka katika benki hizo kwa wastani kidogo sana cha asilimia 0.025.

“Miongoni mwa sababu zilizofanya zilizochangia kupungua kwa amana kwenye benki ni pamoja na uamuzi wa serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka benki za Biashara, kwenda Benki Kuu,” anasema.

BoT imegusia suala la madai kwamba fedha zimetoweka mikononi mwa watu, ni kwamba shughuli zisizo rasmi ambazo ziko nje ya taratibu za serikali, maarufu kama ‘Misssion Town’ zilishikilia sehemu kubwa ya mzunguko wa fedha na sasa zimedhibitiwa.

Ni aina ya shughuli zilizodaiwa kukwepa kodi na wakati huohuo, zinashikilia mzunguko wa fedha nchini.

VIASHIRIA VYA KUKUA UCHUMI
BoT katika taarifa yake inasema kuwa uzalishaji umeme kitaifa kuongezeka kwa asilimia 14.5 katika kipindi cha miezi sita, ambayo imefikia Kilowati milioni 3,454. 2, imechangiwa na miradi ya gesi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara na kituo cha Kinyerezi, Dar es Salaam.

Uzalishaji umeme utokanao na gesi pekee nao umeongezeka kwa wastani wa asilimia 52 na ongezeko la jumla katika sekta ya umeme inaelezwa kuwa na manufaa makubwa katika uchumi.

Pia, kuongezeka uzalishaji saruji nchini kwa asilimia saba, ambayo inatokana na kuanza kufanya kazi kwa kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichoko mkoani Mtwara.

Kiashiria cha tatu, ni ongezeko la kasi ya kukua uchumi wa nchi kimataifa ambayo ni kwa asilimia 15.

Nne, ni kuimarika kwa makusanyo, usimamizi wa makusanyo ya kodi ndani ya kipindi tajwa cha nusu mwaka.

Tano, ni maendeleo yalionyeshwa katika kasi ya ukuaji wa sekta ya benki nchini.

DENI LA TAIFA
Deni la Taifa hivi sasa limefikia Dola za Marekani milioni 20.851 na inatokana na mikopo mipya ya malimbikizo ya malipo ya madeni.

Pia, serikali ilipokwama na kukopa Hati Fungani za BoT ili kugharami bajeti yake, inaelezwa kuwa chanzo kingine cha deni la serkali, huku misaada na mikopo ya nje nayo imepungua.

L Makala hii imeandaliwa kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Tanzania, iliyowasilishwa na Gavana wa BoT Profesa Benno Ndulu, juzi kwa waandishi wa habari.

Habari Kubwa