Pundamilia wa ajabu aliyepatikana Kenya sasa amehamia Tanzania

08Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Pundamilia wa ajabu aliyepatikana Kenya sasa amehamia Tanzania

PUNDAMILIA wa ajabu ambaye hivi karibuni alionekana katika mbuga ya wanyama ya Mara nchini Kenya, amevuka mpaka na kuingia ndani ya Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti.

Pundamilia wa ajabu aliyeonekana Kenya kwenye Mbuga ya Mara amehamia Tanzania, kwenye Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti. PICHA: MTANDAO

Amevuka mpaka pamoja na pundamilia wengine waliokuwa wanahama wakichanganyika na Nyumbu, limeripoti gazeti la Nation nchini Kenya.

Kinyume na pundamilia wengine wenye mistari, kwenye ngozi yake pundamilia huyo ana madoadoa meupe na mistari michache myeupe inayofifia mwilini mwake, jambo lililomfanya kuwa ni wa kipekee.

Taarifa ya kuhamia kwake nchini Tanzania imethibitishwa na makumi ya watalii na walinzi wa mbuga za wanyama pamoja na katibu wa shirika la madereva wa magari ya utalii nchini Kenya, Felix Migoya.

Migoya amesema kuwa pundamilia huyo mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja hivi, kwa sasa yuko katika eneo la Kaskazini mwa Mbuga ya Wanyama ya Serengeti.

Alipinga taarifa za uvumi kwamba kivutio hicho kipya cha utalii katika Mbuga ya Wanyama ya Mara, kilikamatwa na kufungiwa ili kihifadhiwe mahali pake kama ilivyoelezwa katika mitandao ya habari ya kijamii katika kipindi cha wiki tatu zilizopota, Linaripoti gazeti la Daily Nation la nchini humo.

“Taarifa za mitandao ya kijamii ni feki, pundamilia anayeonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii ni mkubwa na alikamatwa nchini Afrika Kusini katika tarehe ambayo haijulikani, miaka kadhaa iliyopita,” anasema Migoya.

Wazazi wa pundamilia huyo mchanga wako katika kipindi cha mwaka cha kuhama kwa zaidi ya mamilioni ya nyumbu baina ya Mbuga ya Wanyama ya Serengeti na Hifadhi ya Wanyama ya Maasai Mara, tukio ambalo huwavutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Tukio hilo, ambalo liliwekwa katika orodha ya '”Maajabu Saba ya Dunia,” kwa kawaida huanza katikati ya mwezi Juni hadi mwezi Oktoba.

Katika kipindi hiki, nyumbu hukutana kabla ya kufanya safari yao ya kurejea sambamba na mamia ya pundamilia, swala na wanyama wengine wanaotafuta malisho.

Pundamilia huyu wa ajabu mweusi kwa mara ya kwanza aligunduliwa na kupigwa picha mapema mwezi Septemba karibu na mto Mara na Antony Tira, mwongozaji maarufu wa safari za watalii kutoka kabila la Wamasai na alimpiga picha hiyo katika kambi ya utalii ya Matira Bush, iliyopo ndani ya mbuga ya wanyama.

Tira alimuita pundamilia huyo mchanga jina la baba yake ‘Tira.’

UTAMBULISHO WAKE

Si mweusi kabisa, na kutokana na utofauti wa ngozi yake katika sehemu mbalimbali za mwili wake, rangi yake, pundamilia huyo amekuwa maarufu ghafla na amekuwa kivutio cha watalii katika mbuga ya Mara.

Migoya anasema, huenda sasa watalii wakaelekea Serengeti kwani watu wengi wanamfuata kiumbe huyo wa ajabu.

Tangu mpigapicha Tira alipotuma picha ya pundamilia huyo na kuwaalika watu kuja kumuona, watu wengi wamekuwa wakiongezeka katika hifadhi ya wanyama ya Mara na kusababisha ‘msongamano’ mkubwa wa watu katika hifadhi hiyo.

BBC

Habari Kubwa