Raha ya meza ndogo pembeni ya kochi, kitanda

03Sep 2016
Vivian Machange
Dar es Salaam
Nipashe
Raha ya meza ndogo pembeni ya kochi, kitanda

MEZA ndogo pembeni ya kitanda au kando ya kochi lako sebuleni huleta uzuri na kutia nakshi ama chumbani unapolala au sebuleni unapovinjari na kufurahia uzuri wa nyumba yako.

Kama huna meza hizi ukitambua umuhimu wake utashangaa na kujisikitikia ni kwa namna gani uliweza kuishi bila kuwa nazo.

Samani hizi zipo za aina mbalimbali kama kioo, plastiki au marumaru, lakini ukitaka iliyo imara na inayodumu kwa miaka mingi chaguo namba moja ya mbao ngumu.

Mbali na kuwa imara meza hizi za pembeni za mbao zina mvuto na ni rahisi kuzitunza kwa kutumia rangi za mbao na kuzifunika kwa vitambaa zisichafuke na vumbi.

Kikubwa kuhusu meza hizi za pembeni ni kwamba hupendezesha mandhari na kuweka vitu karibu nawe wakati unapumzika.

Kama sehemu ya fenicha za sebuleni samani hizi ndogo zina faida zaidi pale zinapokuwa mwishoni mwa sofa au baada ya kiti jirani na pale unapokaa.

Ni sehemu ambayo unaweza kuwekea kinywaji, kitabu au jarida karibu nawe na kujiondolea usumbufu wa kunyanyuka mara kwa mara. Vilevile kwa upande wa sebuleni unaweza kutumia meza hii kuwekea taa na kuipa sebule mvuto zaidi.

Halikadhalika unaweza kutumia meza ndogo za kando kuwekea mapambo na albamu za picha za kumbukumbu za familia.

Kwenye chumba cha kulala wengi wanapendelea kuweka meza ya pembeni ya kitanda ambavyo ina muonekano sawa na rangi ya kitanda.

Ni samani muurua kwa kuwekea taa unazoweza kuzitumia wakati wowote iwe ukijisomea, kujipumzisha au kufanya chochote ukipendacho kabla hujashikwa na usingizi au kuamka.

Au pia unaweza kuwekea glasi ya maji, kitabu, Korani, Biblia yako na nyimbo za kumsifu Mungu kabla ya kulala.
Simu au kifaa kingine chochote unachotaka kiwe karibu na kitanda chako hapo ndipo pahala pale.

Wakati mwingine baada ya kuperuzi mitandaoni ukiwa kitandani, utahitaji sehemu ya kuweka ‘mpakato’. Meza hizi ndilo eneo la kuweka kompyuta yako ndogo tena ikiwa pembeni yako.

Watu wengi wanatumia saa zenye kengele au simu ziwaamshe ili kuwahi na kujiandaa kwenda kazini.

Sehemu sahihi ya kuweka saa yako au simu yenye kengele ya kukuamsha ni juu ya meza ndogo pembeni yako.

Picha za kwenye fremu na maua ni vitu ambavyo pia vinaweza kuwekwa juu ya samani za pembeni mwa kitanda.

Zaidi ya kuwa inawezekana una fenicha zilizokamilika katika chumba cha chakula, kuongeza meza ya kando ni poa kwa kuwa unaitumia kuweka chupa tupu zinazoendelea kutumika kuweka maji na juisi wakati wa maakuli.

Ni eneo linalofaa kuweka bakuli la matunda na matunda mazima lakini hata maua au pambo uliloondoa mezani wakati wa kula.

Kwenye chumba cha chakula, meza hii ndogo yenye droo inaweza kutumiwa kuhifadhia vitambaa vya meza, visu, vijiko na uma.

Licha ya kuwekwa vyumbani au sebuleni vikiwekwa kwenye korido ni suluhisho la kuhifadhia bila kusahau kupendezesha. Hakika meza za kando zina faida nyingi kwenye kila chumba

Zaidi tembelea www.vivimachange.blogspot.com

Habari Kubwa