Rais Museveni na mwarobaini wa maendeleo barani Afrika

31Aug 2016
Raphael Kibiriti
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Museveni na mwarobaini wa maendeleo barani Afrika

AFRIKA ni miongoni mwa Bara ambalo bado liko nyuma kimaendeleo.

Rais Museveni.

Kuna viashiria vingi vinavyotumika kulionyesha hilo la Afrika kutopiga hatua za kimaendeleo, lakini kwa zaidi ya miaka 50 ya kujitawala viashiria vitatu vimetumika zaidi, kabla ya vingine kuibuka.

Tunaweza kuviita viashiria hivyo kuwa ni vya kiasili ama kitamaduni, kwa bara hili kwa kuwa vimejulikana tangu enzi, kwa jina lake maarufu la maadui wa maendeleo, yaani umaskini, ujinga na maradhi.

Hata hivyo, suala la utawala bora kwa muda mrefu limetajwa kuchangia kuendelea kuwapo kwa maadui hao, katika kipindi chote cha miaka 50 ya kujitawala kwa bara hili.

Kwamba, kutokana na watawala kutowajibika kikamilifu kwenye eneo la utawala bora, ndiyo maana bado nchi za Kiafrika, hazijaweza kuwashinda maadui hao.

Katika jitihada mbalimbali za kuwakabili kikamilifu maadui hao, na kuliendeleza bara hili, ndiyo maana basi zikaja na Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM Forum).

Wiki iliyopita, viongozi wa nchi za Kiafrika walikutana jijini Nairobi, nchini Kenya, kwenye Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Mpango huo wa Kujitathmini Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum).

Kuna mambo yaliyonifanya niandike makala hii kuuangazia mkutano huo, lakini mawili ya msingi ni pamoja na vikwazo 10 vilivyoainishwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kuwa ndivyo vinavyolikwamisha bara hili, kupiga hatua za kimaendeleo.

Rais Museveni alivieleza vikwazo hivyo kwenye wasilisho ama mada yake aliyoitoa kwenye mkutano huo, ambayo kwa mujibu wa maelezo yake, inatokana na tathmini yake ya kuangalia matukio ya maendeleo katika bara hili kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Rais Museveni, ameitawala Uganda kwa takribani miaka 30 hadi sasa.

Na suala la pili lililonifanya niuangazie mkutano huo ni kitendo cha viongozi waliokusanyika kwa ajili ya mkutano huo kukubaliana kwa kauli moja kuitumia mada hiyo iliyotolewa na Rais Museveni, kama dira ya kulikomboa bara hili kutoka kwenye giza la umaskini, ujinga na maradhi na kulipeleka kwenye ustawi.

Mkutano huo uliwahusisha karibu viongozi wote wa Afrika, akiwamo Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais John Magufuli.

Mkutano uliongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

“Nimejaribu kuchukua baadhi ya mawazo ambayo yamesababisha sisi tuendelee kuwa nyuma kimaendeleo, mawazo ambayo yanaonekana kugusia maeneo yote kwa mapana yake,” alisema.

VIKWAZO VYENYEWE

Kwa mujibu wa Rais Museveni, vikwazo vinavyolikwamisha Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo ni pamoja na kwanza suala la kuchanganya itikadi, kitu ambacho alisema huzaa ubinafsi uliokubuhu.

Lakini pia udhaifu kwa baadhi ya mataifa ya bara hili, na tatu rasilimali watu duni katika nyanja mbalimbali kama vile taaluma na afya.

Kikwazo cha nne alichokitaja Rais Museveni ni miundombinu hafifu na hasa ya umeme, barabara, reli, usafiri wa anga na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) ambayo inawafanya wawekezaji wasivutike kuja kuwekeza.

Aidha alitaja pia suala la uhaba wa viwanda unaozilazimisha nchi za Kiafrika kusafirisha malighafi kama kikwazo cha tano, ikiwa ni pamoja na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa Afrika, kama kikwazo cha sita.

