Rais Akufo: Tabianchi inakaribisha njaa Afrika

22Mar 2019
Jenifer Julius
Accra
Nipashe
Rais Akufo: Tabianchi inakaribisha njaa Afrika

MATAIFA ya Kiafrika yanaelezwa yako hatarini kukumbwa na njaa, kutokana na mabadiliko ya tabianchi kama hatua ya kupunguza joto la dunia kwa walau nyuzi mbili haitochokuliwa mapema.

Rais Nana Akufo.

Akizungumza jijini hapo, katika mkutano wa Wiki ya Mabadiliko wa Tabia Nchi unaoendelea Accra Ghana , Rais Akufo Addo wa nchini hapo, anasema nchi yake imeamua kuingia katika kampeni kupunguza joto la dunia kupitia sekta ya kilimo.

Anasema, katika utekelezaji wake imewekeza kwenye kiwanda cha kijani, ikianzisha mradi maalum unaojulikana kama ‘One Village One Dam’ (kijiji kimoja bwawa moja) unaolenga kupunguza joto la dunia kupitia kilimo.

Rais Addo anasema, ni mradi utakaohakikisha zaidi ya miti milioni 20 itapandwa na vijana nchini kwake, ili kukabiliana na mabadiliko hayo, ambayo ni tishio kwa dunia kwa jumla.

“Mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa katika kufikia mipango ya malengo endelevu ya dunia (SDG’s), kwa kuwa inasababisha kuwapo majanga kama vile kuchafuka kwa bahari, mafuriko na ukame,” anasema Rais Akufo.

Nchi za Afrika, zinaelezwa kuathitika sana kwa sababu uchumi wake haujitoshelezi kupambana na mabadiliko hayo ya tabia nchi na hazina uwezo wa kukabiliana na mabadiliko hayo vilivyo.

Rais Addo amezitaka nchi za Afrika kutenga bajeti za kutosha, kukamilisha utekelezaji miradi yake inayolenga kupunguza joto la dunia.

Anasema, mabadiliko ya tabia nchi pia yanatishia ukuaji uchumi, hivyo anazitaka nchi za Kiafrika kufuata Mkataba wa Mazingira wa Paris, kuhusiana na upunguzaji wa joto la dunia.

Waziri wa Mazingira wa Ghana, Frimpon Baoteng, anasema mabadiliko ya tabia nchi ni changamoto kubwa inayosababisha ukame na kukauka kwa mito mikubwa nchini kwake na Afrika.

Wakati nchi za Afrika zikijadiliana namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, inaelezwa majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira ni mkubwa sana katika sehemu nyingi.

Hivi karibuni, zaidi ya watu 300 nchini Msumbiji walipoteza maisha, kutokana na mafuriko, huku nchi za Zimbabwe na Malawi zikiathiriwa na kimbunga cha kitropiki.

Habari Kubwa