Akataja vilevile uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli, kama kikwazo cha saba.

Lakini pia kilimo duni kusichotumia mbolea, dawa za kuua wadudu, ukosefu wa mbegu za kisasa, pamoja na kukosekana kwa kilimo cha umwagiliaji, kama kikwazo cha nane.

Aidha Rais Museveni alitaja kikwazo cha tisa kama ni cha makosa ya kisera kwenye maeneo kama vile ubinafsishaji au utaifishaji wa mali zinazomikiliwa na sekta binafsi.

Na mwisho akataja suala la ukandamizaji wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma, kama miongoni mwa vikwazo zinavyolifanya bara hili kutopiga hatua kubwa za kimaendeleo.

UFAFANUZI

Akiongelea kuhusiana na udhaifu wa baadhi ya nchi za Kiafrika, Rais Museveni alisema nchi hizo zinajulikana kutokana na aina ya majeshi zinazoyaunda.

“Zinajenga majeshi ya kikabila…Ukitaka kujenga jeshi na ukaangalia watu wa kabila lako, ni muhimu ukijiuliza kama jeshi la kikabila linaweza kuheshimika nchi nzima,” alisema na kuongeza:

“Sasa katika mazingira kama hayo, ukikumbana na ka-upinzani kadogo, jeshi zima linadondoka, na kisha unaomba Jeshi la Umoja wa Mataifa (UN), ambalo kimsingi hilo ni jeshi la watalii,” alisema.

Kwa upande wa uduni wa rasilimali watu, Rais Museveni aliipongeza Jumuiya ya Kimataifa kwa kulizungumzia hilo, lakini akaongeza kuwa udhaifu wa hatua hiyo ni kulijadili nje ya vikwazo vingine.

Rais Museveni akasema katika mada yake hiyo kuwa, washirika wengi wa maendeleo, hawakuwa wanajali kujenga miundombinu barani Afrika, na hasa ya umeme na hivyo kusababisha kikwazo kingine cha miundombinu.

“Hawa ‘wakubwa’ hawajali kujenga mabarabara ama reli, na matokeo yake ni Afrika Kusini na Libya tu chini ya (Kanali Muammar) Gaddafi, ndizo nchi zilizokuwa na matumizi makubwa ya umeme,” alisema na kuongeza:

“Na la muhimu, uduni wa miundombinu unasababisha ughali wa kufanya biashara, na kwa hali hiyo huwezi ukavutia uwekezaji… Sasa kama hilo huwezi, unatarajia utaondoa vipi umaskini wa watu wako, kama hawaajiriwi,” alisema

Akafafanua kwamba, kutokana na udhaifu wa miundombinu, kinachofuata ni kushindwa kuanzisha viwanda, hali iliyolifanya Bara la Afrika, kuwa muuzaji wa malighafi nje na hivyo kuchangia mapato makubwa kwa nchi za Magharibi.

Alitolea mfano wa nchi yake ya Uganda, ambako kilo moja ya kahawa ghafi inayouzwa nje ya nchi, hununuliwa kwa dola moja ya Marekani, ama shilingi za Kitanzania takribani 2,200 katika soko la dunia, wakati kahawa iliyosindikwa huuzwa kwa zaidi ya dola 14, ama zaidi ya shilingi 30,000 za Kitanzania.

Na kutokana na hilo, Rais Museveni akasema kwamba, Waafrika walikuwa ni wafadhili wa kweli kwa wazungu na kwamba, kwa bahati mbaya walikuwa wanatoa hata ajira zao pia kwa hao hao wazungu.

Kwa upande wa uduni wa sekta ya huduma, Rais Museveni alifafanua kuwa, hiyo ilitokana kwa sehemu kubwa na kutangazwa vibaya kwa Afrika.

Na hiyo alisema inatokana na vita vinavyoendelea kwenye baadhi ya mataifa ya Kiafrika, ikiwa ni pamoja na miundombinu duni miongoni mwake.

Alifafanua, hali hiyo inasababisha wataalamu kuikimbia Afrika na hivyo kuathiri sekta za utalii, elimu, afya, benki, miongoni mwa nyingi.

KILIMO

Kwa upande wa kilimo, Rais Museveni alisema, mtazamo wa biashara kama kawaida unaoharibu sekta ya kilimo, unajenga kikwazo kingine na kwa hali hiyo, alisema inabidi upigwe vita.

Aliwaambia viongozi wenzake kuwa, wakulima wengi katika ukanda wa tropiki, walikuwa wakiendelea kuzalisha kwa ajili ya kujikimu na si kibiashara.

“Ni muhimu kilimo kiwe cha kisasa, na kwa kweli tunapaswa kuongelea usalama wa vipato, na siyo usalama wa chakula,” alisema.

Ufafanuzi mwingine alioutoa ulihusiana na sekta binafsi akisema imedhoofishwa na kudhulumiwa kwa njia ya sera, na akataja kama zile sera za mtangulizi wake, rais wa zamani wa Uganda, Iddi Amin alipowafukuza Wahindi, au kupitia rushwa.

Akaongeza, nchi nyingi zinazoinukia kiuchumi za Bara la Asia, maarufu kama Asian Tigers yaani Singapore, Malaysia na Korea Kusini, zimeendelea kutokana na kuiruhusu sekta binafsi kufanya kazi.

Aidha alihitimisha ufafanuzi wake kwa kuzungumzia juu ya suala la demokrasia.

Hata hivyo kwa hili akasema, nchi nyingi za Kiafrika, zimelishughulikia suala hili kwa ukamilifu wake, na demokrasia ilikuwa inachanua barani kote.

WATAKA MADA IWE YA BARA

Suala la kuichukua mada hiyo ili iwe ya Bara zima, ilipendekezwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, na kuungwa mkono kwa kauli moja na viongozi wa nchi zingine waliokuwapo.

Awali, Marais Macky Sall wa Senegal na Ellen Johnson Surleaf wa Liberia, walizungumzia kuiunga mkono mada hiyo.

Rais Zuma alisema, kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Kiafrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakaozipitia zote, na kuanisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi, na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama.

Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka Sekretarieti ya APRM kupitia vikwazo hivyo na kuwakilisha mapendekezo ya nini cha kufanywa ili kuondokana na vikwazo hivyo, kwenye kikao chao kijacho kitakafanyika nchini Ethiopia.

APRM KUFANIKISHA TANZANIA YA VIWANDA

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Magufuli alisema, Tanzania iko tayari kujifunza kutoka nchi nyingine ambazo ni mwanachama wa mpango huo wa APRM, ili iweze kuboresha hatua ilizozifikia kwenye mpango huo.

Alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada ya Rais Museveni kwenye mkutano huo wa 25 wa mpango wa kujitathmini kiutawala bora barani Afrika.

“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba, Tanzania imeshaanza kutekekeleza mpango kazi kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu, kama zilivyoainishwa kwenye kikao hiki cha APRM,” alisema na kuongeza:

“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele mpaka kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021, ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” alisema.

Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU), kilichofanyika nchini Ethiopia.

Mapema akifungua mkutano huo, Rais Kenyatta alisema, viongozi wa Afrika, hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.

Alisema nchi wanachama wa mpango huo, hawana budi kujenga umoja kama njia mwafaka ya kufikia makubaliano hayo.

Swali linalobaki kwa sasa, ni je baada ya mada hiyo iliyowasilishwa na Rais Museveni kufanywa kuwa ya bara la Afrika, ndiyo mwanzo wa safari ya maendeleo kwa bara hili lililoachwa nyuma kimaendeleo kwa siku nyingi? Tusubiri na tuone!

Habari Kubwa